Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai.

Ulikuwa hutaki kuchukua hatua zozote mpaka ufike mwaka mpya, ndio huo umefika na leo tupo siku ya pili tangu tuupokee mwaka mpya. Ni kama utani ila ukweli ndio tupo mwaka mwingine 2018, unaweza usione tofauti kubwa sana ya mwaka jana na mwaka huu, ila unapaswa kujua safari inaendelea hivyo.

Wengi husubiri hadi mwaka mpya, ukimgusa kufanya jambo fulani atakuambia ngoja kwanza mwaka mpya ufike ndio nitaanza. Hata kama jambo lilikuwa lina uwezekano wa kuanza kufanya mwaka husika aliopo, anafikiri kuna utofauti mkubwa sana kwenye mwaka mpya.

Kweli sikatai kuna mambo mengine huwezi kufanya hadi mwaka mpya ufike, mfano ukitaka kuanza shule utapaswa kusubiri hadi shule zifunguliwa mwaka mpya. Huku maandalizi mengine yakiendelea, huwezi kusema nitaanza shule nikiwa peke yangu hata wenzangu wasipokuwepo, labda ujitafutie mwalimu mtaani aanze kukufundisha peke yako.

Vile vile ukitaka kusogea darasa lingine, utapaswa kusubiri mwaka mwingine ufike ndio uitwe mwanafunzi wa darasa la pili na sio la kwanza tena. Kama ilivyokuwa mwaka uliopita.

Lakini yapo mambo binafsi ya kuchukua hatua wewe kama wewe bila kutakiwa kusubiri wengine, mfano mwingine ukitaka kusafiri na usafiri wa Basi. Utapaswa kusubiri Basi lijae kwanza na muda uliopangwa ufike ndipo uweze kuondoka, huwezi kusema mimi nina haraka nataka tuondoke hivi hivi peke yangu. Labda ulikondishe ulipe gharama ya watu wote waliopaswa kupanda vinginevyo utapaswa kusubiri.

Vitu vingine havipaswi kusubiri wengine, vitu vingine havipaswi kusubiri mwaka mpya, mfano kuachana na tabia fulani mbaya uliyonayo. Hii huwezi kusema ngoja mwaka mpya ufike ndio nitaiacha tabia hii, huko ni kujidanganya mwenyewe, unapaswa kuanzia hapo ulipo kuiacha.

Jambo lingine ambalo wengi huwa wanajidanganya ni kuhusu usomaji wa Neno la Mungu, mtu ana uwezo wa kuanza kusoma Neno la Mungu leo, ila anakuambia subiri mwezi fulani nitaanza, subiri mwaka ujao nitaanza. Cha kushangaza huo mwezi na mwaka unafika wala humwoni akianza chochote, usipofikiri vizuri unaweza ukashindwa kuelewa.

Ukitaka kuelewa vizuri hili, watazame wale wote waliosema mwaka huu lazima watakuwa watu wa kusoma Neno la Mungu, we waulize leo wapo sura ya ngapi katika Biblia. Utasikia majibu yao, na kama ndio wewe ulijiahidi utaanza kusoma Neno la Mungu mwaka utakapoanza, jihoji mwenyewe umeanza hilo zoezi?

Utaona kumbe shida haipo kwenye mwaka mpya, shida ipo kwako mwenyewe, unajikwamisha mambo mwenyewe kwa kufikiri mwaka mpya ndio utakusaidia kuachana na tabia fulani mbaya usizozipenda. Na kuwa na tabia fulani nzuri unayoipenda ukiwa ndani ya mwaka mpya.

Mwaka mpya wako unaweza kuutengeneza hapo ulipo, zile tabia unazozigundua sio sahihi kwako kuwa nazo, unapaswa kuanza kujiondoa kwenye hizo tabia bila kusubiri mwaka mpya wala mwezi ujao. Ukiamua leo naachana na dhambi za siri unazofanya, unaweza kufanya hivyo haraka sana bila kusubiri mwaka mpya.

Ukiamua leo naokoka na kuachana na tabia fulani mbaya, hupaswi kusubiri wakati mwingine, ilimradi umesikia moyoni mwako kuacha maovu na kupaswa kuingia maisha mengine mapya ya kumpendeza Mungu wako.

Ninachosikitika ni kwamba umeshindwa kujua hata Neno la Mungu hupaswi kusubiri kiasi hicho, ni miaka gani hiyo isiyofika tangu kuokoka kwako hadi leo. Unakuja kujidanganya na mwaka mpya, unaanza kwa kasi kubwa baada ya muda fupi unaachana kabisa na kusoma Neno la Mungu.

Hebu ifungue Biblia yako uanze kuisoma, acha uvivu, acha ahadi hewa, acha visingizio visivyo na maana kwako, inapowezekana kujisukuma kwa nguvu kufanya, fanya hivyo. Acha kabisa kusema nitaanza tu kesho si ilikuwa bado mapema kwanza ndio tunaanza mwaka, nakwambia tutaingia mwezi wa pili sasa hivi bado unaimba wimbo ule ule.

Mungu akusaidie kuelewa vizuri zaidi.

Chapeo Ya Wokovu

Email: chapeo@chapeotz.com

Blog: www.chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081