Bwana Yesu asifiwe ndugu, Mungu ni mwema sana ametupa kibali cha kuweza kuiona tena siku ya leo, tunayo sababu ya kumrudishia sifa na utukufu.

Kujijengea tabia ya kujitathimini wewe kama wewe, inakufanya kujifunza mambo mengi zaidi kupitia makosa mengi uliyofanya, pia inakupa uwezo wa kutambua namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali zitazokujia mbele yako.

Kujitathimini inakufanya kujiona umepiga hatua zaidi mbele au umebakia pale pale bila kusogea hatua yeyote. Inakupa nafasi ya kuweza kuongeza bidii zaidi, pia inakupa nafasi ya kujirudi pale ulipolegeza mwendo.

Nimefurahishwa na ndugu yangu mmoja katika Kristo tulikuwa tunasoma Neno la Mungu pamoja, alianza mwaka 2015 tukiwa kundi moja. Ambalo kundi hili lilikuwa la whatsApp, tulienda pamoja hadi tukafika mwaka 2016 tukiwa pamoja, na tulipofika mwaka huu 2017, hakufanya vizuri sana.

Kundi letu lina utaratibu wa kumwondoa yule asiyeshirikiana na wenzake katika kusoma Neno la Mungu, maana tumejiwekea utaratibu baada ya kusoma unapaswa kuwashirikisha wenzako tafakari yako. Hii imekuwa njia nzuri ya kumjua nani kasoma na nani hajasoma siku hiyo.

Huyu ndugu baada ya kutolewa, kitendo kile hakikumpelekea kulaumu tu kutolewa kwake, alikaa chini na kufanya tathimini ya kina. Akajua kosa lake lipo wapi, akajua tangu alivyoanza kusoma Neno la Mungu, mwaka aliofanya vibaya ni huu 2017.

Amefika mahali ameona akatae huo udhaifu, amefika mahali amesema hapana sipaswi kuendelea na hali hii ya udhaifu. Bila kusukumwa na mtu, wala bila kushawishiwa na mtu rudi usome Neno la Mungu kwa mtiririko mzuri bila kukwamakwama, ameamuana kurudi mwenyewe.

Napenda kukushirikisha ujumbe wake alionitumia, unaweza kuondoka na fundisho kupitia ujumbe wake huu mfupi, usipopata la kujifunza utaniwia radhi kwa kutumia muda wako vibaya. Pia nitakuomba uishie hapa kusoma haya ninayoendelea kukushirikisha.

Shalom kaka, naomba ikifika tar 31 unirudishe kwenye group.
Nimegundua mwaka huu 2017 sikuwa mzuri sana kama 2015-2016, kiasi ambacho nilijivunia kujua Neno la MUNGU angalau kwa nukta, ila sasa hivi naona sijui chochote.
NIMEZINGATIA MOYONI, naomba nirudi kuanzia tar 1/1/2018.
MUNGU akubariki.
By F.M

Umeona hapo, hapo yupo nje ya group anaomba kurudi baada ya kujitathimini yeye kama yeye, akajua uzembe aliofanya asiweze kufika mahali alikuwa anataka. Ujumbe wake unaonyesha kujutia sana, ndio maana ameona vyema kuanza tena na sio kuacha moja kwa moja.

Huenda unasoma ujumbe huu ulikuwa msomaji mzuri sana wa Neno la Mungu, lakini ulikwama mahali hukuweza kuendelea tena kusoma. Ninakusihi ufanye tathimini ulivyoacha umepata nini sana na usingeacha ungekuwa wapi sasa hivi.

Huenda unasoma ujumbe huu ulianza kulegeza mwendo katika usomaji wako wa Neno la Mungu, vizuri ukajitafakari kwa upya tunapoelekea kumaliza mwaka huu. Lipo la kujifunza kupitia kujihoji mwenyewe, yapo mengi ya kufanyia kazi baada ya kujitathimini ulipotoka na ulipo sasa.

Bila shaka kama umesoma ujumbe huu mpaka hapa, nina imani lipo jambo umejifunza kupitia ujumbe huu, kile umejifunza vyema kukifanyia kazi kwa vitendo. Vinginevyo utabaki kama ulivyokuwa.

Ulikuwa bado hujaungana na wenzako wanaosoma Neno la Mungu, na unapenda kuungana nao whatsApp group, nitatoa namba hapo mwishoni kabisa. Hakikisha unaitumia vizuri namba hizo na hakikisha umedhamiria kweli, pia hakikisha simu yako ina whatsApp, nitumie ujumbe wako wenye majina yako halisi/kamili kwa njia ya whatsApp.

Mungu akubariki sana.

Chapeo Ya Wokovu

www.chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081