Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, habari za leo ndugu yangu katika Kristo, Mungu ni mwema sana ametupa kibali kingine tena cha kuweza kuiona siku ya leo. Tuna kila sababu ya kumshukuru Mungu na kwenda kuitumia vizuri siku ya leo, kumzalia matunda yaliyo mema.

Kuambatana na mtu/watu wenye wito/kusudi moja la utumishi aliowapa Mungu ndani yenu mtumike katika shamba lake. Inakufanya kuwa imara kila wakati hata pale unapojisikia kuchoka, pale unapoona huwezi kuendelea mbele unapowatazama wenzako wanavyo songa mbele, wanakutia moyo na wewe.

Vizuri kuwa na marafiki wazuri mlio na nia moja, kuambatana na marafiki wenye nia moja, ni rahisi kushauriana pale mmoja wapo anapojikuta yupo njia panda kwa jambo fulani linalomkabili kwa wakati huo.

Pamoja na kuwa na marafiki wazuri wenye wito mmoja, huwa tunajikuta ule moto uliokuwa unawaka ndani yetu unazima kabisa. Wenzako wanaweza kujaribu kukuuliza shida ni nini, unaweza usiwe na majibu mazuri ya kuwapa. Unaweza ukawa unaendelea na utumishi wako aliokupa Mungu, ila ndani yako ukawa umepoa sana tofauti na siku za nyuma ulivyokuwa na ujasiri wa kukemea dhambi waziwazi.

Wakati mwingine watu wanaweza kufikiri umemtenda Mungu dhambi, ndio maana huna ujasiri wa kuisema kweli ya Mungu waziwazi, kumbe huna ovu ulilofanya mbele za Mungu. Bali ndani yako unajisikia kuchoka, hii Labda kutokana na changamoto mbalimbali ulizopitia/ulizokutana katika huduma yako.

Wakati mwingine unajiribu kujisukuma kwa nguvu kufanya huduma, unaona kabisa ndani yako vile viwango ulivyokuwa navyo havipo tena. Na sio kwamba kesho unakuwa na hamu ya kuendelea kutumika, unajikuta kadri siku zinavyozidi kwenda ndivyo unavyozidi kuchoka zaidi.

Usiogope lipo suluhisho la hayo yote, ukiwa msomaji mzuri wa Neno la Mungu, huhitaji mtu wa kuja kukusukuma wala kukupigia kelele za kuendelea mbele na utumishi alioweka Mungu ndani yako. Mungu mwenyewe kupitia Neno lake, atakukumbusha wajibu wako, atakuhimiza kuendelea na utumishi wako aliokupa.

Habari njema kabisa hii, ikiwa Neno la Mungu linaweza kukuamsha pale unapolala, pale unapojisikia kuchoka, pale unaposema utumishi sasa basi, pale unapobanwa na majukumu ya kimwili mpaka ukasahau kazi yako. Mungu mwenyewe kupitia Neno lake takatifu atakukumbusha wajibu wako.

Rejea:Piga kelele, usiache, Paza sauti yako kama tarumbeta; Uwahubiri watu wangu kosa lao, Na nyumba ya Yakobo dhambi zao. ISA. 58:1 SUV.

Unaweza kufika mahali ukachoka kuhubiri habari njema za wokovu, katika usomaji wako wa Neno la Mungu ukakutana na neno hili, USIACHE, paza sauti yako zaidi kama tarumbeta. Kwa mtumishi yeyote anajua anaposema na Mungu huwa inakuwaje ndani yake, ghafla utaona kutiwa nguvu mpya ndani yako, na moyo wa toba unakujia pale pale.

Kwanini usiendelee kulipenda Neno la Mungu, sio kulipenda tu moyoni, kulisoma na kulitafakari kwa kina, kufanya hivyo utaona ndani yako kuzidi kukua na kujengeka zaidi. Hili halitokei kwa bahati mbaya, ni vile unavyozidi kuweka juhudi zako katika kusoma Neno la Mungu.

Unaona ni kiasi gani Neno la Mungu lilivyobeba utumishi wetu, sio kwa wanaokoka tu, sio kwa washirika tu unaowaongoza, hata wewe kiongozi Neno la Mungu linaumba jambo jipya kila wakati kwenye huduma yako ya utumishi.

Tena unapaswa kujenga umakini zaidi kwenye Neno la Mungu, kwa sababu una uelewa mpana zaidi kuhusu Neno la Mungu, tofauti kabisa na mtu anayeanza wokovu leo. Mungu amekupa wito ndani yako, wito ambao unahitaji kuongozwa na Neno la Mungu.

Leo tumejifunza faida ya kusoma Neno la Mungu, linavyoweza kutumika kumsaidia mtu mwenye wito wa kiMungu ndani yake. Hasa anapofika mahali akachoka, tumeona Neno la Mungu linaweza kumpa nguvu mpya ya kuendelea mbele.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.

Facebook: Chapeo Ya Wokovu,

Blog: www.chapeotz.com

Email: chapeo@chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081