Leo tumeuanza mwaka mpya, bila shaka unayo furaha kubwa kufikia mwaka huu, bila shaka unayo mipango mingi ya kufanya mwaka huu. Kila mmoja atakuwa amejiwekea malengo makubwa na madogo, kati ya hayo malengo yapo yatakayotimia na yapo ambayo hayatatimia.

Kila mmoja ana hamasa kubwa ndani yake, hamasa ambayo inamfanya aanze kufanya kile amepanga kwa kasi kubwa. Kasi hii isipokuwa na nidhamu ndani yake, mwezi wa tatu itakuwa mbali utasikia kimya kimetanda na kule kufanya hakupo tena.

Unapaswa kuelewa kama umeamua kujifunza Neno la Mungu mwaka huu, hakuna atakayekuzuia kufanya hivyo. Ni wewe utaamua kusoma kila siku, na wewe huyohuyo utaamua kuishia njiani baada ya siku kadhaa kupita ulivyoupokea mwaka mpya.

Leo najua una hamasa kubwa sana ya kuanza mambo mengi, kwa juhudi kubwa sana, lakini usipokuwa na nidhamu ya kutosha kwa hilo uliloanza nalo kulifanya. Nakuambia hutofika mbali utakuwa umesahau ulianza kufanya nini ulivyoingia mwaka mpya.

Katika kufanya utakutana na changamoto nyingi zenye kukushawishi uachane na hilo unalolifanya kila siku, haijalishi unafanya nini, ilimradi ni kitu kinachokuletea mafanikio. Yanaweza yakawa mafanikio ya kimwili au kiroho, inategemeana na jambo gani umedhamiria kulifanya mwaka huu.

Mwaka huu huenda umepanga uwe mwaka wako wa kukua kiroho kwa njia ya kusoma Neno la Mungu, nisikutie sana moyo nikashindwa kukupa ukweli. Ukweli ni kwamba, usipoweka bidii na nidhamu katika kusoma Neno la Mungu, nakwambia mwezi wa tatu mbali utakuwa umeacha kabisa kusoma Neno la Mungu.

Ukitaka kujua hili, rudi nyuma utazame ni mangapi mwaka 2017 ulipanga kufanya, na ukaanza nayo kabisa kuyafanya, baadaye ukaachia njiani. Ndivyo itakavyokuwa kwenye Neno la Mungu, huenda umejaribu kufanya hili mara nyingi lakini uliishia njiani, uliishia njiani kwa sababu hukuweka mipango vizuri inayoongoozwa na nidhamu.

Utadumu katika kutenda jambo lako mwaka huu, kama utajiwekea nidhamu kwa utakaloamua kulifanya, mojawapo tunalolizungumza hapa ni usomaji wa Neno la Mungu. Hili unaweza kuingia kila mwaka bila mafanikio yeyote yale, kama hutoweka mikakati vizuri.

Sina shaka leo kila mtu atakuwa na hamasa kubwa sana, ila baada ya siku kadhaa kupita ukimya utarudi ule ule wa kutokufanya. Na wapo pia mwaka huu utakuwa mwaka wa historia njema kwao, maana wanaenda kuanza jambo ambalo litakuwa faida kwao siku zote za maisha yao hapa Duniani.

Ninachoweza kukuambia siku ya leo, simamia vyema lile umeamua liwe kwako mwaka huu, kama kuna tabia unatamani uijenge kwako mwaka huu. Hasa tabia ya kujisomea Neno la Mungu kila siku, unaweza ukaitengeneza vizuri kabisa na ikawa tabia yako ya kudumu kabisa.

Kila kitu ni kuthubutu, ukiacha mihemko ya mwaka mpya, ukadhamiria kutoka ndani ya moyo wako, utaona mabadiliko yakianza kutokea ndani yako. Mabadiliko hayataletwa na maneno, yataletwa na matendo yanayosamamiwa kikamilifu kila siku.

Siku tunasema tunafunga mwaka 2018, uwe miongoni mwa watu waliofanikiwa kusoma Neno la Mungu, hili halihitaji kuja kushikiwa fimbo na mtu, ni wewe kuamua kutoka ndani ya moyo wako. Na kuamua kwako kuambatane na nidhamu isiyokuwa ya kinafiki ndani yake, kusoma kwako Neno la Mungu kutoke ndani ya moyo wako.

Sherekea kwa amani na furaha, ila kumbuka malengo yako ya kusoma Neno la Mungu yatatimia kwa kufanya, na kufanya kwenyewe kuwe na nidhamu isiyoyumbishwa na changamoto zozote za maisha au katika usomaji wako.

Usije ukafika mahali ukasema Biblia ngumu nimeshindwa kuelewa ninachosoma, utapaswa kusoma huku ukimsihi Roho Mtakatifu akusaidie kuelewa baadhi ya maeneo unayopata changamoto na sio kuacha, hapo utakuwa umefaulu vizuri sana.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.

Chapeo Ya Wokovu

Blog: www.chapeotz.com

Email: chapeo@chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081