Kujifunza hakuna ukomo, ukijenga ukomo wa kujifunza, umetangaza kuacha kuwa mwanafunzi wa Yesu Kristo. Unapoacha kuwa mwanafunzi wa Yesu Kristo, unakuwa mtu unayeamini vile tu ulivyomeza, haijalishi vipo sawa ama havipo sawa.
Unaposoma agano la kale, uwe unajua pia na agano jipya, maana agano jipya ni bora zaidi ya agano la kale. Unapaswa kuwa makini sana kwa hili, maana agano la kale lilikuwa kivuli cha mambo yajayo, ambayo ni sasa.
Rejea:watumikiao mfano na kivuli cha mambo ya mbinguni, kama Musa alivyoagizwa na Mungu, alipokuwa tayari kuifanya ile hema; maana asema, Angalia ukavifanye vitu vyote kwa mfano ule ulioonyeshwa katika mlima. Lakini sasa amepata huduma iliyo bora zaidi, kwa kadiri alivyo mjumbe wa agano lililo bora, lililoamriwa juu ya ahadi zilizo bora. Maana kama lile la kwanza lingalikuwa halina upungufu, nafasi isingalitafutwa kwa lile la pili. EBR. 8:5-7 SUV.
Umeona huu mstari wa 7 unasema;Maana kama lile la kwanza lingalikuwa halina upungufu, nafasi isingalitafutwa kwa lile la pili.
Kama agano la kale lingekuwa bora, nafasi nyingine isingetafutwa ya kuleta hili agano jipya, maana yake lile la kwanza ambalo ni agano la kale lingeendelea kubaki.
Rejea:Maana, awalaumupo, asema Angalia, siku zinakuja, asema Bwana, Nami nitawatimizia nyumba ya Israeli na nyumba ya Yuda agano jipya. EBR. 8:8 SUV.
Leo hatuna haja ya kuchinja mnyama ndipo tujipatanishe na Mungu wetu, kama ilivyokuwa wakati wa Musa. Mtu hapaswi kutulaumu kwa hayo, maana tunalo agano bora kabisa, agano la Yesu Kristo, aliyejitoa msalabani kumwaga damu yake kwa ajili yetu.
Leo sheria haziandikwi tena kwenye mawe, sheria za Mungu zinaandikwa ndani ya mioyo yetu, na kutupa sheria zake katika nia zetu.
Rejea:Maana hili ndilo agano nitakaloagana na nyumba ya Israeli Baada ya siku zile, asema Bwana; Nitawapa sheria zangu katika nia zao, Na katika mioyo yao nitaziandika; Nami nitakuwa Mungu kwao, Nao watakuwa watu wangu. EBR. 8:10 SUV.
Umeona hapo, nakupitisha haya maandiko matakatifu ili uweze kuona utofauti uliopo agano la kale na agano jipya, leo huwezi kuingia kanisani na damu ya mnyama ukaanza kunyunyizia kila mtu, leo huwezi kuagizwa mbuzi, kuku wa kuja kutoa kafara kwa ajili ya ondoleo la dhambi. Huo utakuwa ni uganga wa kienyeji.
Tunalo agano jipya, agano bora kabisa kuliko la kwanza, katika maandiko matakatifu imenukuliwa kama kuukuu, kitu kianzacho kuwa kikuukuu na kuchakaa.
Rejea: Kwa kule kusema, Agano jipya, amelifanya lile la kwanza kuwa kuukuu. Lakini kitu kianzacho kuwa kikuukuu na kuchakaa ki karibu na kutoweka. EBR. 8:13 SUV.
Mwisho wa sheria za Musa ulimalizwa na Yesu Kristo, sio mimi ninayesema hivyo, ni maandiko matakatifu yanaweka wazi hili;
Rejea: Kwa maana Kristo ni mwisho wa sheria, ili kila aaminiye ahesabiwe haki. RUM.10 :4 SUV.
Nataka uone kitu hapa, ukiona mtu anakupinga kutokana na fundisho lako, usikimbilie kumwona hajui kitu, bali msikilize vizuri. Huenda fundisho unalong’ang’ana nalo ni kuukuu, Yesu Kristo alishaweka mambo sawa, ila kwa kutokujua kwako bado uliona linafaa.
Vile vile hupaswi kupingana na andiko, kwa vile tu limeenda kinyume na mapokeo yako. Naomba unielewe hapa, huenda ulipo hapo kuna imani unayo kuhusu jambo fulani kuwa ni sahihi kwako, hukujua kuwa kuna andiko katika agano jipya linapingana kabisa na hilo fundisho. Unapopewa andiko la kukusahisha, usione tena hilo andiko halifai, bali lichukulie kama msaada kwako.
Mwanzo nilikuambia uwe makini sana, ndio maana nilikushauri kwamba unapaswa kujua vizuri agano jipya, ili iwe rahisi kwako kuelewa unaposoma agano la kale. Usije ukaanza kusema si bora tu agano la kale litolewe tubaki na agano jipya, hapo utakuwa bado hujaelewa ninachokisema hapa.
Kila mstari unaouona kwenye Biblia yako, una maana yake kubwa sana, hata kama unauona kwa namna unaouona wewe, elewa huo mstari ipo siku ukifunguliwa ufahamu wako, utauona ukikufaa sana. Usiukatae mstari kwa namna yeyote ile, hata kama unagusa imani yako moja kwa moja, kubaliana nao, maana ndiyo iliyo kweli ya Mungu.
Mungu akubariki sana.
Chapeo Ya Wokovu
Website: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081