Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa Bwana ametupa kibali cha kuweza kuiona tena. Tunapaswa kuitumia vyema fursa hii kumzalia Bwana matunda yaliyo mema.

Kuna mawazo unaweza kuwa nayo, kwa kupandikizwa, ukabaki kuyashikilia na kuyaishi kama sehemu ya maisha yako. Hasa hili la kuokoka, wengi wakishaingia kwenye wokovu hujivalisha joho la uchanga wa kiroho. Na wengine huvalishwa joho hili na waliokoka siku nyingi sana.

Leo naomba nikusaidie hili, alafu utajiangalia mwenyewe unafaa kuendelea kusingizia wewe bado ni mchanga kiroho. Na una tofauti na aliyeokoka siku nyingi au wote mpo sawa, ila utofauti wenu ni muda wa kuingia ndani ya wokovu.

Uchanga wa kiroho una madaraja yake, unaweza kuona wewe ni mchanga wa kiroho kwa kujiona umeokoka siku sio nyingi. Lakini kupitia kujiona hivyo, ukaweka bidii katika eneo uliloona una udhaifu, siku sio nyingi ukatoka kwenye uchanga huo.

Usikatae kuwa wewe si mchanga wa kiroho, unaweza kuwa ni ukweli kabisa wewe ni mchanga. Ila usitumie kivuli hicho kuwa mzembe kwenye baadhi ya maeneo.

Unaweza kufikiri huwezi kuelewa maandiko matakatifu kwa sababu umeokoka juzi. Ukashikilia msimamo huo bila kukaa chini ujue unachofikiri Kinaweza kukuletea faida yeyote, au kitaendelea kukuweka eneo lile lile la udhaifu wako.

Roho Mtakatifu akiwa ndani yako, unayo silaha muhimu tayari kukusaidia kuelewa maeneo ambayo kwa akili za kawaida huwezi kuelewa chochote. Hii inakuja unapokuwa na bidii katika kujifunza Neno la Mungu.

Unayelalamika huna muda mrefu kwenye wokovu, huna tofauti na mtu aliyeokoka miaka mingi sana alafu akawa hasomi Neno la Mungu, yaani wewe na yeye mpo sawa kabisa. Kama huwa unajiwazia kuwa umepitwa mengi na waliokoka siku nyingi, upande mmoja unaweza kuwa sawa na upande mwingine unaweza usiwe sahihi kabisa.

Kwa mtazamo huu wote wasio na muda wa kusoma Neno la Mungu, ni wachanga bado wa kiroho, bila kuangalia wamekaa ndani ya wokovu miaka mingapi. Wanaweza kutembelea uzoefu wa baadhi ya maeneo, lakini wakawa dhaifu sana kwenye maeneo mengi.

Usijipe sana sababu unapoona uvivu umekukamata, usianze kufikiri ni kwa sababu ya uchanga wa kiroho, hilo ni tatizo la wengi walikoka siku nyingi. Pamoja na kuokoka kwao siku nyingi, kusoma kwao Neno la Mungu ni mtihani kwao, ndio maana unaweza kutazama matendo yao yakakataana kabisa na kile wanasema wameokoka muda mrefu.

Haijalishi muda uliopo ndani wokovu, anza kujizoeza kusoma Neno la Mungu, hata kama unaona ugumu kwenye baadhi ya maeneo. Hakikisha unakataa unyonge wote unaotaka kukufanya usiendelee kusoma Neno la Mungu, taratibu utaanza kuona unafunguka kwenye eneo uliloona ni gumu kwako.

Miaka mingi ya kuokoka haimfanyi mtu kutoka kwenye uchanga wa kiroho, kama mtu huyo hatakuwa na bidii ya kujifunza Neno la Mungu. Neno la Mungu ndio chakula pekee cha mkristo kinachoweza kumtoa gizani kwenye maeneo mengi ambayo alikuwa mchanga, bila kutazama dhehebu lake.

Umeokoka leo au umeokoka siku nyingi, wote tunapaswa kusoma Neno la Mungu, nje na hapo hutokuwa na tofauti na aliyeokoka Leo na aliyeokoka siku nyingi.

Msingi wetu ni Neno la Mungu, tunapaswa kulisoma kwa nguvu zote huku tukimwomba Roho Mtakatifu atusaidie kuelewa yale tunayosoma. Tusisome kama tunasoma vitabu vingine, tusome kama tunasoma kitabu kitakatifu cha Mungu.

Bila shaka, hadi hapo hutokuwa na sababu ya kuendelea kutokusoma Neno la Mungu. Anza na udhaifu wako huohuo, taratibu utaanza kuona mabadiliko ndani yako.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.

Facebook: Chapeo Ya Wokovu

Email: chapeo@chapeotz.com

Blog: www.chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081.