Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa Bwana ametupa kibali cha kuweza kuiona siku ya leo. Fursa kwetu kwenda kumzalia Bwana wetu Yesu Kristo matunda yaliyo mema.

Vipo vituko vingi sana ambavyo wanadamu huwa tunavifanya tukifikiri tunamkomoa mtu, kumbe huwa tunajikomoa wenyewe pasipo kujua kuwa tunajirudisha nyuma.

Wakati mwingine tunaona Neno la Mungu halipandi kabisa, na wakati mwingine tunaweza kujiona hatuwezi kulielewa vizuri Neno la Mungu. Na kuna wakati mwingine tunaweza kujiona ule utamu unaozungumzwa, hauwezi kuwa kwetu.

Tunaona hayawezi kuwa kwetu kwa sababu tunasoma Neno la Mungu Kwa maigizo, wakati mwingine tunataka tuonekane kwa wenzetu kuwa tupo vizuri kwenye kusoma Neno la Mungu.

Kusoma mtu anaanaweza kuwa anasoma vizuri kabisa, ila akili yake ikawa haipo kwenye Neno la Mungu kabisa. Ni sawa na mtu anayetimiza wajibu tu ila moyoni mwake hana msukumo wowote wa kufanya hivyo.

Mtu wa namna hii, wa kusoma Neno la Mungu bila msukumo wowote ndani yake, hawezi kuchukua muda mrefu ataacha kusoma hata kwa kidogo alikoanza nako. Maana ndani yake hafanyi kwa kuwa anaelewa anachofanya, hii ipo tofauti kabisa na mtu anayeona Neno la Mungu ni gumu.

Hakuna tofauti na mtu asiyejua kusoma kabisa, ila kila siku unamwona anaenda kununua gazeti, alafu wakati anasoma anajisahau kuwa ameligeuza hilo gazeti juu chini. Hao ndio watu wa maigizo, watu ambao wanafanya vitu ili waonekane ila mioyoni mwao hawana msukumo wowote wa kufanya.

Tunaweza kuigiza sana mambo mengi, ila kwenye Neno la Mungu jitahidi usilete maigizo. Najua maigizo haya yana maeneo mengi sana katika maisha ya mwanadamu, yapo maigizo ya kujionyesha una furaha wakati moyoni una maumivu makali, yapo maigizo ya kujionyesha unaishi vizuri sana. Lakini ndani yako unaugua usiku na mchana, uitafuta amani ya kweli lakini huipati.

Maigizo mengine yana faida kwa mtu, ila yapo maigizo mengine yanazidi kumdidimiza mtu chini. Kama haya mtu kuigiza anasoma Neno la Mungu, kumbe anafanya hivyo kwa maslahi yake binafsi. Ambayo hayamfikishi popote pale.

Ukitaka kufikia lengo lako katika hili la kusoma Neno la Mungu kila siku bila kuona mzigo wowote, acha ujanja ujanja. Amua kweli kutoka ndani ya moyo wako, bila kuangalia nani anakutazama, bila kuangalia nani atakupongeza kwa maamzi uliyochukua.

Chukulia hili jambo kama ulivyofanya maamzi ya kuokoka, wakati unaokoka si ulifanya uamzi mwenyewe bila kusukumwa na mtu yeyote? Basi na hili la kusoma Neno la Mungu huenda umekutana na mtu akakueleza faida nyingi za kuwa na Neno moyoni mwako. Basi ni vizuri baada ya kumsikiliza, fanya maamzi mwenyewe bila kusukumwa na mtu yeyote yule.

Utaona vitu vya tofauti sana katika usomaji wako wa Neno la Mungu, tena hutakaa uone ukubwa wa biblia kutokana na utamu unaoupata kwenye maandiko matakatifu. Shida tunaona Neno la Mungu ni kama mzigo kwa sababu hatujawa tayari mioyoni mwetu.

Usiigize hili la usomaji wa Neno la Mungu, hilo eneo la kuigiza waachie wengine ambao hawajaamua kumfuata Yesu Kristo katika roho na kweli. Kiri moyoni mwako kabisa, kuwa husomi Neno la Mungu ili uonwe na fulani, unasoma Neno la Mungu kwa faida yako mwenyewe.

Mungu akufungue ufahamu wako uweze kuelewa zaidi umhimu wa kusoma Neno la Mungu.

Nakushukuru kwa muda wako uliotumia kusoma ujumbe huu, endelea kufuatilia masomo haya kila siku utaondoka na maarifa mengi ya kukusaidia kujiweka vizuri katika usomaji wako wa biblia.

Chapeo Ya Wokovu

chapeo@chapeotz.com

www.chapeotz.com

+255759808081