Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai.
Kila mmoja anaweza kufikiri kiongozi wa miguu yake ni akili yake mwenyewe, bila kujua yupo kiongozi mzuri ambaye anaweza kuiongoza vyema miguu yetu.
Miguu yetu ina kiongozi wake ambaye anatufanya tufuate njia sahihi kwa kujiepusha na uovu, vile vile yupo kiongozi anayetufanya tufuate njia mbaya.
Hata tunapoamua kuachana na mambo mabaya, kuna kitu ambacho kimetufanya tuchukue hizo hatua. Hatuachi njia mbaya ilimradi tumeacha, tunaacha kwa sababu tunataka tuliishi Neno la Mungu jinsi linavyotuelekeza.
Rejea: Nimeiepusha miguu yangu na kila njia mbaya, Ili nilitii neno lako. Zab 119:101 SUV
Umeona hapo, kinachotufanya tujiepushe na njia mbaya si kingine, bali tunataka kulitii Neno la Mungu. Maana yake kuacha mabaya yote ni kwa sababu tu unataka kulitii Neno la Mungu, kwa lugha nyingine tunaweza kusema wanaotenda maovu wote hawalitii Neno la Mungu.
Tunapolitii Neno na Mungu kwa kuacha njia mbaya, hilo hilo Neno la Mungu lililotufanya tuache njia mbaya linapaswa kutuongoza hatua za miguu yetu. Ili usijikwae njiani unapotembea, Neno la Mungu linapaswa kuwa taa ya miguu yako, na mwanga wa njia yako.
Ndivyo inavyopaswa kuwa, na ndivyo Mungu anatuambia hivyo kupitia Neno lake takatifu. Hakuna jambo lingine linaweza kukuongoza katika njia sahihi isipokuwa Neno la Mungu tu.
Rejea: Neno lako ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu. Zab 119:105 SUV
Ukiona unatenda dhambi ujue hili, hatua za miguu yako zimeacha kuongozwa na Neno la Mungu, ama Neno la Mungu limekosekana ndani mwako. Likikoseakana maana yake taa yako imekosa mafuta, na mafuta yakiisha taa haiwezi kutoa mwanga wowote.
Kwa leo tungesema taa za umeme zinategemea umeme wenyewe ambao ni LUKU, umeme huwezi kuwaka kamwe kama huna luku, hata kama hujakatwa. Kama taa za umeme haziwezi kuwaka bila kuwepo luku, nasi hatuwezi kuangaza maisha yetu ya wokovu bila neno la Mungu.
Kila siku tunapaswa kuhakikisha hatupungukiwi Neno la Mungu, kama tunavyohakikisha LUKU haikosekani kwenye nyumba zetu. Likishakosekana utaanza kuona mabadiliko ndani yako, hatua za miguu yako itaanza kuelekea kwenye uovu.
Hatua za miguu yetu kama wakristo, zinapaswa kuelekezwa na Neno la Mungu, Neno la Mungu ni dira sahihi ya kututupeleka sehemu sahihi. Tusipoelewa hili, tutajikuta tukimtenda Mungu dhambi, kwa kukosa maarifa sahihi ndani yetu.
Uovu ni rahisi sana kutuvaa tukiwa hatuna Neno la Mungu, na tukiwa nalo tunapaswa kuliruhusu lituelekeze namna ya kuenenda, namna ya kuishi maisha matakatifu ya kumpendeza Mungu wetu.
Rejea: Uzielekeze hatua zangu kwa neno lako, Uovu usije ukanimiliki. Zab 119:133 SUV
Ooh Haleluya, sijui kama unaelewa haya ninayoyasema hapa, maana unapaswa kuelewa haya maandiko matakatifu ili ujue hupaswi kuacha kusoma Neno la Mungu. Wala hupaswi kuona suala la kusoma Neno la Mungu ni la kawaida kawaida au ni mzigo kwako.
Swali la kujiuliza, kama hatua zako hazielekezwi na Neno la Mungu, zitaelekezwa na nini? Bila shaka umeelewa ninachosema hapa, nje na Neno la Mungu yapo mengi ya dunia hii ya kukupotosha umtende Mungu dhambi.
Tena ukisoma Zaburi hii hii Neno la Mungu linaweka wazi kabisa, ili tusimtende Mungu dhambi, tunapaswa kuliweka Neno lake mioyoni mwetu tusije tukamtenda dhambi.
Rejea: Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, Nisije nikakutenda dhambi. Zab 119 :11 SUV
Labda unisaidie wewe, unasema umeokoka na humtendi Mungu dhambi, na huku huwa huna tabia kabisa ya kusoma Neno la Mungu. Je! Unapata uhakika gani wa kujithitishia kuwa humtendi Mungu dhambi?
Nimekupitisha mistari michache ya Biblia uweze kuona uzito wa hili jambo, Neno la Mungu lina maana kubwa sana kuliweka mioyoni mwetu. Tena tunapaswa kuwa na kiu ya Neno kila wakati, hakuna kusema nilisoma zamani imetosha, mbona kula unakula kila siku na hujawahi kusema imetosha?
Tubadilike ndani ya fikra zetu, hata kama ulikuwa unasoma Neno la Mungu, huenda hukuwa unasoma kwa uzito sana. Hebu kuanzia sasa lichukulie Neno la Mungu kwa uzito wa kutosha, utaanza kuona likileta mabadiliko ndani ya maisha yako ya kiroho na kimwili.
Zipo ahadi nyingi ndani ya Neno la Mungu, sio tu kutuepusha na dhambi, tunachopaswa ni kuelewa uthamani wake, mengine yatajileta yenyewe kadri tunavyozidi kulijua.
Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Chapeo Ya Wokovu.
Blog: www.chapeotz.com
WhatsApp: 0759808081