Nakusalimu katika jina kuu la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai sasa na hata milele. Siku nyingine tena mpya kabisa Bwana ametupa kibali cha kuweza kuiona tena, sifa na utukufu tumrudishie yeye Bwana mwenza wa yote.

Hakuna mwisho wa kujifunza, hakuna mwisho wa kutungwa vitabu, kadri siku zinavyozidi kwenda mbele. Watumishi wa Mungu na watu wa dunia hii wanapata mafunuo mbalimbali ya kuandika vitabu vingine vya kufundisha maeneo fulani katika maisha yetu.

Kinachofanya watumishi wapate kuandika vitabu vingine vipya kila wakati ni Neno la Mungu, kadri mtu anavyosoma Neno la Mungu kila siku. Kuna somo anapata la kuweza kuwashirikisha wengine ambao hawakuweza kuona kile amekiona ndani ya biblia.

Unaweza kufikiri umesoma sana vitabu vingi, na ukafikiri hakuna usilolijua kuhusu vitabu. Ila kama ni msomaji wa vitabu, utagundua ladha mpya za waandishi mbalimbali jinsi Roho Mtakatifu alivyowaongoza kuchimbua vitu ambavyo hukuwahi kufikiri haraka.

Maisha yako yote unaweza kuchagua kusoma vitabu mbalimbali jinsi Mungu atakavyokujalia kufanya hivyo. Ila shida inakuja pale kama utakuwa msomaji mzuri wa vitabu, ila unayojifunza ndani ya vitabu huyafanyii kazi.

Unaweza kuonywa sana na kuelekezwa sana namna ya kuenenda maisha matakatifu, lakini ukawa hufanyi hivyo. Huko ni Kuuchosha mwili bure. Maana hakuna mwisho wa kutungwa vitabu, utaendelea kusoma sana na kujua mengi, ila kama hutochukua hatua ya kuyaweka katika matendo ukayaishi. Itakuwa kazi bure na Kuuchosha mwili wako bure.

Kusoma sana kunachosha mwili na akili, hili lipo wazi na wote mnaosoma sana vitabu mtaungana nami katika hili. Kama inachosha mwili kusoma, alafu ukawa huyafanyii kazi yale unayosoma, ina faida gani kuendelea kusoma vitu ambavyo haupo tayari kuviishi?

Unapaswa kufikiri hili jambo vizuri, tunajifunza kila siku ndani ya kitabu kitakatifu cha biblia, kuwa uzinzi na uasherati ni dhambi. Lakini pamoja na kujifunza hayo yote, bado unaendelea kufanya uchafu huo.

Unasoma uongo ni dhambi, ila huachi kudanganya wenzako kila siku, tena unafanya hivyo kwa makusudi kabisa na imekuwa kama mfumo wako wa maisha. Huko ni Kuuchosha mwili wako bure kusoma vitu ambavyo haupo tayari kuviishi.

Unajifunza kila siku uwe na bidii kwa mambo ya Mungu, pamoja na kujua mambo mengi ila wewe ndiye unayeongoza kwa uvivu. Na kuweka sababu nyingi za kutokuwa na bidii. Bora kuacha kujifunza maana unauchosha mwili wako bure alafu hakuna unalofuata hata moja.

Umejifunza mengi sana kuhusu umhimu wa kusoma Neno la Mungu, lakini wewe ndiye unayeongoza kwa uzembe wa kupuuzia kusoma Neno la Mungu. Kujifunza kwako sana hakukusaidii kitu chochote, na unaweza kuamua kuendelea kujifunza, ila huko ni kuuchosha mwili wako bure.

Rejea:Tena, zaidi ya hayo, mwanangu, kubali maonyo; hakuna mwisho wo wote wa kutunga vitabu vingi; na kusoma sana huuchosha mwili. MHU. 12:12 SUV

Kubali maonyo na mahusia yaliyo ndani ya biblia yako unayoisoma kila siku, yale unayojifunza ndani ya biblia takatifu. Hakikisha unayaweka katika matendo, yaishi yale unayosoma kila siku, nasema yageuze yale unayojifunza yawe ndani ya moyo wako. Hapo ndipo utaona matunda yake, utajiona una tofauti na mwanzo.

Vinginevyo utasoma sana Neno la Mungu, lakini utashangaa bado unashindwa kusamehe, utashangaa bado unashindwa kuwa mkweli kwa wenzako. Na utashangaa umeokoka ila bado unateswa na kumbukumbu mbaya za nyuma, huko ndipo tunasema ni Kuuchosha mwili wako bure bila faida yeyote. Maana hakuna ukomo wa maarifa sahihi.

Somo hili linakuhusu msomaji wa biblia au vitabu mbalimbali vya watumishi wa Mungu, hakikisha matendo yako yanafanana na yale unayojifunza. Hasa Neno la Mungu, hili halina onyo ambalo utasema hupaswi kuliishi wewe, kila onyo linafaa kuzingatiwa ndani biblia.

Mungu akubariki sana kwa muda wako. Karibu group la whatsApp tujifunze Neno la Mungu pamoja kama bado hujajiunga.

Facebook: Chapeo Ya Wokovu

Email: chapeo@chapeotz.com

Blog: www.chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081