Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai.
Kuna vitu tunaweza kujiona Mungu ametusaidia kupanda juu kutokana na mafanikio tunayoyaona yanakuwa kwetu. Bila kujihoji ni mafanikio yenye nia njema kwetu ama ni mpango wa shetani kutuvuruga.
Wengi tukisikia tumepandishwa daraja/ngazi/cheo, huwa tunafurahi sana na wakati mwingine tunafanya na sherehe ya kufurahia kitendo kile. Wengi wetu huwa hatukai chini tukatafakari hadi kupandishwa cheo, kuna nini kimeonwa kwetu.
Hicho kizuri kilichoonwa kwetu, ni chenyewe tu ndio kinatufanya tupandishwa daraja kazini, hata moyoni mwako unaona bidii yako kazini ndio imekufanya upandishwe cheo. Ukijitazama kweli ulikuwa na kadii japo sio sana ukijilinganisha na fulani anayejitumaga sana.
Kutokuwa na maarifa moyoni mwako, Roho Mtakatifu anaweza kukuambia cheo hichi sio sahihi kwako, unajikuta umeingia moja kwa moja kwa kuona hayo ni mawazo potofu. Kumbe nyuma ya hicho cheo kuna uovu, nyuma ya hicho cheo kuna mtego wa kuangamiza maisha yako, nyuma ya hicho cheo kuna kilio.
Mama/dada unapata taarifa ya mume wako kupandishwa cheo kazini, na kazi aliyopata ni nzuri sana, na mahali anapoenda kufanya kazi huwezi kwenda naye kutokana na majukum yako uliyonayo. Mnachofanya ni kuweka mipango vizuri ya kutembeleana mara kwa mara.
Kumbe kupandishwa kwake cheo mumeo ilikuwa namna ya kumsogeza mbali na wewe, ili pawepo na mwanya wa yule boss kutembea na wewe. Kumbe kupandishwa cheo mumeo ilikuwa mbinu ya shetani kuharibu ndoa yako, yupo mwanamke mwingine anaenda kuchukua nafasi yako ya mke.
Baba/kaka unapata taarifa ya mke wako kupandishwa cheo kazini, kumbe hicho cheo nia yake ni mbaya juu ya ndoa yako. Hicho cheo kilikuwa ni rushwa ya ngono, kwa kuwa hukujua hilo wewe ulienda na kanisani kutoa sadaka ya shukrani.
Sikuambii kila kupandishwa cheo kuna nia mbaya katika maisha yako ya ndoa, sikuambii kila kuhamishwa kikazi kuna mpango mbaya katika ndoa yako. Kupandishwa cheo kwingine ni kuzuri kabisa na kuhamishwa kikazi kwingine ni kuzuri kabisa hakuna nia mbaya.
Unachotakiwa kujihoji wewe kama wewe, hiyo nafasi unayopewa kazini kwako ina nia njema au ni mpango uliotengenezwa wa kukuharibu wewe au kuharibu familia yako.
Hili unapaswa kulipeleka ngazi yeyote ile katika maisha yako, hata kanisani kwako unaposali, kuna nafasi huwa zinakuja ghafla unaambiwa utakuwa fulani. Unashangaa tangu ulivyopata hicho cheo cha kuitwa fulani, umepoa sana rohoni, umekosa hata ule ujasiri uliokuwa nao wa kukemea dhambi.
Umebaki unaitikia kila kitu ili kulinda nafasi uliyopewa, lakini kuna wakati unajiona kuna kitu kimepungua kwako na ukijaribu kuwa kama mwanzo, unaona kama kuna mahali umefungwa miguu yako. Kadri siku zinavyoenda mbele marafiki zako wanaanza kukuambia ndugu vipi mbona siku hizi umebadilika sana.
Unaweza kufikiri ni marafiki zako, kumbe ni Mungu anawatumia kusema na wewe, unaweza kufikiri wameanza kukuonea wivu kwa nafasi uliyonayo, kumbe shetani anakuletea hilo wazo ili usiweze kufahamu cheo/nafasi uliyopewa ndio imeua ujasiri wako wa kusema kweli ya Mungu.
Unafurahia umepewa ofa ya kwenda kula Christmas nje ya nchi, na sharti ulilopewa hupaswi kwenda na mume wako maana nafasi ni moja tu. Na mume wako baada ya kusikia hivyo alifurahia sana na kuona familia yenu sasa Mungu ameikumbuka, mmeanza kusafiri nje ya nchi.
Mbinu zote hizo za mke wako kwenda kupumzika nje ya nchi, ni mbinu tu ilikuwa inatafutwa ya kwenda kukusaliti, tena ulitiwa moyo ulivyoambiwa awamu nyingine mtaenda wote. Kwa kuwa hujawahi kwenda nje ya nchi, unabakia unafurahia tu na wewe utaenda.
Sikuambii kila kwenda nje ya nchi ni njia ya kusalitiwa, ninachotaka uone hapa ni kitu cha muhimu sana Roho Mtakatifu anakufundisha, uwe na akiba ya maarifa haya moyoni mwako. Wengi wamepotezwa kwa kutokujua hili, ndoa nyingi zimeharibika kwa njia hii, ukifuatilia vizuri utakuta kuna sauti ilisema nao, kuna wakati walikosa amani kabisa kuhusu hiyo nafasi waliyopewa, lakini walishindwa kujua.
