Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, Mungu wetu ni mwema sana ametupa kibali kingine tena cha kuweza kuiona siku ya leo. Sifa na utukufu tumrudishie yeye Bwana mwenza wa yote.
Unapoona mkristo yeyote amejawa na ujasiri mkubwa, ujasiri unaompa nguvu ya kufanya vitu bila hofu yeyote. Uwe na uhakika mtu yule amekomaa kiroho na anatambua kwanini awe jasiri, na asiwe myonge.
Unapoona mkristo yeyote amejawa na hofu nyingi, na anashindwa kufanya vitu vitakavyomsaidia kwa siku za baadaye kwa kuogopa kuingia hasara. Uwe na uhakika mtu yule hana maarifa sahihi ya kutosha ndani yake.
Ukijiona binafsi huwezi kuwekeza pesa yako mahali ambapo utaanza kuvuna matunda yake baada ya miaka miwili au mitano ijayo. Uwe na uhakika huna Neno la Mungu la kutosha ndani yako, ama huna maarifa sahihi ya watumishi wa Mungu.
Wakati mwingine wakristo tunashindwa akili hata na watu wasiomjua Mungu wa kweli, hii ni kutokana na kutopenda kutafuta maarifa sahihi yatakayotusaidia kwenye maeneo mbalimbali ya maisha yetu.
Maarifa mengi sana yanapatikana ndani ya vitabu, vipo vitabu vizuri vinavyoweza kukutoa hatua moja kwenda nyingine. Na ukajiona ni mtu wa tofauti kabisa, na wakati mwingine vinaweza kukuamsha kwenye usigizi mzito uliokuwa nao.
Vitabu hivi vya watu wa dunia, sio vyote vinaweza kukufaa, unapaswa kuwa na Neno la Mungu la kutosha ili usije ukapotoshwa. Neno la Mungu linakusaidia kuchuja maarifa yapi ya kuchukua na yapi ya kuacha.
Jambo lingine la muhimu zaidi, ni kujua msingi wako mkuu unapaswa kuwa kwenye Neno la Mungu. Neno la Mungu limebeba maarifa yote ambayo tungesema ukusanye vitabu vya kuyapata hayo maarifa, ingekuwa ngumu sana kuvipata vyote.
Tunaposoma vitabu vingine vya watumishi wa Mungu, vinatuongezea uelewa zaidi wa yale tuliyosoma ndani ya biblia. Kama ulisoma habari za damu ya Yesu Kristo, ukipata kitabu cha watumishi mbalimbali wanaoelezea hiyo habari. Ufahamu wako unapanuka zaidi ya mwanzo, maana unajifunza kwa namna gani watu wengine waliona mengine zaidi. Ambayo huenda wewe hukuweza kuyaona kwa wakati huo.
Leo biblia inafundisha namna ya kuanzisha biashara, kwa kutegemea kupata faida kwa baadaye. Kwa maana nyingine tunaweza kusema tunafundishwa namna ya kuwekeza sasa, ila matunda yake tutapata kwa siku za baadaye.
Hapa tunaweza kutumia mfano wa mkulima, mkulima anapanda mbegu leo hategemei kuvuna siku hiyo hiyo, ana mategemeo ya kuvuna siku zijazo.
Uwe na uhakika sio kila Mbegu unayopanda utaweza kuvuna, wakati mwingine unaweza kuingia hasara kabisa. Pamoja na kuingia hasara, bado hatupaswi kuogopa, maana Neno la Mungu linatupa nguvu ya kufanya hivyo.
Najua unaweza kuona haya hayapo ndani ya biblia takatifu, leo unaenda kuona hili alafu ubaki mwenyewe uamue kusoma Neno la Mungu. Ili uendelee kujipatia maarifa mengine mengi zaidi au uamue mwenyewe kuishi kwa kubahatisha.
Nimejaribu kupitia biblia moja yenye kiswahili cha zamani na kiswahili cha sasa, yaani kiswahili cha kisasa zaidi. Nimependa kiswahili cha biblia ya habari njema, hii biblia haina tofauti yeyote na biblia ya swahili Union version. Ila hii ya kiswahili cha kisasa imefafanua kwa kiswahili kirahisi mno huu mstari ninaoenda kukupatia hapa.
Nia yangu ni uelewe jinsi gani Neno la Mungu lilivyobeba maisha yetu, binafsi nimechota kitu kikubwa ambacho naenda kukitendea kazi kwa bidii kubwa.
Rejea:Jishughulishe na biashara hata kama kwa kubahatisha; yawezekana baadaye ukapata chochote kile. Mhubiri 11:1 BHN
Utaamua mwenyewe kuendelea kukaa bila kujishughulisha au utaamka hapo ulipo ukajishulishe, Neno la Mungu limemaliza kila kitu. Ni wewe sasa kuamua kunyanyuka ukafanye kazi, kafanye kazi halali utapata faida. Hata kama uliwahi kufanya ila ukaacha ulivyoingia hasara, kafanye tena.
Acha kulalamika maisha magumu huku umelala kitandani, amka kafanye kazi, kukaa unaomba Mungu akupe pesa alafu hufanyi chochote huko ni kukosa maarifa. Omba Mungu huku unaendelea kujishugulisha, Mungu atakuinua kwenye hicho hicho kidogo unachofanya.
Haijalishi unapanda leo kwa machozi mengi ya huzuni, amini wakati ukifika utavuna kwa machozi ya furaha nyingi.
Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Facebook: Chapeo Ya Wokovu
Email: chapeo@chapeotz.com
Blog: www.chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.