Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai.

Mnapoanza safari pamoja, lazima uangalie mmefika wangapi katika safari yenu mlioanza nao, maana si wote huwa wanafika mwisho. Wengi huwa wanaishia njiani wakati wengine wanaendelea na safari yao.

Kuanza inaweza isiwe shida sana, changamoto ni kufika kwenye kile ulichokianza, na hili huwa hatulizingatii sana. Wengi huwa tunajivunia sana mwanzo wetu mzuri kuliko mwisho wetu wa safari, tunatumia muda mwingi kujivunia yaliyopita wakati huo tumeishia njiani.

Kweli tunaweza kujivunia mwanzo wetu mzuri tulivyokuwa watu maridadi katika utendaji wa mambo mbalimbali, lakini tukumbuke kinachoangaliwa ni mwisho wetu mwema. Haijalishi ulifanya vizuri sana ulivyoanza safari yako, kama mwisho wako wa safari utakuwa mbaya, itakuwa haina maana yeyote.

Hili likusaidie katika safari zako zote, unapofika mahali ukajikuta umechoka na huna hamu tena ya kuendelea mbele. Ukiangalia bado hujafika mahali ambapo ulitarajia kufika, unapaswa kujipa moyo mkuu wa kusonga mbele ili uweze kufika pale ulitamani kufika.

Wengi tulianza kwa kasi kubwa sana safari ya kusoma Neno la Mungu, hasa mwaka ulivyoanza, safari hii ya usomaji wa Neno la Mungu ilikuwa na watu wengi wenye moyo wa hamasa kubwa. Kadri siku zinavyozidi kwenda mbele, kila hatua walizidi kupungua mmoja mmoja.

Wale wanaondelea na safari nao wamekosa tumaini kabisa la lile walilokuwa wamepanga kulifanya katika maisha yao yote hapa Duniani, wamekosa ile ladha ndani yao ya kuendelea mbele. Muda wowote na wao wanaweza kurudi nyuma kama wenzao walivyokata kamba njiani.

Wengi walikuwa wanampenda Mungu wakati wana kazi/biashara nzuri, sasa walivyozipoteza vitu hivyo wameona waachane na mambo ya Mungu kwanza. Na wengine walimpenda Mungu wakati ndoa zao zimejaa kicheko cha furaha, baada ya mambo kwenda kinyume, wameachana kabisa na kujishughulisha na mambo ya Mungu wao.

Wapo pia walikuwa karibu sana na Mungu wao wakati wana shida ya kupata mtoto, mume, mke, baada ya shida yao kuisha, wameona waachane na kujituma na mambo ya Mungu. Unaweza kuona jinsi gani shida yake ndio ilimfanya ampende Mungu, Mungu baada ya kumsaidia badala ya kuendelea kumpenda zaidi anakuwa kinyume chake.

Wakati mwingine kama vile tunamwambia Mungu ulikosea kututoa kwenye shida yetu, kama wakati hujatutoa tulikupenda, ulivyotutoa mbona tumejitenga na mambo yako. Ni kama vile tunamwambia Mungu aturudishie shida zetu ili tuendelee kumpenda zaidi, kumbe hatupaswi kumpenda Mungu kwenye upande wa shida tu wala hatupaswi kumpenda Mungu wakati wa raha tu.

Linda sana mwisho wako uwe mwema, pamoja na changamoto ngumu unazokutana nazo, hakikisha hujitengi na Mungu wako. Ulikuwa msomaji mzuri wa Neno la Mungu, hakikisha unaendelea na zoezi hilo hadi mwisho wako, usije ukakata kamba njiani.

Mungu anaangalia mwisho mwema na sio mwanzo mwema, wengi hawapendi kusikia hili ila ukweli ndio huo, ingekuwa Mungu anaangalia mwanzo mzuri huenda wengi tungejivunia sana tulivyoanza wokovu. Huku tukiwa ndani ya dhambi, tunakuwa hatuna wasiwasi wowote kwa sababu mwanzo wetu ulikuwa mzuri sana.

Mungu mwenyewe akaliona hili, akaamua kutuwekea angalizo hili, ili unapofika mahali umechoka, vyema ukamwambia akutie nguvu uweze kumaliza safari yako salama. Maana kinachoangaliwa kwako ni mwisho mwema na sio mwanzo mwema.

Rejea: Heri mwisho wa neno kuliko mwanzo wake, Na mvumilivu rohoni kuliko mwenye roho ya kiburi. Mhubiri 7:8 SUV.

Tena ameongezea kusema na mvumilivu rohoni, kumbe ili ufike mwisho mwema unapaswa pia kuwa mvumilivu rohoni. Vipo vya kukuvunja moyo wako ila hupaswi kuacha lile linalomtukuza Mungu na kukujenga moyo wako.

Endelea kusoma Neno la Mungu kwa bidii zako zote, usiishie njiani haitakuwa na maana yeyote. Kila ukikumbuka hili wakati umechoka iwe chachu kwako kuendelea kusimama imara katika usomaji wako wa Neno la Mungu.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.

Chapeo Ya Wokovu

www.chapeotz.com

+255759808081