Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, Mungu wetu ni mwema ametupa nafasi nyingine tena ya kuweza kukutana pamoja.
Kila mmoja anaweza kuwa kiongozi, inategemeana na uongozi wenyewe ni wa namna gani. Unaweza ukawa kiongozi wa maisha yako mwenyewe, unaweza ukawa kiongozi wa familia yako, unaweza ukawa kiongozi wa dini yako, na unaweza ukawa kiongozi mtaa/kijiji chako.
Maeneo ni mengi sana ya kiuongozi ambayo mengine sijayataja mahali hapa, lakini yote yanawakilisha uongozi. Ikiwa utakuwa na nafasi ambayo upo kwa ajili ya kuwasaidia wengine.
Nafasi hizo ambazo wengi wanakuwa nazo katika jamii yetu, kila nafasi ya uongozi huwa ina weka sheria au taratibu za kuweza kusimamia haki za wale anaowaongoza.
Wengi wanakuwa wanatumia nafasi zao vibaya kabisa za kiuongozi, kuwakandamiza wale walio chini kujinuifaisha wao wenyewe. Na wakati mwingine wanabadili sheria zile zilizowekwa ili kuwakandamiza wanyonge haki zao.
Wakijua hata wasipowepo katika nafasi hizo za kiuongozi, hakuna sheria itawahukumu. Maana tayari wamejiwekea kinga za kisheria wakati wa uongozi wao.
Pamoja na mambo yote hayo mabaya wanayowatendea wanyonge yaani watu wa chini yao. Mungu anaona matendo yao mabaya wanayoyatenda juu ya watu wake.
Kupitia Neno lake takatifu, anawaonya wote wenye tabia hiyo ya kupotosha wenye haki wasipate haki yao. Wanaotumia nafasi zao za kiuongozi kuwaumiza wanyonge.
Rejea: Ole wao wawekao amri zisizo za haki, na waandishi waandikao maneno ya ushupavu; ili kumpotosha mhitaji asipate haki yake, na kuwanyanganya maskini wa watu wangu haki yao; ili wajane wawe mateka yao, na kuwafanya yatima waliofiwa na baba zao kuwa mawindo yao! ISA. 10:1-2 SUV
Kama umesoma hayo Maandiko Matakatifu kwa haraka, naomba urudie tena kusoma kwa umakini sana. Mwanzo kabisa inasema hivi; ole wao wawekao amri/sheria zisizo za haki, na waandishi waandikao maneno/makala/machapisho ya ushupavu; ili kumpotosha mhitaji asipate haki yake…
Kazi ipo kwako, Neno la Mungu limeshasema, ndio maana ni muhimu sana kujua Neno la Mungu linasemaje. Kuishi maisha ya wokovu huku ukiendelea kufanya yasiyo mpendeza Mungu, hakuna kisingizio cha kuja kusema sikujua.
Mungu anakuuliza, baada ya kufanya hayo yote duniani, je siku ya mwisho utakuja kufanyaje? Na utamkimbilia nani akupe msaada? Na utukufu wako wa kiuongozi utauacha wapi?
Sio mimi ninayesemayo haya, ni Neno la Mungu linasema haya, ikiwa utaendelea kushapaza shingo yako. Itakuwa ni wewe umeamua, maana tayari umeshajua madhara ya kufanya hivyo.
Rejea: Nanyi mtafanya nini siku ya kujiliwa, na wakati wa uangamivu, utakaokuja kutoka mbali sana? Je! Mtamkimbilia nani mpate msaada? Na utukufu wenu mtauacha wapi? ISA. 10:3 SUV
Nafasi uliyonayo leo, fahamu ni ya hapa duniani, kumbuka siku ya mwisho yaja, utaishi maisha mazuri kwa mali za dhuluma na kupokea rushwa ili upotosha haki za wengine. Fahamu hayo yote ni ya hapa hapa duniani.
Umeokoka na unatamani siku moja ukaishi maisha ya umilele mbinguni, vizuri ukasoma Neno la Mungu na kujua linasema nini juu ya maisha yako. Leo unaweza usiwe kiongozi, ila kesho ukawa kiongozi wa mahali popote pale, ukiwa unajua haya hutotenda mabaya.
Bila shaka umejifunza mambo mengi kupitia ujumbe huu, huu sio ujumbe wa kupotosha kama lilivyosema Neno la Mungu. Huu ni ujumbe wa kukumbusha yale unapaswa kutenda na yale usiyopaswa kuyatenda, ikiwa kuna mahali umeona unaenda kinyume, vyema ukarudi mbele za Mungu na kutubu.
Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Chapeo Ya Wokovu
www.chapeotz.com
+255759808081