Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai. Ashukuriwe Jehovah kutupa nafasi nyingine ya kuweza kuiona siku ya leo.

Sijui unapita kwenye hali gani ambayo imekufanya mpaka umekosa hamu ya kuutafuta uso wa Mungu kwa bidii zako zote. Unayejua ni wewe na Mungu wako.

Uzito wa jambo na maumivu makali uliyonayo ndani ya moyo wako, ni wewe unaona vizuri kuliko mtu mwingine yeyote yule. Hii ni kwa sababu hatuna kipimio halisi cha kuweza kujua uchungu wa mtu ulivyo ndani yake.

Lipo jambo moja tu, kukimbilia kwa Bwana wetu Yesu Kristo, hakuna mahali pengine sahihi pa kukimbilia. Haijalishi umejiona moyo wako umejaa huzuni nyingi ambayo inakufanya ukose hata ile hamu ya kumtafuta Mungu kwa bidii.

Fahamu kwamba kukosa kwako hamu ya kumtafuta Mungu kwa bidii, haiwezi kubadilisha ukweli kuwa unapaswa kufikiri upya juu ya maamzi yako. Maana anayeweza kukusaidia katika shida yako ni yeye unayemkimbia.

Badala yake sisi tukiwa tunapita kwenye hali fulani ngumu, tunaacha kabisa kujishughulisha na mambo ya Mungu, huko ni kukubali kirahisi kupotezwa na hali mbaya tunazopitia.

Mwingine akiwa kwenye raha hana mpango wowote na mambo ya Mungu, anasubiri pale apoteze furaha yake ndipo akumbuke kuna Mungu. Wakati kulikuwa na uwezekano wa kutosubiri apoteze kwanza vitu fulani kwenye maisha yake.

Mtafute Mungu kwa bidii maadamu bado unapumua, huyu ndiye anaweza kugeuza chochote kile kinachokukabili katika maisha yako. Usikubali kupumbazwa ufahamu wako na hali mbaya ya muda, ukaacha kuutafuta uso wa Mungu kwa bidii.

Usiache kusoma Neno la Mungu kwa sababu una shida, mwenye kuweza kukuondoa kwenye hiyo shida ni Yesu Kristo. Sasa unapomkimbia unataka msaada wapi tena?

Yeye anayeweza kugeuza mauti juu yako, yeye anayeweza kuufanya mchana kuwa giza, yeye aliyezifanya bahari kwa kushusha mvua chini ya ardhi. Je! Atashindwa kushughulika na changamoto ngumu za maisha yetu? La hasha.

Neno la Mungu linasema hivi;

Rejea: Mtafuteni yeye afanyaye Kilimia na Orioni, na kukigeuza kivuli cha mauti kuwa asubuhi, na kuufanya mchana kuwa giza kwa usiku; yeye ayaitaye maji ya bahari, na kuyamwaga juu ya uso wa nchi; Bwana, ndilo jina lake. Amosi 5:8 SUV

Tunayemwamini ni Mungu aliye hai, hatumwamini mungu baali asiyeweza kusema, hatuamini ndama ya kuchonga na madhahabu isiyoweza kusema chochote. Tunamwamini aliyezaliwa kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, akafa na baada ya siku tatu akafufuka.

Rejea:Akawaambia, Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na kufufuka siku ya tatu. Luka 24:46 SUV

Rudi kwa Yesu Kristo, huyu ndiye wa kuutafuta uso wake kwa bidii zote maana anapatikana na anaweza kutusaidia katika shida yetu.

Rejea:Mtafuteni BWANA, maadamu anapatikana, Mwiteni, maadamu yu karibu. ISA. 55:6 SUV

Haleluya, nimetiwa moyo na huu mstari,Mtafuteni BWANA, maadamu anapatikana, Mwiteni, maadamu yu karibu. ISA. 55:6 SUV.

Maneno kama haya yatakutia nguvu pale unapoyasoma, kusoma kwako Neno la Mungu kila siku, inaweza kukufanya ukakutana na andiko zaidi ya hilo kutokana na uhitaji wako.

Badala ya kuachana na mambo ya Mungu wakati unapita kwenye shida, wewe nenda kinyume kabisa. Wakati wote uwe wa kumwendea Mungu wako, haijalishi unapitia nini, usiache ushirika na Mungu wako.

Mungu akubariki sana.

Chapeo Ya Wokovu

www.chapeotz.com

WhatsApp +255759808081