Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa Bwana ametupa kibali cha kuweza kuiona tena. Haijalishi ulipo unapita kwenye jambo fulani gumu, umepata fursa ya kuiona siku pamoja na yule ambaye anajiona yupo vizuri. Kwa hiyo wote tumeingia siku ambayo hakuna aliyewahi kuingia, vizuri ukajiona mtu wa pekee anayependwa na Mungu.

Wapo watu waliotutangulia kiimani, wameona mengi, wamekutana na changamoto nyingi katika maisha yao ya wokovu. Kwa mtazamo huu tunaweza kusema wanaufahamu mkubwa wa mambo mengi, na wakati mwingine tunaweza kuwaona ndio suluhisho la maswali mengi yanayotusumbua/yanayotutatiza vichwani.

Tunaweza kuwa sahihi kabisa, ila tunapaswa kuelewa baadhi ya maeneo ili tusije tukawa tunajifariji mtu fulani akituambia jambo fulani linakuwa sawa. Kumbe aliyekuambia mwenyewe hakuwa na maarifa sahihi ya Neno la Mungu, ila kutumia uzoefu wake wa miaka mingi aliopo ndani ya wokovu akakulisha tango pori bila hata yeye kujua.

Tango pori ni Neno lolote lisilo sahihi, haijalishi unajua kuwa sio sahihi au haujui kabisa kuwa hilo ulilosema halikuwa sahihi. Fahamu kwamba ni tango pori.

Tunaweza kujenga dhana hii ya kuwaamini sana watu, upande mmoja tunaweza kuwa sahihi kutokana na sababu hii. Watu wale wanakuwa wameokoka siku nyingi, sio siku nyingi tu, wanakuwa na umri mkubwa, na ni wazee wetu. Hapa uwe na uhakika Neno atakaloongea utaliamini sana kutokana na imani kubwa uliyonayo kwake.

Je tuache kuwaamini wazee wetu au wazazi wetu wa kimwili/kiroho? La hasha ninachotaka ukielewe ni hichi hapa;

Wengi wetu tunaishi kwa mapokeo yasiyo sahihi, na wala hatuna mpango wa kujifunza zaidi ili kujiondoa kwenye mapokeo hayo. Kama ilivyo kwako unaona uvivu kusoma Neno la Mungu, wapo nyuma yako walio wavivu zaidi yako, na hawana mpango kabisa wa kusoma Neno la Mungu.

Kutokujua Neno la Mungu, hilo watu hawalioni kama ni tatizo kwao kutokana na wanaona hawatendi dhambi zile maarufu zinazofahamika sana na wengi. Ukichanganya na wameishi ndani ya wokovu kwa miaka mingi, wanaona wamejua kila kitu haina haja tena ya kuongeza mengine.

Hapo ndipo shida ilipo, hebu fikiri umekutana na mtu wa namna hii niliyokueleza sasa hivi. Yaani mtu asiyejua Neno la Mungu alafu yupo kwenye dini kwa muda wa kutosha, sema mwenyewe bila kukwepesha kitu.

Unaweza kuona kwa upande mwingine tunahitaji msaada mkubwa sana katika hili, hatuwezi kuishi kwa kuamini watu kwa kila jambo. Ndio maana tunapaswa kuwa watu wa kufuatilia Neno la Mungu linasemaje, tena hatulifuatilia kwa mitazamo yetu, tunapaswa kuongozwa na Roho Mtakatifu. Na ili uongezwe na Roho Mtakatifu ni sharti uwe umejazwa.

Dawa wa hili ni kusoma Neno la Mungu, ukishajaa Neno la Mungu utaona mwenyewe jinsi unavyocheua. Kufikiri kwako kutabadilika kabisa, hata jinsi unavyozungumza utaonekana ni mtu mwenye maarifa sahihi ya Neno la Mungu.

Sikuambii uache kuuliza waliokutangulia katika imani, wala sikufundishi usiwe na imani kwa wazazi wako wa kiroho. Unachopaswa kujua na wao ni wanadamu, wana mapungufu kama yako. Ila Mungu amewaweka hapo kwenye nafasi walizonazo na anajua wanatufaa, je wanapoacha kuisema kweli ya Mungu huwa tunajua?

Kuna wakati wanaweza kukengeuka wakaiacha kuisema kweli, bila sisi kujua tukawa tunaendelea kuwaamini. Kumbe tayari wameshafarakana na Mungu wao, kama huamini angalia wana wa Israel kwa mfalme wao Sauli.

Mungu akusaidie uweze kuelewa vizuri haya niliyokueleza hapa.

Chapeo Ya Wokovu

chapeo@chapeotz.com

www.chapeotz.com

+255759808081