Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai sasa na hata milele, siku nyingine tena njema kabisa Bwana ametupa kibali cha kuweza kuiona. Sifa na utukufu tumrudishie yeye Bwana mwenza wa yote.

Uharibifu wa mtu huanzia ndani mwake, japo kwa macho ya mwili huwezi kuona hili kwa haraka, ila fahamu kwamba ukimwona mtu anaanza kuonyesha tabia mbaya kwa nje. Ujue hiyo tabia haikuanza tu ghafla, ilianza kumharibu kwa ndani, kisha ikatokea kwa nje.

Unapoona tabia njema kwa mtu, hadi ukafika mahali ukaanza kuitamani ile tabia yake, usifikiri ilitokea tu, ipo gharama kubwa alilipa ndio akawa na hiyo tabia. Tena kuanza kutengenezwa kwa hiyo tabia njema kulianza kwa vitu vidogo vidogo vyenye kumjenga ndani yake, hivyo vitu vidogo vidogo ndivyo vilivyoondoa ile tabia ambayo haikumstahili kuwa nayo ndani.

Haikuwa kazi rahisi kuiondoa hiyo tabia asiyoipenda awe nayo, ila kutokana na nidhamu yake ya kujifunza maarifa sahihi ya kuondosha kile kisichompendeza. Na kusimamisha kinachomfaa yeye na Mungu wetu pia, ilimfanya afikie hapo alipo.

Si unakumbuka ulivyookoka siku za mwanzo kabisa, kuna vijitabia ulikuwa huvipendi kwako, ila pamoja na kutovipenda bado vilikuwa vimekung’ang’ania tu. Lakini kadri ulivyoongeza bidii ya kumjua Mungu, vilianza kukuachia, wakati mwingine hukumbuki vilikuachiaje.

Neno la Mungu ni Matengenezo ya mtu wa ndani, linapokutengeneza kwa ndani ukaiva vizuri, matokeo yake hayabaki tu kwa ndani, yanatokeza hadi kwa nje. Ndipo watu waliokuwa wanakufahamu ulivyokuwa siku za nyuma, wanaanza kujiuliza imekuwaje huyu mtu amebadilika kiasi hichi.

Usishangae mtu ameokoka lakini bado unamwona ana vijitabia vilevile vya upagani, unaweza kujiuliza sana inakuwaje mtu aliyemkiri Kristo kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yake. Bado ana tabia za ajabu ajabu? Jibu ni kwamba bado ametawaliwa na uchanga wa kiroho.

Shida ya uchanga wa kiroho huondolewi na maombi, unaondolewa na maarifa sahihi ya Neno la Mungu, iwe kwa kusoma Neno la Mungu au iwe kwa kufundishwa Neno la Mungu na watumishi wa Mungu. Hapo ndipo unaweza kuagana na uchanga wa kiroho, ambao unaweza kukusababisha ushindwe kutofautishwa na yule ambaye hajamjua vizuri Yesu Kristo.

Vizuri ukawekeza zaidi maarifa sahihi ndani yako, vizuri elimu ya kiMungu ikawa kwa wingi ndani ya moyo wako, hii itakufanya ufurahie wokovu wako. Sio umeokoka alafu unasumbuliwa na vitu vidogo vidogo tena vya kitoto kweli kweli, unashindwa kueleweka hata na watu wa Dunia waliojaza maarifa ya kidunia, yasiyo na pumzi ya Mungu.

Ukomavu mzuri wa kiroho unaanzia ndani ya moyo wako ndipo matokeo yake yanaonekana katika mwili, kwa asiyejua anaweza kufikiri unaigiza kumbe ndio maisha yako halisi. Lakini kama utataka kuiga maisha ya aliyekomaa kiroho, utakwamia njiani pale utakapoguswa na changamoto ngumu.

Aliyejengeka vizuri ndani yake, hawezi kurudishwa nyuma kirahisi na jambo lolote lile, hata kama kwa macho ya nyama au kwa akili za kibinadamu linaonekana ni jambo gumu sana na haliwezekani. Bado utamwona amesimamia msimamo wake ule ule wa kumtumainia Mungu wake.

Ushauri wangu kwako, wekeza muda wako mwingi katika kulisoma Neno la Mungu, usikubali changamoto yeyote ikuondoe kwenye hili. Itokee nini, hakikisha msimamo wako upo pale pale, hii inakuja kama tayari umejua umhimu wa Neno la Mungu.

Mungu akusaidie kuelewa vizuri zaidi hili ninalokueleza hapa, vinginevyo utabaki kuona nakupigia kelele, ila namwamini Roho Mtakatifu ni mwaminifu sana. Lipo jambo utakuwa umeondoka nalo katika kusoma kwako hapa.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.

Facebook: Chapeo Ya Wokovu

Email: chapeo@chapeotz.com

Blog: www.chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081