Unapokuwa na Neno la Mungu ni rahisi kwako kujua haya, ndio maana kuna umhimu wa kukua kiroho, Mungu anaweza kusema nawe kupitia Roho Mtakatifu. Ukaona ni mawazo tu potofu ya kukuzuia kitu kizuri, ukafanya unavyojua wewe, baadaye ukishaharibikiwa unaanza kusema niliona hivi na vile.
Ninakueleza mambo ambayo yapo, na ninakueleza habari iliyomkuta Daudi tunayesoma habari zake njema za uhodari aliokuwa nao. Naomba usome haya maandiko matakatifu kwa umakini kabisa, uone jinsi Daudi alishtukia hili la kupewa nafasi/cheo.
Rejea:1 Samweli 18 :18, 21_27 SUV
18 Naye Daudi akamwambia Sauli, Mimi ni nani, na jamaa zangu ni akina nani, au mbari ya babangu, katika Israeli, hata mimi niwe mkwewe mfalme?
21 Naye Sauli akasema moyoni, Mimi nitamwoza huyu, awe mtego kwake, tena kwamba mkono wa Wafilisti uwe juu yake. Basi Sauli akamwambia Daudi mara ya pili, Leo utakuwa mkwe wangu.
22 Naye Sauli akawaagiza watumishi wake, Zungumzeni na Daudi kwa siri, na kusema, Angalia, mfalme anakuridhia, na watumishi wake wote wanakupenda; haya basi! Na uwe mkwewe mfalme.
25 Naye Sauli akasema, Mwambieni Daudi hivi, Mfalme hataki mahari yo yote, ila anataka govi mia za Wafilisti, ili ajilipize kisasi adui za mfalme. Basi Sauli alidhani kumwangamiza Daudi kwa mkono wa Wafilisti.
27 basi Daudi akainuka, akaenda yeye na watu wake, akaua katika Wafilisti watu mia mbili; na Daudi akazileta govi zao, wakampa mfalme hesabu kamili, ili awe mkwewe mfalme. Naye Sauli akamwoza Mikali, binti yake.
Umeona mtego huo? Ukipata nafasi ya kusoma sura yote ya 18 utaelewa zaidi, hapa nimekupitisha mistari michache ya kukusukuma ujifunze zaidi kuhusu hili. Huyu alikuwa ni kijana anayemsikiliza sana Mungu wake, hebu fikiri leo aliye vuguvugu anaweza kutoka kwenye mtego huu?
Turudi kwenye Maandiko Matakatifu, tuwe na muda wa kujifunza maisha halisi jinsi Mungu anavyoweza kutusaidia kwenye mitengo inayokuja kwa njia ya kupandishwa cheo/daraja au kupewa ofa mbalimbali zilizo na hila ndani yake.
Haleluya, sijui kama unaelewa ninachokueleza hapa, hebu tuone mtego mwingine aliouona Elisha baada ya Naamani kuponywa ukoma wake.
Rejea:2 Wafalme 5 :14_16 SUV.
14 Ndipo akashuka, akajichovya mara saba katika Yordani, sawasawa na neno lake yule mtu wa Mungu; nayo nyama ya mwili wake ikarudi ikawa kama nyama ya mwili wa mtoto mchanga, akawa safi.
15 Akamrudia yule mtu wa Mungu, yeye na mafuatano yake yote. Akaja, akasimama mbele yake; akasema, Sasa tazama, najua ya kwamba hakuna Mungu duniani mwote, ila katika Israeli; basi nakuomba upokee mbaraka kwa mtumwa wako.
16 Lakini akasema, Kama Bwana aishivyo, ambaye nimesimama mbele yake, sipokei kitu. Akamshurutisha apokee; lakini akakataa.
Haya mambo unapaswa kuyajua kwa kujifunza Neno la Mungu, Mungu ametupa Neno lake tuweze kujifunza mambo mbalimbali. Ukisoma hiyo sura mpaka mwisho utaona Gehazi aliona Elisha anakataa zawadi, ngoja yeye atumie hiyo fursa kwenda kujipatia mali.
Hakujua kukataa kwa Elisha kulikuwa na sababu, badala yake Ugonjwa uliokuwa kwa Naamani ukawa kwa Gehazi. Unafikiri Gehazi hakuwa mchaji wa Mungu? La hasha Elisha hakuwa na mtumishi asiyemjua Mungu.
Usipigwe upofu na cheo ukamkosea Mungu wako, usipigwe upofu na fedha ukakosa nguvu ya kukemea uovu unaofanywa na waliokupa fedha ya kununua vyombo, kujenga nyumba yako, kujenga jengo la kuabudia Mungu.
Haijalishi umesubiri kupandishwa daraja miaka mingi, ikiwa utaona hicho cheo kina hila ndani yake usikubali, haijalishi una hali ngumu kiuchumi, kama unaona fedha unazopewa unakosa amani moyoni mwako na kadri unavyotaka kulazimisha uzichukue unasikia kelele, achana nazo kabisa.
Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Chapeo Ya Wokovu
www.chapeotz.com
+255759808081