Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa tumepata kibali cha kuifikia. Tuna kila sababu ya kuitumia vizuri hii siku, ili kuweza kumzalia Bwana matunda yaliyo mema.

Kama umekuwa makini na usomaji wako wa Neno la Mungu, utakuwa kuna vitu vipya vinakushangaza sana kuviona vimeandikwa ndani ya Biblia. Kwa mwingine inaweza ikawa kawaida kutokana na jinsi alivyolichukulia lile Neno au inatokana na vile alivyoguswa.

Kuna jambo hukuwahi kufikiri kama linaweza kupatikana ndani ya Biblia yako, ila katika kusoma kwako, ukashangaa umekutana nalo. Unaanza kusema moyoni mwako, ama hakika hakuna jambo jipya chini ya jua.

Lakini kabla ya kukutana na andiko la namna hiyo, unaweza kuliona ni jambo jipya sana, wakati huo umesahau kwamba uliwahi kukiri kwa kinywa chako “hakuna jambo jipya chini ya jua”. Kadri unavyozidi kujifunza Neno la Mungu, inatokea tena unakutana na andiko lingine linalogusa moja kwa moja kile unapitia wakati huo.

Utabaki kushanga tu, na wakati mwingine inaweza kukujia hali ya kutoamini kwa yale unayokutana nayo katika kujifunza kwako. Wakati mwingine unaweza kuona ngumu kwako kubadilika jinsi Neno la Mungu linavyokutaka uwe, kutokana na vile umekua, umekuta watu wanaenda hivyo.

Hali ya kujikuta umebaki njia panda kwa unayoendelea kujifunza, inaweza kukutokea mara nyingi sana, usipokuwa mwangalifu unaweza kuanza kuona Neno la Mungu limekosewa au unaanza kufikiri labda unatafsiri vibaya.

Hakuna cha kutafsiri vibaya japo inaweza kutokea hilo, hasa unapotumia sana akili zako za kibinadamu kuliko kumruhusu Roho Mtakatifu akufundishe zaidi jinsi inavyopaswa.

Usibaki kushangazwa na maandiko matakatifu unayoendelea kukutana nayo kwa njia ya kujifunza kwako, vyema kile kinakushangaza ukaanza kukifuata vile kinakuelekeza uishi. Inaweza kuwa ngumu kwako, ila amini kwa msaada wa Mungu mwenyewe atakusaidia.

Elewa kwamba Mungu hawezi kukuambia ishi hivi wakati anajua kabisa hakuna mwanadamu yeyote anaweza kuishi hivyo, wala hawezi kukuambia acha hili, fanya hili, ishi hivi, akiwa anajua kwako haiwezekani kuishi hivyo.

Mungu hawezi kutupa kanuni ngumu za kutukomoa, bali ametupa namna ya kuishi maisha matakatifu yanayompendeza yeye. Tukienda kinyume cha hapo tunakuwa tunamkosea yeye, hata kama sisi tutajiona tupo vizuri kwa kile tunafanya.

Uwe na uhakika kwake ni chukizo, na utaona kabisa dhamira ikikushitaki kwa hayo mabaya unayoyatenda, ikiwa tu dhamira yako itakuwa hai. Maana dhamira zingine zimeshakufaga, mtu anakuwa hasikii vibaya kwa kile anafanya.

Tushangazwe na Neno la Mungu, Mungu alivyotuwekea kila kitu ndani ya Neno lake, katika kushangazwa huko tujitahidi kuliishi Neno la Mungu. Hata kama itaonekana ni ngumu sana kwako, anza kidogo kidogo mazoezi huku ukimwomba Mungu akusaidie kuwa vile anataka yeye uwe.

Muda mwingine tumejipa hofu wenyewe za kushindwa, kwa kuogopa kujaribu kuishi vile Mungu anataka, mtu anaona vyema kuendelea kungang’ana na maisha yale yale aliyozoea kuishi nayo. Anajipa moyo kwamba amezaliwa amekuta wazazi wake wanaishi hivyo, na Mungu amekuwa akiwatumia, ndivyo anavyojitia moyo.

Kwa wewe unayejifunza Neno la Mungu kila siku, usiwe na tabia hiyo, Mungu ana kusudi jema kwako kukuonyesha Neno lake, kwa namna ambayo imekuwa ni rahisi kwako kulielewa vizuri. Ndio maana unaweza kukuta siku zote ulikuwa unasoma, ila hukuwahi kuelewa kwa namna ulivyoelewa siku hiyo.

Mungu akushangaze kupitia Neno lake, na wewe uwe tayari kubadilika, bila kuwa tayari Neno la Mungu litageuka mzigo kwako, na utafika mahali hutolifurahia.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.

Facebook: Chapeo Ya Wokovu

Blog: www.chapeotz.com

Email: chapeo@chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081