Haleluya,

Miezi michache iliyopita nyuma, nilipatwa na shida kidogo ya kuumwa, na kilichokuwa kinauma sana ilikuwa ni kichwa. Wakati naumwa kichwa nilitamani kufanya mambo kadhaa ya kutumia kufikiri ila sikuweza.

Wakati mwingine nilitamani kusoma Neno la Mungu, ila nilikuwa nashindwa hata kuangalia maandishi ya biblia. Ni kama ilikuwa mchezo fulani ila sikuweza hata kusoma mstari mmoja, kichwa kilikuwa kimenikamata kisawasawa.

Wakati ambao nilianza kuwaza mengi sana, nikaona kumbe ipo siku ingekuja nisingeweza kufanya haya yote niliyokuwa nafanya hapo kabla sijapata shida! Muda mwingine niliona kama ni nafasi ninayo ya kufanya kile nataka, kumbe unakuja wakati nitatamani kufanya jambo fulani ila sitoweza kulifanya.

Niliona hata ule uwezo wa kufikiri umepungua kabisa, kwa jinsi kichwa kilivyokuwa kinauma. Yaani hata ningefanikiwa kusoma mstari mmoja ile kutengeneza tafakari kwa kile nakisoma kwenye biblia nilikuwa siwezi kabisa.

Hivi ndivyo inaweza kumtokea mtu yeyote yule katika maisha yake, unaweza usiumwe kama mimi ila likatokea jambo ambalo litakufanya usiweze hata kushika biblia yako. Utajaribu kufanya hivyo ila hutoweza kutokana na mazingira magumu uliyopo, unaweza kukamatwa na mahangaiko ya moyo wako kiasi kwamba usiweze kupata utulivu wowote.

Upi wakati unafaa kusoma Neno la Mungu? Wakati ni sasa, tena sasa hivi. Ukisubiri uwe na nafasi sana ndipo uweze kusoma Neno la Mungu, hiyo nafasi hutakaa uipate maishani mwako, unaweza kufikiri nakutania ila kuipata nafasi ya kusoma Neno la Mungu inaweza isipatikane. Ila ukitaka nafasi ya vitu vingine unaweza kuipata kirahisi mno.

Leo husumbuliwi na kitu chochote, upo mzima wa afya, akili zako zinafanya kazi vizuri, unaweza kujiamlia jambo lolote na ukalifanya. Nakusihi sana ndugu yangu usome Neno la Mungu, hakuna wakati mwingine utaupata nje na huu ulionao sasa.

Leo si unasema kazi za ofisini zinakubana sana, subiri ufukuzwe kazi uwe na muda wa kutosha wa kukaa nyumbani uone kama utakuwa na uwezo wa kushika biblia yako. Jambo rahisi tu kufikiri, wakati huna kazi ulikuwa na muda wa kusoma Neno la Mungu? Ukute hata huo muda ulikuwa huna kabisa.

Kuna vitu tunaweza kusingizia sana kuwa vimetubana, ila ukija katika ukweli unaona sio kweli kabisa. Ukitaka kujua sio kweli subiri upatwe na jambo ambalo litaondoa kabisa uwezo wako wa siku zote, sio kukutisha nataka kukusaidia kufikiri zaidi.

Leo una macho yote mawili, inaweza kutokea bahati mbaya ukapoteza hayo macho. Vitu ambavyo ulitakiwa kuvifanya wakati unaona, unaweza usiweze tena kuvifanya kutokana na shida ya macho. Hapo ndipo utakapokumbuka wakati unaona, wakati ambao ulikuwa na nafasi ya kufanya mambo mengi lakini hukufanya.

Kaa utulie ufikiri vizuri, weka akiba leo ya kutosha, Neno la Mungu likae kwa wingi ndani ya moyo wako. Ikitokea siku huwezi kufanya vile ulikuwa unafanya, uwe na akiba ya kutosha, uwe na hazina ikayokusaidia kuishi vizuri wakati huwezi kufanya chochote.

Tunaweza kufananisha hili kama mkulima anavyofanya wakati wa mavuno, lazima ajiwekee akiba ya kutosha wakati wa mavuno. Ili itakapofika wakati usio wa mavuno awe na uwezo wa kula chakula bila mahangaiko yeyote.

Wakati ulionao sasa ni wakati wa mavuno, vuna kadri ya uwezo wako wote, ili itakapofika wakati usio na mavuno, uwe na uwezo wa kustahimili ukame. Linaweza lisikuingie vizuri hili ila likikufika ndio utaelewa nilikuwa nakueleza nini, vizuri usisubiri ufikie huko.

Mpaka hapo utakuwa umepata kitu cha kukusaidia kusonga mbele katika usomaji wako wa Neno, usiishie kusema kweli bwana. Nenda katika vitendo halisi, soma Neno la Mungu kwa umakini na kujitoa haswa pasipo kukwamakwama.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.

Facebook: Chapeo Ya Wokovu

Blog: www.chapeotz.com

Email: chapeo@chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081