Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa Bwana ametupa kibali cha kuweza kuiona tena.

Madhara ya uchanga wa kiroho yanaweza yasionekane sana kwa watu wengi waliokoka, na wakati mwingine inaweza isichukuliwe kama changamoto. Ambayo kila mmoja anapaswa kupigana kwa hali zote kuhakikisha anatoka katika eneo hili la uchanga.

Kutokujua kwetu kuwa hili ni tatizo, tunaendelea kuishi na changamoto hii ambayo mwisho wake sio mzuri kabisa kwa mwamini. Kwa mtu aliyeamua kuachana na maisha ya dhambi na kuishi maisha matakatifu.

Uwezakano upo hujawahi kufikiri madhara ya hili jambo, ila leo ninaenda kukuonyesha jinsi linavyoweza kukuletea shida. Kama utaweza kuchukua hatua zozote za kukuondoa kwenye uchanga huo wa kikiroho, uweze kujiondoa haraka iwezekanavyo.

Unapokuwa umeokoka miaka mingi alafu ukawa huna Neno la Mungu la kutosha, bila shaka utakuwa na mapungufu mengi sana. Mapungufu hayo yatakupelekea kutenda matendo ambayo wakati mwingine ni chukizo kwa Mungu wako.

Unaweza kujishangaa kabisa unakosa ujasiri wa kumweleza rafiki yako habari njema za Yesu Kristo, aibu inaweza kukutalawa kiasi kwamba ukashindwa kabisa kusimama mbele za watu hata wawili kuwaambia uzuri wa Yesu Kristo.

Sio ajabu ukahalalisha dhambi kwa aibu uliyonayo, sio ajabu ukashindwa kuwaambia marafiki zako ukweli kutokana na lile mbaya wanalolitenda. Sio ajabu ukaulizwa umeokoka, ukakataa kuwa hujaokoka.

Unaweza kufikiri bora kutetea uhai wako kuliko kulitaja jina la Yesu Kristo, na ukajiona upo sawa kabisa kwa kufanya hivyo. Bila kuelewa ulichofanya ni kibaya mno mbele za Mungu.

Kushindwa kwako kukemea dhambi kwenye kizazi hichi kilichojaa maovu, kwa kufikiri marafiki zako watakutenga, hakuwezi kukuacha salama siku ya hukumu. Kwako unaweza kuona haina madhara sana, ila ina madhara makubwa ndio maana unasikia dhamiri inakushtaki ndani yako.

Haikusaidii chochote wala haikuongezei kitu kuonea injili haya, unaweza kusema nikimwambia huyu aache kutenda dhambi atanichukia. Kweli upo sahihi kwa mawazo hayo, ila hiyo ni mbinu mbaya kwako, tena ni mtego mbaya sana kwako aliokuwekea shetani.

Unavyojitoa na kujiweka pembeni ili usionekane mbaya kwa watu wanaomtenda Mungu dhambi, unawaacha ili mwendelee kuwa marafiki mnaopendana sana. Huo sio upendo, ni ujinga ambao shetani ameutumia kama nafasi ya kuwahifadhi wabaya wake.

Upo kanisani na unaongoza kundi lolote, unaona hilo kundi linapotea alafu huliambii ukweli, kwa kuogopa kuchukiwa na watu. Huko ni kujitafutia matatizo mbele za Mungu, maana kitendo hicho kinamchukiza sana Mungu.

Wakati mwingine tumezoea kuona ukiwa mtenda dhambi huwezi kumkemea mtenda dhambi mwenzio, sasa ipo nyingine ya kukosa ujasiri wa kumweleza rafiki yako anachofanya ni kibaya na anapaswa kuacha.

Neno la Mungu linakuondoa wasiwasi na kukujaza ujasiri mkubwa sana, maana unakuwa unajifunza ahadi za Mungu mbalimbali juu ya maisha yako. Ambazo hizo ahadi huwezi kuzipata ukiwa umekaa tu bila kujishughulisha na jambo lolote linalokufanya ukue kiroho.

Kama unajijua huwa unamwonea Yesu Kristo aibu, tena wakati mwingine ukibanwa vizuri kwenye kona. Unaruka kabisa kuwa hujaokoka, usifikiri hilo unalolifanya ni nzuri sana kwako.

Leo nataka nikuonyesha madhara ya unachokifanya, kwa sababu usipojua unaweza kuja kushangaa siku ya mwisho mbona sikujua haya.

Rejea: Maana kila mtu atakayenionea haya mimi, na maneno yangu, katika kizazi hiki cha uzinzi na dhambi, Mwana wa Adamu atamwonea haya mtu huyo, atakapokuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika watakatifu. Marko 8:38 SUV

Wakati wenzako wanakemea uovu, unawaona wamekosa kazi za kufanya, kisa unaona aibu/haya kufanya kama wao. Usifikiri upo salama sana, utapendwa sana na waovu, ila utakuwa sio rafiki wa Yesu Kristo.

Wakati unaona cheo chako na elimu yako ni ya maana sana kuliko Yesu Kristo aliyekuokoa kwa gharama kubwa. Unajidanganya mwenyewe, huko ni Kujitengenezea mazingira mabaya.

Ukijiona unakuwa mwoga sana hata kwa mambo ya msingi, usikubali hiyo hali. Hakikisha unafanya kila njia kutoka kwenye eneo hilo, maana si salama kabisa kwako.

Usiwe miongoni mwa watu wanaopaka dhambi mekapu, kuwa miongoni mwa watu waopasua yaliyo maovu. Haya yote uyafanyayo yafanye kwa hekima ya kiMungu iliyo ndani yako, inayokuongoza katika yote.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.

Facebook: Chapeo Ya Wokovu

Email: chapeo@chapeotz.com

Blog: www.chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081