Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai.

Kutokufanya na kufanya, vyote vipo mikononi mwako, yaani ni vitu ambavyo vipo ndani ya uwezo wako. Ambavyo unao uwezo wa kuamua kukifanya na kikafanikiwa, na vile vile unao uwezo wa kufikiri kushindwa, na ukashindwa kweli.

Unapojua manufaa ya kile unafanya, utaona upenyo mbele yako, utaona ipo njia ya kupita ili uweze kufika mahali unapataka kufikia. Hata kama milango yote itaonekana imefungwa, wewe utaona upo mlango unaonekana umefungwa ila hujafungwa.

Siku zote unapojua umhimu wa jambo lolote lile, mawazo hasi juu ya hilo jambo yatakuwa hayapati nafasi ya kukaa, hata yakitaka kukujia yanakosa nguvu kabisa ndani yako. Wewe utakuwa unaona ushindi tu, na unapoona ushindi mbele yako, hata silaha za kukusaidia kushinda utakuwa unaziona kirahisi.

Tofauti na mtu anayeona kushindwa, yeye anaweza kujiona hawezi, sio kwa sababu ya jinsi anavyojiona kwa nje, ni vile tayari ameshashindwa ndani yake. Tumaini la kushinda vikwazo viliopo mbele yake halipo kabisa, na wala hafikiri kuwezekana kushinda.

Labda nikutolee mfano huu utanielewa vizuri zaidi, hivi umewahi kukutwa na mvua ukiwa mahali, alafu muda fulani unapaswa kufika sehemu ya muhimu sana. Yaani hutamani wala hutakiwi kukosa kwa namna yeyote ile.

Bila shaka huwa unaona mvua sio kitu kwako, tena unaweza kuiona kama vile hainyeshi, maana upo tayari kutumia gharama yeyote kufika mahali unatakiwa kufika. Na wakati mwingine kama huna usafiri wako binafsi na ule ulioagiza uje ukuchukue, ukichelewa kidogo unaweza kuanza kutembea kwa miguu, hata kama mvua inanyesha.

Huo ni mfano wa mvua, ipo mifano mingi sana, zipo changamoto nyingi sana hujitokeza mbele yetu, ambapo kwa akili ya kawaida unaweza kuona kushindwa. Ila ukijua vizuri umhimu wa kile unachopaswa kufanya, lazima utaona upenyo mbele yako.

Ukiona mtu anakwambia hawezi kwenda kanisani kwa sababu fulani fulani ambazo ukizisikiliza unaona kabisa huyu mtu amejichokea, ujue yule mtu ameondolewa ile hamu na uthamani wa kwenda kukusanyika pamoja na wenzake.

Kama hajaondolewa ile hamu ndani yake, ujue yule mtu hajaona umhimu wa hilo jambo, wala hana uzito ndani yake, afanye asifanye haoni hasara wala faida kwake, aende asiende haoni kupungukiwa kitu ndani yake, na akienda haoni kuongezeka kitu ndani yake.

Muda mwingine ndio maana unaona kunatumika ulazima, maana unakuwa huelewi unalopaswa kulitenda/kulifanya kwako. Yaani unakuwa kama mtoto mdogo asiyejua umhimu wa shule, yeye anaona kulala au kucheza ndio muhimu sana kwake.

Wengi wetu hatutajua umhimu wa kusoma Neno la Mungu, ndio maana tunakuwa na visingizio vingi vya kushindwa, yaani mtu yupo tayari kujitengenezea sababu ndogo tu. Ila akaikuza kiasi kwamba ikaonekana kubwa sana, ambapo hawezi kabisa kupata nafasi ya kusoma Neno la Mungu.

Hiyo yote ni kutojua kile kinapatikana ndani ya Biblia, lakini mtu yeyote anayejua nini anapata ndani ya Biblia iliyobeba Neno la Mungu. Huwezi kumkuta akikubali kuzuiliwa na jambo lolote lile, atakwama leo, ila amini kukwamishwa kwake atakuwa amepata njia mbadala ya kutoshindwa kwake kesho.

Tofauti kabisa na mtu mvivu asiyejua umhimu wa kusoma Neno la Mungu, huyu kila siku yeye ni mtu wa sababu za kumzuia kusoma Neno la Mungu. Sababu zenyewe ukizisikiliza unaona kabisa huyu mtu ana shida mahali, na hakubali kwamba ana shida, yeye anaona yupo vizuri tu.

Kushindwa kwako jambo, ni vile hujajua umhimu wa hilo jambo, yaani kwako ni kama jambo la ziada sana. Lakini ingekuwa umeambiwa usiposoma Neno la Mungu siku moja ujue utakufa, hata kama ingetokea nini mbele yako, ungehakikisha unasoma Neno la Mungu.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.

Facebook: Chapeo Ya Wokovu

Blog: www.chapeotz.com

Email: chapeo@chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081