Haleluya,
Tumwamini nani na tusimwamini nani, ni swali linalotesa wengi sana. Maana kila mtu anayekuja mbele yetu anasema Mungu amesema naye. Je nani wa kuamini na nani wa kupuuza kwa maneno yake? Ni ngumu kung’amua kwa haraka hili jambo.
Wengi sana tumekuwa tunapelekeshwa na upepo wa manabii wa uongo tukisema wametoka kwa Mungu, na wengine tumekuwa tukiwapuuza manabii wa kweli tukifikiri ni wa uongo.
Tulichobaki nacho ni kubashiri huenda huyu akawa wa kweli, na huenda huyu akawa wa uongo, kwa jinsi anavyoonekana kwa mwonekano wake wa nje.
Changamoto ni kwamba, wa uongo anasema Roho wa Mungu amesema naye, na wa ukweli naye anasema Roho wa Mungu amesema naye. Ni kama mambo yanachanganya hivi, ukijaribu kutulia unaona kabisa mbinguni inakuwa ngumu kuingia.
Kukataa hili ni kujifariji, ila ukweli wengi wameona bora wawe wanaende tu kukusanyika na wenzao. Ila tumaini kabisa la kusema wapo mahali sahihi, wamelikosa kutokana na wametembea madhehebu mengi sana wakaona yale yale, hadi wamefika mahali wamerudi pale pale pa mwanzo.
Haijalishi mwanzo walitoka kwa sababu waliona sio mahali sahihi, wanaona bora warudi tu. Kwao wanaona ni heri wafanye hivyo, na wana sababu nyingi za kufanya hivyo, kutokana na mambo waliyoyaona katika kuingia kwao kwenye dini/madhehebu tofauti tofauti.
Hili jambo Mungu alishaliona mapema na akalitoa tahadhari, kwa sababu hatuna mpango wa kujifunza Neno lake tunajikuta kwenye utata ambao hatukupaswa kuwa nao. Maana tayari tulishapewa njia nzuri ya kuwatambua hawa wanaosema Mungu amesema nao.
Hatuwezi kuamini kila roho, tunapaswa kuzipima kwa Neno la Mungu, Neno la Mungu ndio kipimio chetu kikubwa na cha mwisho kuweza kumtambua kila mtu anayesema ana Roho wa Mungu ndani yake.
Rejea:Wapenzi wangu, msimsadiki kila mtu asemaye kwamba ana Roho wa Mungu, bali chunguzeni kwa makini kama huyo mtu anaongozwa na Roho wa Mungu au la, maana manabii wengi wa uongo wamezuka ulimwenguni. 1 Yohane 4:1 BHN
Wapo watu wanafikiri wamejazwa na Roho Mtakatifu, kumbe sio kweli wamejazwa na Roho wa Mungu, ipo roho nyingine ya mwovu shetani iliyowaingia ndani yao.
Wapo watu wanafikiri mtu fulani anatumia Roho wa Mungu kuwasaidia matatizo yao, kumbe mtu yule amevaa li roho la pepo wa utambuzi. Anayeweza kuona mambo yasiyoweza kuonekana kwa macho ya nyama.
Rejea:Ndipo Sauli akawaambia watumishi wake, Nitafutieni mwanamke mwenye pepo wa utambuzi, nipate kumwendea na kuuliza kwake. Watumishi wake wakamwambia, Tazama, yuko mwanamke mwenye pepo wa utambuzi huko Endori. 1 SAM. 28:7 SUV
Kutokujua kwako Neno la Mungu, anatokea mtu anakutabiria Mambo yanayokusumbua katika maisha yako, unaona huyu ndiye mtumishi wa Mungu wa kweli. Unaanza kabisa kusimlia ndugu na marafiki zako kuwa umekutana na nabii wa kweli.
Wapo pia watu hawatabiri ila wanasema Roho wa Mungu anawatumia kusema nao, na kweli ukiangalia mafundisho yao. Unaona ni sahihi kabisa na Mungu anawatumia kweli, unaona hivyo kwa sababu huna chunjio la kutenganisha majani na chai.
Najua umefika mahali umeona hakuna Mungu, najua umefika mahali umeona hakuna nabii, mtume, mwalimu, mchungaji na mwinjilisti wa kweli. Umeona wote ni waongo tu, sio kweli hakuna mtu wa Mungu anayemtumikia katika roho na kweli, wapo wazuri sana, vile vile wapo wabaya sana wanaopotosha.
Kazi sana kuwatambua kwa macho ya nyama, ila ukiwa na Neno la Mungu la kutosha moyoni mwako, utawambua kwa matendo yao. Utawapima kwa Neno la Mungu lililo ndani yako, ndio utajua yupi anamtumikia Mungu kweli, na yupi anamtumikia baba wa uongo.
Toka njia panda, soma Neno la Mungu kwa bidii zote, hili halihitaji kuumiza kichwa sana, ni wewe kuamua kuchukua hatua sasa.
Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Chapeo Ya Wokovu
Blog: www.chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081