Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa Bwana ametupa kibali cha kuweza kuiona siku hii njema.
Wengi tunaanza kusoma Neno la Mungu kwa bidii sana, ila inapofika katikati ya safari, tunaanza kurudi nyuma taratibu. Hii inawakumba wengi sana katika hili la kusoma Neno la Mungu kila, siku.
Tusikubali kusema ni mingiliano tu ya mambo/maisha, tufike wakati tujue sababu zinazotufanya tuwe na hamu Mwanzoni ila inapofika katikati ya safari tunaona haina haja tena kuendelea mbele.
Tukishajua sababu itatusaidia kila mmoja wetu kuweza kujipanga vizuri, ili isije ikafika mahali hata wewe uliyekuwa mwenye bidii ukaishia njiani. Vipo vitu vidogo vidogo ambavyo huwa tunavipuuza ila vina mchango mkubwa sana kuua bidii zetu.
Uwezakano upo kabisa jinsi tunavyochukulia Neno la Mungu ikawa ni sababu ya kurudisha nyuma, wakati mwingine tunafikiri ni rahisi tu kusoma Neno la Mungu. Ndio maana tunapokutana na changamoto kidogo tunaamua kuishia njiani. Lazima tufike mahali tujipange vizuri katika hili la kusoma Neno la Mungu, bila hivyo tutakuwa tunapiga danadana.
Kabla ya kuingia kwenye usomaji wa Neno la Mungu, jua kuna changamoto na vipingamizi vingi katika hili. Kuna wakati unaweza kusoma na usielewe chochote ulichokisoma, hapa unapaswa kuwa makini, huenda wakati unasoma ulikuwa umechoka sana au wakati unasoma hukuwa kwenye utulivu mzuri.
Unaweza kulalamika kila siku mbona huelewi unachosoma, kumbe sababu inayokufanya usiweze kuelewa ni kule kuchoka kwa akili na mwili. Unapoona umechoka ni vyema ukapata muda mchache wa kupumzika, au ukiona ukipumzika unalala moja kwa moja, vyema ukapanga muda mzuri wakati akili yako bado ina nguvu.
Usikubali kuanza vizuri kusoma Neno la Mungu alafu baada ya muda unaona huwezi kuendelea tena, tafuta dawa ya kukosa hamu ya kuendelea kusoma maandiko matakatifu. Na sio kuacha kabisa kusoma Neno la Mungu bila sababu ya kueleweka sana.
Nimeona wengi sana wanaanza vizuri kusoma Neno la Mungu kwa bidii sana, ila baada ya muda mfupi wanapotea kabisa au wanapoa kabisa unafikiri sio wale wa mwanzo. Hii inaletwa na mchanganyiko wa mambo mengi katika maisha, sasa wewe usikubali kujiingiza katika kundi la kushindwa moja kwa moja.
Jua mapungufu yako yapo wapi, ili uweze kukabiliana nayo na sio kukwepa. Hii itakupa nafasi ya kuwa msomaji mzuri sana wa Neno la Mungu, asiyeweza kurudishwa nyuma na jambo lolote lile linalokuja mbele yake.
Usiwe mtu wa kulipukalipuka kwa jambo linalogusa moyo wako, yaani usisubiri kusikia mhubiri fulani akikuambia kusoma Neno la Mungu ni jambo la muhimu sana. Alafu ukishasikia hivyo unaanza kutafuta Biblia yako ilipo, unaanza kusoma Neno la Mungu kwa kasi kubwa sana, lakini baada ya muda mfupi unarudia maisha yako ya kutokusoma Neno.
Ukishaamua kuwa msomaji wa Neno la Mungu, amua kweli kutoka ndani ya moyo wako, bila kuangalia marafiki zako watakutia moyo au watakukatisha tamaa. Wewe simama upande wa kusoma Neno la Mungu, hii iwe ratiba yako ya kila siku, haijalishi hujisikii vizuri. Wala haijalishi unajisikia vibaya, wewe soma Neno la Mungu kwa bidii zako zote.
Ukishajijengea utaratibu huu wa kila siku, taratibu utaanza kuona mabadiliko ndani yako, kimwili na kiroho. Hata wale marafiki zako waliokuzoea wataanza kukuuliza maswali, maana wataanza kuona vitu vya tofauti kwako.
Usirudi nyuma kwenye hili zoezi la kusoma Neno la Mungu, hakikisha unabanana hadi tone la mwisho. Bila kuangalia changamoto ngumu unazopitia, elewa husomi Neno la Mungu kwa sababu una maisha mazuri au una maisha magumu. Unasoma Neno la Mungu kwa sababu ni chakula chako cha kiroho.
Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Facebook: Chapeo Ya Wokovu
Blog: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081