Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai.

Kuna vitu lazima tukae chini tujichunguze kwa upya, bila hivyo mwisho wetu unaweza kuwa mbaya kuliko mwanzo wetu tulioanza nao, na kinachoangaliwa kwetu ni mwisho mzuri.

Wakristo tulio wengi tumeanza kushindwa bidii ile ya kumtafuta Mungu wetu, hata na wale ambao tunaona hamwabudu Mungu wa kweli. Sio jambo geni sana wewe jaribu kuangalia yale madhehebu mengi yanayoonekana na wengi wanamwabudu mungu mwingine asiye wa kweli, alafu linganisha na yale wanayosema wanamwabu Mungu wa kweli.

Utakuta kuna tofauti kubwa sana, ile bidii ya ibada na kupenda mambo ya Mungu haipo kwenye matendo, imebaki kwenye midomo yao. Lakini wale wanaoonekana wamepotea njia, ndio wana bidii kweli kweli.

Wakati wewe unajiona upo dini nzuri ya kukusaidia kufika mbinguni, husomi Neno la Mungu wala huna muda nalo. Lakini mwenzako ambaye unamwona yupo dhehebu/dini mbaya ya kumpotosha, ana bidii kweli kweli kwenye Neno la Mungu.

Wakati wewe unajiona upo dhehebu/dini nzuri ya kukusaidia kufika mbinguni, hukumbuki mara ya mwisho kuwa na maombi ya kufunga. Lakini mwenzako unayemwona yupo mahali pasipo sahihi haipiti mwezi lazima ajinyime chakula kwa ajili ya mungu wake.

Hukumbuki mara ya mwisho kuwahi ibada ilikuwa ni lini, lakini mwenzako unayemwona amepotea hakosi kuwahi ibadani. Wakati mwingine hukumbuki mara ya mwisho kuacha shughuli zako, na kuingia nyumba ya Bwana kuomba hata nusu saa. Lakini mwenzako unayemwona yupo mahali pasipo sahihi anafunga shughuli zake, anapata muda wa kuingia ibadani.

Usishangae siku ya mwisho ukaenda kumwona ameketi pamoja na Bwana Yesu Kristo, kwa sababu hujui siku anakutana na Mungu wa kweli akambadilisha kabisa. Maana hatuna muda na Mungu wetu, ila tuna muda wa kuongea sana, inatufaa nini kuongea sana wakati tunashindwa bidii na wale tunaowaona kama tunavyowaona sisi?

Tunashindwa akili hata na ndege wa angani, wanajua nyakati zao, lakini wanadamu wenye akili tulizopewa na Mungu hatujui amri za Mungu wetu. Na kweli tutazijuaje wakati hatuna muda kabisa na Mungu wetu.

Rejea: Naam, koikoi angani ajua nyakati zake zilizoamriwa; na hua na mbayuwayu na korongo huangalia wakati wa kuja kwao; bali watu wangu hawazijui amri za Bwana.Yeremia 8:7 SUV

Tutapataje kupona ndugu zangu, ukisoma hilo andiko unaona labda hakuna kitu kama hichi? Hebu kuwa tu mkweli maana tunaweza kujiona tupo vizuri kumbe tumeshapoteza mwelekeo kabisa.

Tunapaswa kuzijua amri za Mungu zilizo amriwa kwetu wanadamu, na ili tuzijue tunapaswa kuwa na muda na yeye, tusibaki tunajisifia tuna dini nzuri, wakati uhusiano wetu na Mungu ni mbovu.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.

Chapeo Ya Wokovu

www.chapeotz.com

WhatsApp 0759808081