Bwana Yesu asifiwe, matumaini yetu bado unaendelea kumpenda Mungu na kumtumikia kwenye nafasi aliyokuitia. Usichoke kumtumikia hata pale unapokutana na mazingira ya kukufanya ushindwe, yeye aliyekuita yu pamoja nawe.

Leo tunaenda kujifunza jambo la muhimu sana kwenye maisha yetu, matumaini yetu mpaka kufikia mwisho wa makala hii. Utakuwa umepata jambo la kukusaidia katika safari yako ya wokovu, pia utakuwa umepata mwanga mkubwa sana.

Hasa mwaka mpya unapoanza, huwa kuna tabiri nyingi sana za manabii, na wengi wetu tunapenda kusikia Mungu ametuandalia nini mwaka mpya. Shetani baada ya kuona tunapenda sana kutabiriwa mambo mazuri na makubwa katika maisha yetu, ameamua kufanya kazi kwa nguvu sana na watenda kazi wake.

Bila kuchuja, bila kufikiri ni tabiri za namna gani, bila kujiuliza ni tabiri za kutoka wapi, bila kuchunguza kwenye maandiko matakatifu. Tumejikuta tunafurahia sana unabii ambao mara nyingi umekuwa hutumii kwetu, unaambiwa mwaka huu utakuwa hivi, utapata hichi, utapokea hichi kwa Mungu, lakini mwaka unaisha huoni hata kimoja ulichotabiriwa kitakuwa kwako.

Tena ukijaribu kuhoji mbona utabiri niliotabiriwa hukutimia, unaanza kupewa maneno mengine ya kukuchenga, utaambiwa utatimia kwa wakati wake. Je! Ni wakati gani tena? Na wakati uliambiwa mwaka huo lazima upate hicho ulichotabiriwa?

Bila kufikiri vizuri unaweza kuanza kuona Mungu ni muongo, ndio utaanza kufikiri hivyo bila kujua muongo ni huyo nabii anayekutabiria vitu vya moyo wake mwenyewe. Ambavyo ki uhakika havitoki kwa Mungu, bali alinena maono ya moyo wake mwenyewe.

Kama umetabiriwa mwaka huu utamiliki mume/mke alafu usimwone hata huyo mume/mke, si uongo? Kama umeambiwa mwaka huu hupiti bila kupata kazi, alafu ukapita bila kazi, si uongo? Kama mwaka huu uliambiwa hupiti mke/mume wako atarudi nyumbani, alafu akawa hajarudi, si umetabiriwa uongo? Kama mwaka huu ulitabiriwa hupiti utakuwa umepata kazi nzuri, alafu ukapita bila kazi, si utakuwa uongo?

Leo fikiri kwa kina kidogo, je! Mungu anaweza kusema uongo juu ya maisha yako? Ikiwa mpango umebadilika wa kutokupa hayo aliyokuambia, je! atashindwa kukujulisha tena? La hasha hatashindwa kukujulisha.

Huna haja ya kufikiri mara mbili mbili labda Mungu amekudanganya, yeye si mwanadamu aseme uongo, tena amesema mwenyewe kupitia Neno lake takatifu.

Rejea: Mungu si mtu, aseme uongo; Wala si mwanadamu, ajute; Iwapo amesema, hatalitenda? Iwapo amenena, hatalifikiliza? Hesabu 23:19 SUV.

Huenda umefika mahali umechoka, umetabiriwa sana katika maisha yako na manabii mbalimbali, ila ukikaa ukapiga hesabu hakuna unabii uliowahi kutimia katika maisha yako. Nafasi yako leo kuamka usingizini, kufunguka moyo wako, kupitia haya maandiko matakatifu ninayoenda kukushirikisha hapa.

Rejea: Bwana wa majeshi asema hivi, Msisikilize maneno ya manabii wakiwatabiria; huwafundisha ubatili; hunena maono ya mioyo yao wenyewe; hayakutoka katika kinywa cha Bwana. Yeremia 23:16 SUV.

