Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, Mungu ametupa kibali kingine tena cha kuweza kukutana pamoja. Tutumie nafasi hii kujifunza zaidi mambo yanayoweza kutusaidia katika safari yetu ya wokovu.

Ulianza vizuri kusoma Neno la Mungu ghafla ukafunika biblia yako ukaiweka kwenye droo au meza au kabati au saduku lako la nguo. Ukabaki unaenda nayo siku za jpili, tena jpili yenyewe muda mwingine unaona uvivu wa kuifungua fungua unaamua kumchia jirani yako afanye hiyo kazi.

Pamoja na mtu kuwa na biblia ya gharama kubwa bado hana hamu ya kuisoma kabisa, wakati ananunua aliweka mipango mingi sana ya kuisoma kila siku. Ila badala yake imebakia inafutwa siku za ibada, inapigwa upepo wa nje inarudishwa tena mahali ilipokuwa.

Zoezi hili halina ukomo, miaka inaenda bila mafanikio yeyote kuachiliwa katika kifungo hicho, mfungwa huyu amebakia kutolewa nje kupigwa na upepo basi. Kifungo chenyewe alichopewa sio kwamba kina mwaharibia maisha yake, zaidi kinamkosesha mfungaji mwenyewe maarifa ya msingi.

Pamoja na kelele zote za kufungua biblia zao kwenye kifungo hicho cha maisha, bado msisitizo huo unaonekana ni makelele mbele yao. Kila wakijaribu kufungua wanaona hawaoni kiu ya kupata maarifa ndani ya Neno la Mungu.

Wimbo wao ni kesho, mara mwezi ujao, mara mwaka ujao, wamebakia na hilo tu, hakuna kinachoonekana kinabadilika. Kinachobadilika kwao ni miaka kusonga mbele bila kuchukua hatua zozote.

Bado siku chache tuanze mwaka mpya, utasikia mipango mbalimbali ya kusoma Neno la Mungu, kelele hizi zitasikika ndani ya mwezi huo wa kwanza labda zikienda sana hadi mwezi wa pili. Baada ya hapo hutosikia tena mtu akizungumzia hilo jambo, biblia zinabaki kwenye kifungo kile kile cha awali.

Naamini tumezifunga biblia zetu kwenye kifungo ambacho hatukupaswa kabisa kuzifunga, ukizingatia na umhimu wake kwetu sisi. Mimi na wewe tunapaswa kuchukua maamzi sahihi na wa kumaanisha kwa kile tulichoamua, bila hivyo wimbo utabaki ule ule miaka yote.

Muhimu kwako ni kuiachilia huru biblia yako huko ulipoificha, kificho hicho kinakosesha wewe mwenyewe mambo ya msingi. Ambayo yangekusaidia kukujenga maeneo mengi katika maisha yako ya wokovu, tofauti na sasa hivi unajiona upo vizuri, ila ukweli haupo vizuri kabisa.

Shida nyingine mtu akishaelezwa kitu kikamwingia vizuri, anakipeleka mwaka mpya, anasubiri mwaka mpya ufike ndio aanze kusoma Neno la Mungu. Huko ni kujidanganya ndugu yangu, kama ni kuanza ni sasa, acha habari za wiki ijayo unaanza, anzia hapo ulipo.

Biblia haina kosa lolote unaifunga ya nini kiasi hicho, ukiifungua huwa inakufanyia nini ambayo unahisi ukifungua tena itakuangamiza maisha yako. Kama Yesu Kristo ni Bwana na mwokozi wa maisha yako, unapaswa kuisoma biblia yako kwa bidii sana.

Bidii yako ya kulijaza Neno la Mungu moyoni mwako, itakusaidia kujiepusha kwenye dhambi ambazo unaweza kuzifanya kwa kukosa maarifa sahihi ya Neno la Mungu. Ndio unaweza kufanya dhambi zingine bila kujua kama unamkosea Mungu wako, kwa kukosa tu kwako maarifa ya Neno la Mungu.

Tufungue mioyo yetu kwenye Neno la Mungu, na tuone lilivyo la muhimu katika maisha yetu ya wokovu, tutaona utayari wa mioyo yetu na ilivyo rahisi kwetu kuliweka mioyoni mwetu. Zaidi ya hapo utaendelea kuiacha biblia yako kwenye kifungo kisicho na mwisho wake.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.

Chapeo Ya Wokovu

www.chapeotz.com

+255759808081