Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai.
Ukikutana na aliyechoka na safari, usipokuwa mwangalifu anaweza kukuambukiza hali aliyonayo yeye wakati huo. Maneno yake yanaweza kukufanya ushindwe kuendelea na safari yako, ama macho yako yanaweza kukupa ujumbe ambao utakufanya ushindwe kuendelea mbele.
Rejea: Macho yako yataona mambo mageni; Na moyo wako utatoa yaliyopotoka. Mithali 23:33 SUV
Kumbe unaweza kumtazama aliyechoka au aliyekata tamaa, moyo wako ukakupa tafsiri ambayo itakufanya na wewe ukate tamaa. Hasa kwa yule mtu uliyemwamini, au yule uliyetegemea asingeweza kuwa vile unamwona.
Ndivyo inavyokuwa kwa mtu aliyevunjika moyo, mtu wa namna hii anaweza kuwaambukiza au kuwapandikiza moyo usio na matumaini ya kusonga mbele. Kutokana na yeye haoni tena tumaini, haoni tena kufanikiwa katika lile analolifanya katika maisha yake.
Wengi wameacha bidii kwa mambo ya Mungu, kwa sababu walikutana na marafiki zao waliovunjika moyo, waliojaza maneno ya chuki ndani yao, wenye moyo usio na toba, waliojaa hasira za mambo mabaya waliyotendewa na wengine.
Rejea: Bali kwa kadiri ya ugumu wako, na kwa moyo wako usio na toba, wajiwekea akiba ya hasira kwa siku ile ya hasira na ufunuo wa hukumu ya haki ya Mungu. Warumi 2:5 SUV.
Ukiwa na rafiki aliyejiwekea akiba ya hasira, na ukiwa na mtu unayemwamini alafu akawa amejaza maneno ya hasira/chuki moyoni mwake. Uwe na uhakika mtu yule atakuachia maneno mabaya, na kama usipokuwa mtu uliyekomaa wa kuweza kuchuja maneno, utajikuta amekuingiza eneo baya.
Uwe makini sana, hasa unapokuwa mwenye bidii kwa mambo ya Mungu, utakutana na aliyekuwa na bidii kwa mambo ya Mungu akarudi nyuma. Mtu yule anaweza asiwe salama kwako, kwanini asiwe salama kwako? Nimekuambia kwamba anaweza kukulisha maneno mabaya yaliyoujaza moyo wake.
Unaweza asikusemeshe sana, ila kutokana na wewe unavyotazama mambo, ukamaanisha ki vingine kabisa, ambapo unakuwa umeujaza moyo wako vitu visivyofaa kwako. Hasa katika safari yako ya kile ulichoamua kukifanya kwenye maisha yako.
Neno la Mungu linatusihi sana katika hili, linatueleza kwa uwazi kabisa ulinde sana moyo wako kuliko yote uyalindayo. Uwe mwepesi wa kuchuja maneno unayoyasikia na kuyaona kwa macho yako, usipofanya hivyo ujue ukishaharibikiwa moyoni mwako ujue madhara yake yataonekana kwa nje.
Rejea: Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo; Maana ndiko zitokako chemchemi za uzima. Mithali 4:23 SUV.
Nia yangu ya kukueleza haya ni ipi? Japo nimekupitisha maeneo mengi, nilitaka ujifunze zaidi ila lengo langu ilikuwa ujue hili, unapokuwa msomaji wa Neno la Mungu. Unaweza kukutana na mtu aliyejikatia tamaa, mtu aliyevunjika moyo wa kusoma Neno la Mungu, mtu wa namna hii anaweza kukupandia maneno mabaya.
Unapopandiwa maneno mabaya yasiyofaa, usipokuwa mwangalifu na wewe utajikuta umekuwa kama yeye, sio jambo la kushangaa, ndivyo tunavyojifunza kupitia Neno la Mungu.
Uwe mwangalifu sana katika safari yako ya usomaji Neno la Mungu, anaweza kutumika mtu usiyemtegemea kukurudisha nyuma. Na hutoweza kutambua wakati huo, utakuja kutambua wakati ambao unaona tabu kuanza tena kusoma Neno la Mungu.
Vizuri ukaelewa haya, itakusaidia sana katika usomaji wako, tena itakufanya uwe na akili njema, akili itakayokusaidia kuondosha mawazo potofu yanayouvamia moyo wako.
Bila shaka lipo jambo umejifunza kupitia ujumbe huu, maombi yetu kwako Roho Mtakatifu aendelee kukufundisha zaidi kadri unavyoendelea kutafakari hili.
Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Facebook: Chapeo Ya Wokovu
Blog: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081