Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai.
Ndivyo tunavyojidanganya kila siku mwaka mpya na mambo mapya, tunaenda na kauli hii kwa miezi michache sana, baadaye tunarudi pale pale kwenye maisha yetu tuliyozoea.
Yapo mambo kweli yanaweza kusubiri hadi mwaka mpya uanze, maana ratiba yake ndio imekaa hivyo, huwezi kuanza leo wakati imepangwa siku maalum ya kuanza siku fulani na mwaka fulani.
Pamoja na hayo, maandalizi yake huwa yanaendelea kila siku ili kufikia siku maalum iliyopangwa, uwe umejipanga vizuri. Ukifikiri vizuri unaona hata hiyo unayoona utaanza mwaka mpya, bado kuna vitu umeshavianza mapema maandalizi yake.
Labda unaweza kuwa unapanga mwaka mpya lazima mtoto wako anze shule, maandalizi yake utaanza leo, kama ni kwenda shule kuuliza taratibu zake, utaanza sasa na sio kusubiri hadi mwaka mpya.
Yapo mambo yenyewe hayahitaji mwaka mpya ufike ndio uanze kufanya, mfano kama umejigundua una tabia fulani sio nzuri. Unapaswa kuanza kujirekebisha sasa, labda huna matumizi mazuri ya pesa, labda huna matumizi mazuri ya muda wako, kama huzipendi hizi tabia hupaswi kusubiri mwaka mpya.
Unapaswa kuanza sasa, kujiondoa kidogo kidogo kwenye tabia usiyoipenda, hadi kufika mwaka mpya utakutwa umeshaanza kuwa mtu wa tofauti kabisa. Wakati wenzako wana shamramra za mwaka mpya na mipango mingi mipya, wewe utakuwa tayari umeanza kuishi malengo yako.
Usijidanganye mwaka mpya naanza kusoma Neno la Mungu kwa kasi mpya, kwa sasa ngoja upumzike kwanza. Nakwambia bora uache kujipa matumaini hewa, maana hutofanya kwa kiwango ulichokuwa unakifikiria.
Mwaka mpya unaanzia ndani yako, mwaka mpya wa mabadiliko unayoyataka yanapaswa kusukumwa nje kwa vitendo bila kusubiri namba zibadilike yaani kusubiri 7 iondoke, ije 8.
Anza leo kusoma Neno la Mungu, ndio unategemea mwaka mpya uanze vizuri, ila mimi nakusihi uanze sasa yaani leo. Wakati unafika ile tarehe moja, kama ni gari liwe tayari lipo gia namba 3, unaingia mwaka mpya unapandisha gia namba 4.
Wakati wenzako wanaendelea na mikakati mingi ya kuanza kusoma Neno la Mungu, wewe tayari upo mbali sana. Hata ukifika mahali pa mlima unapopaswa kushusha gia, tayari safari yako itakuwa imekolea mwendo.
Jikumbushe tu mwenyewe, mangapi mwaka ulivyoanza ulipanga kuyafanya na uliendelea kuyafanya? Utakuta ni mengi sana uliishia njiani. Ndio maana nakwambia anza leo, wakati uliokubalika ni sasa.
Rejea:(Kwa maana asema, Wakati uliokubalika nalikusikia, Siku ya wokovu nalikusaidia; tazama, wakati uliokubalika ndio sasa; tazama, siku ya wokovu ndiyo sasa.) 2 KOR. 6:2 SUV
Haleluya, siku ya kusoma Neno la Mungu ndio sasa, acha kujisubirisha hadi mwaka mpya uanze au mwezi mpya uanze, anza leo, hapo ulipo ndio wakati unaofaa.
Roho Mtakatifu akusaidie kuelewa haya ninayokueleza hapa, ipo siri ya mafanikio yako ya kiroho katika kuanza sasa/leo. Wengi wameshindwa kufanikiwa kwa kusubiri kuanza kesho, Neno la Mungu linasema hivi; wakati uliokubalika ndio sasa.
Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Chapeo Ya Wokovu
www.chapeotz.com
WhatsApp 0759808081