Tunakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, tunamshukuru Mungu ametupa nafasi nyingine tena ya kuweza kusema nawe kuhusu umhimu wa kusoma Neno la Mungu.

Wengi walianza vizuri kusoma Neno la Mungu mwaka ulivyoanza, walipofika katikati ya safari yao, hawakuweza kuendelea na safari yao. Na wapo wengine wameweza kusoma kuanzia January hadi leo tunapoelekea mwishoni mwa mwaka.

Pamoja na juhudi zao za kuweza kufikia siku kama ya leo, wengi hawatamani tena kuendelea na mpango huu wa kusoma Neno la Mungu kila siku. Wameona mioyoni mwao upo umhimu wa kulijua Neno la Mungu, ila ile kiu ndani yao haipo tena.

Wapo walianza safari hii miezi michache iliyopita, baadhi yao waliweza kuendelea hadi leo, na baadhi yao wameshindwa kuendelea kama walivyopanga. Wapo wana miaka miwili sasa tangu waanze mpango huu, na wapo wana miaka zaidi ya miwili, na bado wana kiu ya kuendelea.

Swali linakuja kwako, wewe kama wewe, je unajiona bado una kiu ya kuendelea kusoma Neno la Mungu? Hakuna anayeweza kukujibia swali hili, wewe ndiye unayeweza kujijibu, hahitaji mtu mwingine kujua umepata jibu gani. Inatosha wewe mwenyewe kujijua unajisikiaje ndani yako.

Huenda kweli mlipanga wengi sana kutimiza lengo moja la kusoma Neno la Mungu, wenzako wote mliopanga nao wameona waishie njiani. Umebaki peke yako, kama umebaki peke yako, bado kiu ipo ya kuendelea na ratiba yako au umeona na wewe uache?

Huenda umepata nafasi ya kusoma ujumbe huu, na ulikuwa miongoni mwa watu waliopanga mwaka huu, utakuwa mwaka wao wa kuwa karibu zaidi na Mungu wao. Jambo moja wapo uliloona mioyoni mwao linafaa zaidi kulifanya lilikuwa kusoma Neno la Mungu.

Pamoja na kupanga kote huko, hawakuweza kumaliza hata kitabu kimoja cha Mathayo Mtakatifu, wamebaki wanaiba wataanza kesho, hiyo kesho haijawahi kufika hadi tunaenda kufunga mwaka huu na kuanza mwingine.

Njia nzuri ya kutoka kwenye ahadi hewa, ni kuanza leo, yaani leo hii unapaswa kupanga vizuri ratiba yako. Acha kabisa ahadi hewa, kusoma Neno la Mungu sio kuanzisha biashara useme utaanza ukipata mtaji.

Mungu haangalii ulikuwa mwenye bidii sana mwaka jana, kama mwaka huu utalegea na kurudi nyuma, itakuwa hasara kwako. Maana kinachoangaliwa kwako ni mwisho wako utakuwaje na sio mwanzo wako.

Rejea: Heri mwisho wa neno kuliko mwanzo wake, Na mvumilivu rohoni kuliko mwenye roho ya kiburi. Mhubiri 7:8 SUV.

Usikubali kiu ya kusoma Neno la Mungu ikatike, endelea kuchochea moto wa Roho Mtakatifu ndani yako, ili ukusaidie kukusukuma kufanya mambo yanayompendeza Mungu.

Usije ukawa unaangalia historia njema ya nyuma, wakati huo huna hiyo nafasi tena, haitakusaidia kitu mbele za Mungu. Unapaswa kuwa mvumilivu hata pale unapokutana na changamoto, linda kiu ya kusoma Neno la Mungu isikatike.

Usitazame mlioanza nao wamerudi nyuma na wewe ukaanza kutamani kuwa kama wao, linda mwisho wako uwe mwema. Maana kila mmoja atatoa hesabu yake ya matendo yake, na si kikundi cha watu.

Mungu akubariki sana kwa muda wako, endelea kufuatilia masomo mengine mazuri yanayokujia kila siku.

Chapeo Ya Wokovu

www.chapeotz.com

+255759808081