Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, karibu sana tujifunze pamoja somo hili.
Ukiambiwa au ukisikia Neno la Mungu limebeba maisha ya watu, usichukulie tu kawaida, ni ukweli kabisa Neno la Mungu linakuza watu kiroho/kiakili. Kwa maana nyingine tunaweza kusema unaondolewa hatua moja ya kuhangaishwa/kuteswa na vitu vidogo vidogo, ambavyo havikupaswa kuendelea kukupa shida ndani yako.
Badala ya kuendelea kuteswa na jambo ambalo hata ungeendelea kuliwaza, hakuna faida ungeipata zaidi ya kuendelea kujiumiza moyo wako. Utageuza hilo jambo kuwa somo lako la kutorudia kosa lililokupelekea uingie kwenye shida ya namna hiyo.
Kama ulifanya kosa mwenyewe kibinadamu utaumia, kwa sababu hakupanga hufanye kosa la namna hiyo. Kuumia kwako hakutadumu moyoni mwako hadi kuanza kuleta madhara makubwa kwako, kutokana na ukomavu wako wa kiroho, utalifanya kuwa somo kwako.
Kama uliumizwa na mtu kwa namna yeyote ile, hutomweka moyoni huyo aliyekuumiza, bali kwako utakuwa umepata somo la kukusaidia siku nyingine asikuingize kwenye mazingira ya kukuumiza. Maana tayari umeshajua hadi kuumizwa, kuna mazingira yalikupelekea wewe kuumia.
Ukiona unakuwa mtu wa kulalamika sana hadi kupitiliza, ujue Neno la Mungu halipo ndani yako, maana huwezi kupata nafasi ya kumhifadhi aliyekukosea. Wakati unajua unapaswa kusemehe na kuachilia ndani yako, tena hili la kusemehe sio jambo la kufikiri mara mbili kwa mtu mwenye safari ya kwenda mbinguni.
Haijalishi umepatwa na jambo gani kwa kusababisha mwenyewe au kwa kusababishwa na mtu mwingine, geuza hilo jambo kuwa darasa kwako la kujifunza. Fanya hilo somo ulilopata ungeweza kulilipia kwa gharama kubwa sana, na gharama uliyolipia ni punguzo kubwa sana.
Labda tuseme umepoteza 5 million, badala ya kukiona kiasi kile kikubwa cha pesa ulichopoteza, ruhusu akili yako kuona somo ulilopata. Utaona somo ulilopata ni kubwa sana na lenye faida zaidi ya kiasi kile ulichopoteza, ambapo kwa akili ya kawaida utaona umerudishwa nyuma sana.
Nasema hivi, Ayubu kupitishwa katika majaribu mazito ya kupoteza mali zake na watoto wake, ni kama vile alimpa Mungu vile vitu vyake kwa muda fulani kwa makubaliano ya kuzalisha faida. Maana alikuja kupata zaidi ya vile alivyokuwa navyo, bila shaka unaifahamu sana habari ya Ayubu. Kama huijui unaweza kuisoma katika kitabu cha Ayubu, ila mimi nitakupitisha mstari mmoja.
Rejea: Basi hivyo Bwana akaubarikia huo mwisho wa Ayubu zaidi ya mwanzo wake; naye alikuwa na kondoo kumi na nne elfu, na ngamia elfu sita, na jozi za ng’ombe elfu, na punda wake elfu. Ayubu 42:12.
Nazungumza kuhusu kutokewa jambo badala ya kuendelea kunung’unika moyoni hadi ukafika mahali hilo jambo likaanza kukosesha usingizi. Unapaswa kufahamu kwamba hilo ni somo kwako, linakufanya siku nyingine uwe mwangalifu wa kutorudia makosa yale yale.
Huwezi kuzuia maumivu, ila unaweza kuyafanya yale maumivu yasidumu ndani yako. Hili linakuja kama utakuwa na maarifa sahihi ya Neno la Mungu, kukua kwako kiroho kuna mchango mkubwa sana, hasa katika kugeuza mambo mabaya yaliyokutokea kuyaona kama mtaji au faida kwako.
Tunaona Neno la Mungu halitusaidii tu kumtomtenda Mungu dhambi zile tunazozifahamu sisi, linatusaidia pia kiafya. Maana kama utaweka maumivu ndani yako kwa muda mrefu, yanaweza kukuletea madhara makubwa kwenye mwili wako.
Lione Neno la Mungu kwa sura nyingine tena kupitia somo hili la leo, kama umekuwa msomaji mzuri wa Neno la Mungu kwa muda mrefu sasa. Utakuwa shuhuda mzuri kwa hili ninalokufundisha hapa, ukianza kujifuatilia kwa umakini tangu uanze kusoma Neno la Mungu. Na kabla hujaanza kusoma Neno la Mungu, utaona kuna tofauti kubwa sana ndani yako ya kuchukulia mambo.
Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Facebook: Chapeo Ya Wokovu
Blog: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081