Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa Bwana ametupa kibali cha kuweza kuiona tena. Sifa na utukufu tumrudishie yeye Bwana mwenza wa yote, karibu sana tujifunze pamoja.
Zipo tabia za asili ambazo mtu anaweza kuzaliwa akafundishwa au akajifunza, na akaanza kuziishi kutokana na mazingira yanavyomtaka aishi. Wazazi/walezi/majirani wanaweza kuwa sehemu ya mtoto wao kuwa jinsi walivyo kutokana na tamaduni zao.
Tabia ya mtu yeyote iwe nzuri au mbaya, haioti kama uyoga, tabia inatengenezwa ndani mwa mtu. Inaweza ikapandwa mbegu ndogo ikakuzwa kidogo kidogo kadri siku zinavyo kwenda mbele ikazaa matunda. Yaani jinsi mtu yule anavyozidi kukua na akaona kuishi tabia ile haina shida ndivyo atakavyokuwa katika maisha yake.
Tunaweza kuwa watu wazima na si watoto, ila tukaingiza tabia mpya kabisa kutokana na mazingira na watu tunaoishi nao. Wakati mwingine kutokana na imani tuliyonayo kwa hao watu, ikatufanya tuige tabia zao na kuanza kuziishi sisi.
Inakuwa nzuri sana kama utakuwa umeiga tabia njema, na itakuwa mbaya sana kama umeiga tabia mpya na mbaya, huku moyoni mwako ukifikiri ni tabia njema inayompendeza Mungu wako.
Unapokuwa umeokoka, unapaswa kujichunguza kila mahali kuhusu tabia zako, upo uwezekano mkubwa umeokoka lakini bado una tabia za asili zinazowakera wengine. Na ambazo zimekuwa kikwazo kwa ndugu wa kiroho, sio kwamba ni vita vimeinuka juu yako na wala sio uelewa mdogo wa watu. Maana hilo nalo linawezekana pia kutokana na maarifa waliyonayo hao watu.
Lakini zipo tabia mbaya sana unaweza kuziona ni nzuri ila sivyo hivyo jinsi unavyoziona. Hili utajua pale utakapoingiza maarifa mapya ndani yako, yaani kuona kwako tabia uliyonayo sio njema. Utaona pale utakapopata maarifa sahihi ya kukuingia kabisa ndani ya moyo wako.
Maarifa haya ni Neno la Mungu au mafundisho sahihi ya Neno la Mungu, haya ndio yatakuondoa kwenye giza la kukufikirisha upo sahihi kumbe haupo sahihi. Ukishajua tabia uliyonayo ni mbaya, na kero kwa wengine, itaanza kugeuka kero kwako. Hapo ndipo itakuwa rahisi kwako kuanza kumwomba Mungu akufungue kwenye kifungo cha tabia mbaya.
Unapoambiwa soma Neno la Mungu kwa bidii zako zote, usifikiri tu kwa upande mmoja, hili jambo limeshika kila eneo la maisha yako ya kiroho na kimwili. Kuna maeneo mengine yanaweza yasionekane kwa haraka, pia kuna maeneo huwezi kusikia yakizungumzwa sana. Kupitia usomaji wako wa Neno la Mungu, unakuwa unajengwa taratibu kiasi kwamba ni ngumu kwa mazingira ya kawaida kutambulika.
Kujifunza kwako Neno la Mungu kunaweza kukuondolea tabia moja mbaya sana na uliyoizoea kuiishi ukijua ni tabia njema kabisa. Inaweza kuchukua muda kuzoea kuishi tabia mpya, ila vyema kuchukua muda kuizoea tabia mpya na njema. Kuliko kuishi kwenye tabia mbaya isiyompendeza Mungu na jamii inayokuzunguka.
Utajuaje tabia uliyonayo nayo ni njema au ni mbaya? Utajua kwa kujifunza maarifa sahihi ambayo yanapatikana ndani ya Neno la Mungu. Huenda hapo ulipo ni mkristo wa siku nyingi sana na una cheo kikubwa kanisani kwako, lakini ukawa na tabia ambayo uliibeba kwa rafiki yako unayemwamini. Kumbe haikuwa tabia njema ya kuibeba na kuanza kuishi nayo.
Leo amua kufanya uchunguzi wa kina kwa kumruhusu Roho Mtakatifu, uchunguzi huu utaambatana na kuanza kujaza maarifa ya Neno la Mungu. Unaweza usielewe sana hili ninalokueleza, ila nikuombe uendelee kutafakari taratibu utaona mengi sana, ambayo wakati mwingine huwa unamhuzunisha Roho wa Mungu.
Nina imani kuna kitu umekipata, hicho kitu ulichokipata jaribu kukiweka katika matendo, utaona matokeo mazuri katika maisha yako ya kiroho.
Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Facebook: Chapeo Ya Wokovu
Blog: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081