Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa tumepata kibali cha Bwana wetu. Tuna kila sababu ya kumshukuru Mungu na kwenda kumzalia matunda yaliyo mema.

Kukua kiroho bila kuonyesha matendo ya ukuaji wako, inaweza kutia shaka, maana kadri mtu anavyozidi kujifunza Neno la Kristo, kuna mabadiliko ndani yake yanazidi kuonekana. Na kuonekana huku ni kwa jinsi matendo yake ya nje yanavyoonyesha.

Jinsi ya kuwaza kwake kunakuwa tofauti kabisa na mtu asiyesoma Neno la Mungu au anayesoma kwa kulipua ilimradi aonekane na yeye amesoma. Ndio maana unapaswa kujijua vizuri, unapaswa kujitathimini wewe kama wewe, mara kwa mara ujue unapiga hatua au umebakia pale pale.

Huwezi kusema Neno la Mungu limenibadilisha maisha yangu, alafu unaonekana yule yule kila siku, kwa jinsi ya kutafakari kwako mambo. Tofauti yako inakuwa ndogo sana na yule ambaye hasomi kabisa Neno la Mungu.

Unapaswa kadri unavyokazana kusoma Neno la Mungu, na mabadiliko yako yazidi kuonekana kwa nje, kadri Neno la Mungu linavyozidi kukubadilisha ndani yako. Watu wengine wanaanza kuona mabadiliko kupitia matendo yako ya nje, bila hivyo huwezi kujivuna umebadilishwa kiasi kikubwa na Neno la Mungu.

Sio maonyesho kwa kila mtu, ila itaonekana tu kwa nje, kuwa huyu mtu sio yule wa miezi kadhaa iliyopita, maana viwango vyako vinaonyesha dhahiri kwa nje. Hii inavutwa au inaletwa na wewe mwenyewe, ki vipi? Kwa kuwa na kiu ya kukua zaidi ya jana au juzi.

Mabadiliko haya ya ukuaji utayaona unavyozidi kupambana zaidi kutobaki kama jana, kutoonyesha dalili yeyote ya kufanya tofauti na jana. Bado utahesabika mtu usiyetamani kusogea hatua nyingine tofauti na jana.

Vyema usomaji wako wa Neno la Mungu uonyeshe ukuaji wako, kama mwaka jana ulikuwa na mwendo fulani hivi, mwendo huo uonyeshe una mabadiliko zaidi mwaka huu. Sio kufanya vitu ki mazoea, hata kama kuna faida unapata, tamani kusogea hatua nyingine zaidi tofauti na jana.

Usibakie na usomaji wako wa mazoea, usomaji usiokua, wala usioweza kubadilisha maisha yako, bali unapaswa kuwa na usomaji unaozidi kubadilisha maisha yako kadri unavyozidi kujifunza Neno la Mungu.

Usikubali kudumaa pale pale, hata kama unaonekana upo vizuri, tamani kuwa vizuri zaidi, yaani tamani kumpendeza Mungu zaidi ya jana. Haya yote atakuwezesha yeye ukiwa na kiu, kiu inayokusukuma kumwomba Mungu akusaidie kusogea hatua zingine zaidi mbele.

Sawa na kuwa na mtoto mdogo, kama hajaanza kukaa peke yake, utakuwa unatamani akae peke yake, na akishaanza kujitegemea kukaa peke yake. Utatamani aanze kutambaa, na akishatambaa kwa muda fulani, utaona ndani yako unaanza kutamani kumwona akisimama peke yake.

Utaona hapo hakuna hatua ya makuzi ya mtoto wako, unayotamani aendelee kubakia sehemu moja siku zote. Kila hatua ya ukuaji wake unatamani asongee hatua nyingine zaidi, hivi ndivyo ilivyo kwako, hivi ndivyo ninavyokusihi hapa uwe. Unapaswa kuongezeka hatua zingine zaidi katika usomaji wako wa Neno la Mungu.

Utashangaza watu kuendelea kubakia palepale, Lakini ukionesha kusogea hatua nyingine mbele, hakuna atakayekushangaa, wala hakuna atakayeshtuka. Bali kila mtu anayekutazama atazidi kushangaa ukuaji wako unavyoenda mbele zaidi siku hadi siku, kadri siku zinavyozidi kwenda mbele unasogea hatua nyingine mpya.

Umefanikiwa kujenga tabia ya kusoma Neno la Mungu kila siku, jipongeze kwa hilo pia, ila sasa tamani hatua zingine zaidi mbele. Hiyo ndio kuonyesha kukua, kubakia hatua ile ile kila siku, hiyo sio kukua ni kudumaa eneo moja.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.

Facebook: Chapeo Ya Wokovu

Blog: www.chapeotz.com

Email: chapeo@chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081