Umeona tahadhari ya Mungu inavyosema hapo juu kwenye andiko lake? Inakuwaje wewe unatabiriwa kila mwaka, na huo unabii hautimii, umefungwa na nini hiyo hadi umeshindwa kujua huo ni unabii wa uongo. Lazima ufike mahali ushtuke, najua sio rahisi kusikia haya ninayokuambia hapa, ila angalia Neno la Mungu linasemaje.

Huenda umesikia sana makelele mengi juu ya manabii wa uongo, hadi umefika mahali umeona watu wana chuki nao. Ila fahamu wapo katikati ya kundi la manabii wa ukweli, ikiwa wa uongo wapo, fahamu na wa ukweli wapo, tena wa ukweli Mungu anawatumia haswa.

Tunapoendelea kujifunza hapa, Mungu anaendelea kutilia mkazo zaidi kupitia Neno lake, anasema manabii hao hakuwatuma yeye.

Rejea: Mimi sikuwatuma manabii hao, lakini walikwenda mbio; sikusema nao, lakini walitabiri. Yeremia 23:21 SUV.

Hawa manabii si wa uongo tu, bali hukukosesha vitu vya kiMungu juu ya maisha yako, kwa majivuno yao ya upuzi, wamefanya hayo ambayo hadi leo hujawahi kuona yakitimia kwenye maisha yako.

Rejea: Tazama, mimi ni juu ya hao wanaotabiri ndoto za uongo, asema Bwana, na kuzisema, na kuwakosesha watu wangu kwa uongo wao, na kwa majivuno yao ya upuzi, lakini mimi sikuwatuma, wala sikuwapa amri; wala hawatawafaidia watu hawa hata kidogo, asema Bwana. Yeremia 23:32 SUV.

Kutokana na ufahamu wako kushikwa na hao manabii, huenda hata haya ninayokueleza hapa, huamini kama ni kweli, na huenda ukaenda kumuuliza haya uliyosikia hapa. Nakwambia atakupindisha maneno, sio mjinga kiasi hicho akubali ukweli wa namna hii.

Labda unajiuliza utatokaje hapa, labda unajiuliza utajuaje ni nabii wa uongo, Neno la Mungu linasema tutawajua kwa kazi zao na matendo yao. Kwanza hupaswi kuendelea kujiuliza hilo, maana tangu uanze kutabiriwa huwa huyaoni hayo uliyotabiriwa, huhitaji ushahidi mwingine, huo ni ushahidi tosha.

Tumalize na Neno hili; Wala msisikilize maneno ya manabii wawaambiao ninyi, ya kwamba, Hamtamtumikia mfalme wa Babeli; maana wanawatabiria uongo. Kwa maana mimi sikuwatuma, asema Bwana, bali wanatabiri uongo kwa jina langu; nipate kuwatoeni nje, mkaangamie, ninyi, na manabii hao wanaowatabiria. Yeremia 27:14-15 SUV.

Haya yote yapo ndani ya Biblia yako, Biblia unayoiona kama adhabu kwako, sio maneno niliyotunga mwenyewe hapa, ni maneno ya Mungu mwenyewe. Vyema ukaanza kuiona Biblia yako kwa jicho la tofauti, jicho la kuona maisha yako yote yapo ndani ya Neno la Mungu.

Hakuna namna nyingine ya kufahamu haya kama husomi Neno la Mungu, unapaswa kusoma Neno la Mungu ili uweze kuwa na ufahamu wa kutosha. Hutohangaishwa na mbwembwe za manabii wa uongo, maana tayari Neno la Mungu linatenda kazi ndani yako.

Ulikuwa unasoma Neno la Mungu kwa mazoea, hivi sasa unapaswa kuanza kusoma kwa mtazamo chanya, yaani unapaswa kuliona Neno la Mungu ndio kila kitu kwako. Hapo ndipo utaanza kuona unakaa mbali na uongo mwingi wa manabii unaokutabiria yasiyopangwa na Mungu wako.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.

Facebook: Chapeo Ya Wokovu

Blog: www.chapeotz.com

Email: chapeo@chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081