Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, Mungu wetu ni mwema ametupa kibali kingine cha kuweza kukutana tena mahali hapa.

Katika maisha yako najua umewahi kukutana na changamoto ngumu ambayo ilikufanya ukose usingizi mzuri. Changamoto ambayo kila aliyekufahamu alijua unalopitia kutokana na ukubwa wa jambo lenyewe.

Huenda walijua kupitia wewe mwenyewe ama huenda walijua kupitia marafiki au ndugu zako. Baada ya kufahamu unayopitia, kila mmoja alikuja na ushauri wake, na kila aliyekushauri aliamini ushauri wake ni bora zaidi.

Kila mmoja anaweza kuona ushauri wake ni mzuri sana kutokana na ulimfaa yeye au mtu mwingine aliyemshauri yeye. Ujasiri wa kukuambia na wewe utumie njia aliyotumia yeye, unaweza kuwa mkubwa sana.

Fikiri umekutana na marafiki watano, kila mmoja akakupa ushauri wake, na kila mmoja anaamini ukifuata ushauri wake utakuwa salama kwako. Utachukua upi na utaacha upi, hilo ndio wengi wamepotelea humo baada ya kufuata ushauri mbaya.

Kuna wakati unapaswa kusimama wewe na Mungu wako, serikali yako ndio inatakiwa ikuongoze wakati ambao huoni msaada mwingine zaidi ya Mungu pekee.

Unaweza kushauriwa vibaya mpaka wewe ukaona moyoni mwako ni upotofu, sio kila rafiki anaweza kuwa na imani iliyosimama kwa Mungu kisawasawa.

Wapo watu imani zao ni haba, pamoja na wanasema wameokoka, lakini bado matendo yao yanaonyesha sio watu waliosimama na Mungu wa kweli.

Unaweza kupewa ushauri wa kwenda kutafuta msaada kwa miungu mingine, kwa sababu una shida na umeteseka vya kutosha, na kwa sababu unamwamini na kumweshimu huyo aliyekushauri. Unaona ni heri ukaenda mahali anakuelekeza huyo rafiki/ndugu yako.

Hatuachi kusikiliza ushauri wa wengine, ila tunapaswa kuwa na uwezo wa kuchuja yale tunayoshauriwa. Na tunapochuja tupate yale yanayotufaa kuyatendea kazi, inawezekana pia ukawa na chujio lililotoboka.

Neno la Mungu ndilo linapaswa kukukomaza na kukuweka imara ili uwe na uwezo wa kuchuja mambo vizuri. Wakati unachukua hatua, isitokee ulimkosea Mungu kwa maamzi yako, na isitokee ukapuuza ushauri mzuri ukafuata mbaya.

Isitokee ukatamani kufuata ushauri wa mtu aliyekuambia uende kwa mchawi atakusaidia shida yako, ukaona ushauri wake ni wa maana sana. Ukaamua kumweka Yesu Kristo pembeni na kwenda kufanya yaliyo machukizo kwake.

Jiulize umefuata ushauri mara ngapi ambao ulikuja kugundua mwisho kabisa, hukuwa ushauri mzuri kwako. Tayari wakati huo umemchukiza Mungu wako, na unaona kama vile mbingu na nchi zinakuzomea wewe peke yako.

Unaweza kuwa ulishauriwa vibaya kwenye ujana wako ukaingia ndoa isiyo ya mpango wa Mungu, inawezekana ulishauriwa vibaya ukaingia kwenye biashara ambayo haikuwa sahihi kwako na kwa Mungu wako.

Pamoja na hayo na mengine mengi ambayo ulitambua ulikosea mbele za Mungu, bado unayo nafasi ya kurekebisha hayo kwa kutubu. Muhimu ni umejua mapema kabla upo hai, ni nafasi kwako kurekebisha.

Kuepuka kuingia kwenye mitego mibaya ya mwovu shetani, anayotumia uchanga wetu wa kiroho kutuingiza kwenye mambo yake mabaya. Ni kuamua kulijaza Neno la Mungu mioyoni mwetu kwa wingi.

Neno la Mungu ndilo litakalotusaidia kujua kumsikiliza na kumtii Roho Mtakatifu, vinginevyo tutaendelea kuangamizwa kwa kukosa maarifa sahihi ndani yetu.

Umejua siri ya kukuondoa kwenye uchanga wa kiroho, umebaki wewe mwenyewe kuchukua hatua ya kukusaidia kufikia mahali ukaweza kusimama kwa miguu yako. Katika maeneo mbalimbali ya maisha yako.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.

Chapeo Ya Wokovu

www.chapeotz.com

+255759808081