Kwanini tuwe na mtu anayejua ratiba yetu ya kila siku katika kusoma kwetu Neno la Mungu? Ni swali ambalo unapaswa kujiuliza ili utakapopata majibu yake yawe msaada kwako, na mwingine atakayehitaji msaada wako.

Tunapokuwa na watu wanaojua ratiba au kile tunakifanya kila siku, siku umeacha kufanya hivyo bila sababu yeyote. Watu wale wawe sababu ya wewe kurudi tena kwenye ratiba yako ya kusoma Neno la Mungu.

Mtu huyo anaweza akawa mmoja au akawa zaidi ya mmoja cha msingi ni uwe naye, hata kama hatakufuatilia kila siku. Angalau ajue unachofanya kila siku, na akikuona ukifanya ajue umeshaingia kwenye ratiba yako.

Pale unapopenda kusomea biblia yako, ndio mazingira sahihi kwako watu kujua, maana sio jambo la siri la kusema utajificha mahali ambapo hutaonekana na mtu yeyote.

Mtu wa kwanza kufahamu kama umeoa/umeolewa ni mume/mke wako, huyu ndiye rafiki yako wa karibu sana. Hata kama hajaokoka, wewe ukawa umetangulia kuokoka, kama amekujua upo vizuri na Mungu wako. Lazima kuna baadhi ya ratiba zako atakuwa anazijua, kama huwa una ratiba ya maombi atajua, kama huwa unapenda kusoma Neno la Mungu atajua.

Faida ya kujua mke/mume wako ni hii, siku umeacha kusoma Neno la Mungu jinsi alivyokuwa anakuona mwanzo. Mungu atamtumia huyo huyo kukuuliza mbona siku hizi sikuoni ukisoma Neno la Mungu, unaweza kushangaa imekuaje leo mwenzangu ananiuliza hili swali wakati alikuwa anaonyesha namkera!

Bila kusukumwa na mtu yeyote utashangaa umejisikia vibaya ndani ya moyo wako, kwanza utajiuliza kumbe kuna mtu alikuwa ananifuatilia kwa kile nilichokuwa nafanya. Utajitetea lakini mwisho utaona urudi kusoma Neno la Mungu kama zamani.

Sehemu nyingine nzuri ya kukumbusha ni kuwa na kikundi cha kusoma Neno la Mungu, kikundi hichi kitakuwa kichocheo kwako pale utakaposikia kuacha kusoma Neno la Mungu. Kwa kuwa unapenda kusoma Neno la Mungu, kila utakapoona wenzako wanakazana kufanya hivyo, na wewe utaona huna haja ya kuacha kufanya hivyo.

Pia inaweza kuwa watoto wako waliokuzoea kukuona ukisoma Neno la Mungu, siku umeacha kusoma, utasikia mama/baba mbona siku hizi hatukuoni ukisoma Neno la Mungu. Unaweza kuwaambia Neno lolote la kuwafariji ila moyoni mwako utakuwa umeachiwa jeraha ambalo litakufanya ukumbuke kurudi tena upya kwenye usomaji wako.

Muhimu sana ndugu au marafiki zetu kujua kile tunafanya, sio lazima wawe wengi, hata mmoja tu anatosha maana sio jambo la matangazo kila mmoja ajue kile unafanya. Japo kadri unavyozidi kusimamia ratiba yako ya kila siku, wengi watazidi kujua kile unafanya hata kama wasipokuambia kuwa wameshajua unachokifanyaga.

Hata wale ambao hujui kama wanajua kile unafanya, siku umeacha kusoma Neno la Mungu, watakuuliza mbona hivi. Itakuwa ni swali la kukushtua ambalo kwanza hukulitegemea, pili litakuwa ni swali ambalo litakufanya ukumbuke ulivyokuwa mtiifu katika kusoma Neno la Mungu.

Kuwa na mtu anayekuhimiza kusoma Neno la Mungu, mtu huyo sio lazima ajue kuwa huwa anakuhimiza wewe na anaweza asikujue kabisa. Ila wewe unayemfuatilia lazima uwe unamkubali sana ili anapokueleza umhimu wa kusoma Neno la Mungu iwe rahisi kwako kumtii na kuhamasika zaidi.

Ukishafanya hivyo utaona miaka ikienda mbele bila kuacha kusoma Neno la Mungu, mwisho utajishangaa imekuwa tabia yako ambayo haiwezi kutoka kirahisi. Tofauti na mwanzo ulivyokuwa unajilazimisha kusoma Neno la Mungu.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.

Chapeo Ya Wokovu

www.chapeotz.com

WhatsApp +255759808081