Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena Bwana ametupa kibali cha kuweza kuiona.

Kila mtu ana ratiba yake inayomwelekeza kufanya yale aliyojipangia kwa siku, hata kama hajaandika vitu katika mtiririko wa kuvifanya siku husika. Kama jambo ni la muhimu kwake, atakuwa na muda wa kulifanya siku hiyo.

Wapo watu wamejipangia ratiba yao, ikifika saa fulani anapaswa kuacha kila kitu na kuingia kanisani. Mwingine amejipangia ikifika saa fulani lazima apate chakula cha tumbo, labda itokee amefunga kama huwa anafanya hivyo.

Wengine wamejiwekea ratiba ya maombi ya pamoja kila siku, wengine wamejiwekea ratiba ya kufanya mazoezi kila siku. Wameweka na muda kabisa, hawezi kupitisha huo muda labda awe amebanwa na jambo la muhimu sana zaidi ya hilo.

Wapo wamejiwekea ratiba ya kuandika makala/ujumbe kila siku inayokuja mbele yao, iwe anaumwa ataandika, iwe mvua ataandika, iwe amechoka sana ataandika, na iwe hajisikii vizuri ataandika tu.

Wapo pia wamejiwekea ratiba ya kusoma Neno la Mungu kila siku, awe amebanwa sana na kazi, atatafuta upenyo wa kusoma, awe amechoka sana atasoma. Ndani ya ratiba ile ameweka nidhamu ambayo hawezi kuivunja mpaka amefanya kile amejipangia.

Pamoja na kujiwekea ratiba, na kuhakikisha ratiba ile unaisimamia vizuri, inafika mahali unakutana na changamoto ngumu sana mbele yako. Changamoto ambazo zinakufanya ukose utulivu mzuri, sio utulivu tu, hata ile hamu ya kuendelea kufanya kile umejipangia inaisha kabisa.

Leo napenda tuzungumzie sana kuhusu kusoma Neno la Mungu, wengi sana wanaanza vizuri kujiwekea ratiba ya kusoma biblia kila siku. Wanaenda vizuri na ratiba yao, ila wanapokutana na changamoto ngumu, ile ratiba yao inaanza kusuasua, mwisho wake wanaacha kabisa kusoma.

Ukweli kuna mambo yanaingilia ratiba zetu, wakati mwingine unakosa kabisa upenyo, ila moyoni mwako unakuwa unajua mahali ulikosea. Ndani ya kubanwa huko unaondoka na somo ambalo kesho huwezi kurudia kosa lile lile kila siku.

Kuna vitu ambavyo vinaweza kutuondoa kwenye utulivu, kama vile; kufiwa, safari ndefu na mengine yanayoweza kujitokeza ndani ya ratiba yako.

Siku zote unapaswa kufahamu kwamba, changamoto huwezi kuziepuka, lazima zije kwa namna tofauti kabisa na ya mwingine. Zinapokujia, hakikisha unatafuta njia nyingine ya kukufanya uendelee kusoma Neno la Mungu.

Ukijidanganya ngoja nipumzike kwanza kusoma Neno la Mungu hadi pale utakapokaa sawa, uwe na uhakika huo ndio utakuwa mwisho wako wa kusoma Neno la Mungu. Zaidi utaendelea kuchoka zaidi kwa sababu unakosa chakula cha kiroho, kuomba kwako kunaweza kuwa vibaya, na imani yako inaweza kushuka kwa kiwango kikubwa sana.

Hakuna kitu kibaya kama kupungukiwa na Neno la Mungu, unapopungukiwa na Neno la Mungu moyoni mwako ni rahisi sana kwako kumtenda Mungu dhambi. Ndio pale utamsikia mtu akisema nilifanya bahati mbaya sikukusudia, kumbe roho ya uasi ilipata nafasi ndani yake bila yeye kujitambua.

Ushauri wangu kwako, kama utakumbana na changamoto inayokuondoa kwenye ratiba ya kusoma Neno la Mungu. Na ukiangalia unaanza kuona kukinai kwako Neno la Mungu kunakujia, usikubaliane na hiyo hali, hakikisha hukosi kusoma Neno.

Utafika wakati unasoma Neno la Mungu, ila unaona haupo kama zamani, hiyo isikufanye uache kusoma Neno la Mungu. Hakikisha unamwambia Mungu akupe utulivu wa moyo wako, huku unaendelea kusoma Neno la Mungu.

Utashangaa badala ya kuendelea kurudi chini, utaona kuinuliwa tena, unaweza usione kwa wakati huo. Ila kadri unavyoendelea kusoma Neno la Mungu, utaona hata ule mzigo uliokuwa nao moyoni mwako unazidi kuwa mwepesi.

Kuacha kusoma Neno la Mungu kwa sababu unapitia mambo magumu, unaonyesha udhaifu mkubwa sana mbele za Mungu. Wakati mwingine imani yako ipo kwenye kipimo, hupaswi kuonyesha huwa unampenda Mungu wakati wa raha, hata wakati wa magumu unapaswa kumpenda Mungu kwa matendo yako.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.

Chapeo Ya Wokovu

Blog: www.chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081