Ratiba ninayoizungumza hapa, ni ratiba ya kusoma Neno la Mungu, wengi wamekubali kuondolewa kwenye ratiba zao za kusoma Neno la Mungu. Baada ya kuingia kwenye mahusiano ya uchumba, wengine ndoa zao, wengine kazi zao, na wengine biashara zao.

Kabla ya kupata mchumba, alikuwa vizuri sana kwenye kutenga muda wa kusoma Neno la Mungu. Lakini baada ya kumpata tu mchumba, na kusoma Neno la Mungu kulikufa hapo hapo.

Kabla ya kuingia kwenye ndoa, alikuwa vizuri sana kwenye kutenga muda wa kusoma Neno la Mungu, tena pamoja na kuwa na majukumu mengi ya kazi. Alikuwa anajitajihidi sana kutenga muda wa kusoma Neno la Mungu, hata kama alikuwa anapata dakika chache, alikuwa anazitumia vizuri.

Kabla ya kupata kazi, alikuwa mtiifu sana kwenye kusoma Neno la Mungu, tena alikuwa makini sana kwenye hilo. Ila baada ya kuipata hiyo kazi, na kusoma Neno la Mungu kuliisha hapo hapo, anaweza kukuambia anabanwa sana kazini. Ila ukija kwenye uhalisia, kwenye kazi anatoka mapema kabisa, pia akiwa kazini anao muda wa kutosha kabisa kuchati kwenye magroup ya whatsApp. Ila kwenye Neno la Mungu anakwambia hana kabisa muda.

Wakati biashara iko chini, biashara iliyokuwa inatumia muda mwingi kukuza mtaji, biashara iliyokuwa inatumia muda mwingi kutafuta wateja. Alikuwa anao muda wa kusoma Neno la Mungu, tena ilikuwa haipiti siku bila kusoma. Ila baada ya mtaji kukua na kuongezeka, na kuongeza wafanyakazi wa kumsaidia kazi, ameanza kuona kusoma Neno la Mungu ni kupoteza muda.

Wakati hana biashara ya kumwingizia chochote, wakati ambao hata pesa ya kuweka bando ilikuwa shida, alikuwa anajitahidi kutenga muda wa kusoma Neno la Mungu na kupata nafasi ya kutafakari yale aliyojifunza. Ila sasa amepata kabiashara cha kumwingizia kipato, uzembe wa kutosoma Neno la Mungu umemwingia.

Unaweza kuona kumbe kuna vitu Mungu akitupa, huwa ndio tiketi ya kumwacha kabisa, lakini kabla ya kutupa tulikuwa watiifu kweli kweli. Bila kuelewa bila yeye kuwepo kwenye hicho alichotupa, kinaweza kuyeyuka tu bila kuelewa sana chanzo chake.

Wewe mume/mke wako amekukuta umejijengea utaratibu wa kusoma Neno la Mungu kila siku, wakati mko wachumba alikuwa analifahamu hilo kabisa. Imekuwaje baada ya kukuoa, kusoma kwako Neno la Mungu kumekufa ghafla? Imekuwaje baada ya kumwoa, kusoma kwako Neno la Mungu umekufa ghafla?

Unaweza ukawa na sababu nyingi sana, pamoja na hizo sababu, Jiulize Mungu anaweza kukupa mtu wake ambaye angekuja kuua kitu kilichokuwa kinamtukuza yeye? Bila shaka Mungu hawezi kukupa mwanaume/mwanamke ambaye angekuja kuua bidii yako kwa mambo ya Mungu. Ni wewe tu umeruhusu hicho kitu kiwe kwako.

Kama hujaruhusu wewe, hayo mahusiano yako uliyoingia, hayakuanza na Mungu, kulikuwa kuna kona kona. Ulipaswa kuwa zaidi ya awali, maana tayari una mwenzako anayekutia moyo wa kuweka bidii zaidi kwa mambo ya Mungu.

Alikukuta nacho, usikubali akuondolee ratiba yako ya kusoma Neno la Mungu, kama unaona kuna vitu vipya umekutana navyo. Ambavyo hukuvitegemea, hakikisha unajua namna ya kukabiliana navyo, mweleze Mungu akusaidie pale unapoona peke yako huwezi.

Haiwezekani upate kitu alafu kikakuondoa kwenye utaratibu wako wa kusoma Neno la Mungu, Neno la Mungu ni chakula chako cha kiroho. Ukiacha kulisha roho yako, kinachofuata ni kitu gani? Si kingine bali ni anguko la kumwasi Mungu wako.

Chochote kilichokujia kwenye maisha yako, kiwe kizuri sana, usikubali kikakuondoa kwenye utaratibu wako wa kusoma Neno la Mungu. Nakueleza haya upate ufahamu wa kiMungu ndani yako, ili utoke kwenye shimo lililokumeza. Hata kama mume/mke wako anaonyesha kukupenda sana, kama analeta vikwazo usiweze kuendelea na ratiba yako, hilo jambo si la kawaida. Nenda mbele za Mungu akupe akili ya kuweza kukabiliana na hayo.

Mungu akubariki sana.

Chapeo Ya Wokovu

Website: www.chapeotz.com

Email: chapeo@chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081