Haleluya,

Zipo sababu nyingi sana zinazomfanya mtu arudi nyuma au aache kile alichokuwa anakifanya kila siku, moja ya sababu hizo ni wale wale waliotuvutia kile tunafanya sasa. Ndio hao hao wanatumika kuturudisha nyuma.

Wanatumikaje kuturudisha nyuma? Labda ndio swali unalojiuliza sasa, ni pale wanapoanza kukuvunja moyo kwa kile chema walichokushawishi ukifanye. Kumbe wao tayari hawafanyi na wameshaingia kwenye mambo mengine yasiyompendeza Mungu wao.

Ikiwa walitumika kukushauwishi mambo mazuri, wanataka kukurudia tena ufanye yale wanayofanya wao. Tena wanaweza kuja kwa nguvu ambayo hukutegemea kabisa waje nayo.

Hili lipo hasa kwa watu ambao walikuwa wameokoka, sasa wamerudi nyuma. Hata wale wenzao waliovuta kwa Kristo, wanaanza kuwapa maneno ya kuwafanya waaache wokovu kama wao walivyoacha.

Hii inaenda hata katika bidii ya maombi, unakuta yule aliyekuvuta uwe mwombaji mzuri, ndiye anaanza kutumika kukuvuta nyuma tena. Ukiangalia shida ni nini, unakuta uhusiano wake na Mungu alishaupoteza siku nyingi.

Hili linawapelekea hata wale walioanza vizuri kusoma Neno la Mungu, wanafika mahali wanaacha kabisa kusoma Neno la Mungu. Ukiangalia sababu haswa, unakuta yule aliyemfanya ashawishike kusoma Neno la Mungu, ndiye anayetumika kumvuta nyuma.

Wengine sio lazima waje wakuambie achana na hicho, binafsi ukiwatazama walivyoacha kufanya, na wao walitumika kukuvuta ukawa hapo ulipo. Utaanza kuona ya nini na wewe kuendelea na kitu ambacho aliyekushawishi uingie mwenyewe kwanza hana mpango nacho tena.

Unaweza kuvunjika moyo na kuona haina maana tena, bila kufahamu huyo alitumika kama daraja tu kukuvusha sehemu ulipokwamia. Haijalishi ameacha kusoma Neno la Mungu, kama wewe unaona ipo faida ya kusoma Neno la Mungu, hakikisha huachi kwa sababu yake.

 

Utakuwa ni uchanga wa kiroho kuona hicho unachofanya hakina maana tena baada ya kuona mtu wako wa karibu tena aliyekushawishi ameacha kabisa. Narudia tena, hiyo isikusumbue sana.

Badala yake wewe uwe sababu ya yeye kurudi tena mwendelee na kile mlikuwa pamoja katika kukifanya, isiwe na wewe ukavutika kuingia kwenye upande mbaya.

Mwombee Mungu amsaidie atoke huko alipoingia, ila sio na wewe kumfuata, hata kama unampenda sana na kumkubali. Kwenye uzembe na dhambi hakuna ushirika kabisa, maana kila mtu ataenda kutoa hesabu yake yeye mwenyewe.

Ulianza kurudi nyuma kwa sababu yule aliyekufanya uanze kusoma Neno la Mungu ameacha, kuanzia sasa usifikiri hivyo tena. Uamzi unaotaka kuuchukia haufai kabisa, futa kabisa hayo mawazo.

Mungu akubariki sana.

Chapeo Ya Wokovu

www.chapeotz.com

+255759808081