Usifikiri kila mahali ulipo unaweza kuona uongo/upotoshaji wa waziwazi, kama inavyoweza kujitokeza kwa manabii wengine. Kuna mahali panaweza kuwa panamwabudu shetani waziwazi, ila ukawa umefungwa ufahamu wako usiweze kuona kabisa.

Wenzako waliofunguliwa macho, wanaweza kukueleza ukweli, hapo ulipo si sahihi kabisa, hutokaa uamini, tena kila anayekuja kukueleza habari njema unaweza kumwona ni adui yako mkubwa sana. Sio kwamba unajua upo hivyo, ufahamu wako unakuwa umefungwa mahali pale watu wanapoona si mahali sahihi pa kumwabudu Mungu wako wa kweli.

Saa nyingine unaweza kupata wasiwasi kabisa kuhusu mahali ulipo, unashangaa kama vile umeonwa au umejulikana unachongaika nacho moyoni mwako. Kesho unashangaa unahubiriwa/unafundishwa yale yale yaliyojaa moyo wako kukusumbua, unaanza kuona kumbe ulianza kufikiri vibaya, wakati mahali ulipo ni sahihi kabisa.

Ndugu wengi sana wanafikiri wameokoka na kumwabudu Mungu wa kweli, ila ukweli usioweza kupingika mahali walipo si sahihi kabisa. Japokuwa wao wanaona mahali walipo ni sahihi, ila ukirudi kwenye msingi wa Neno la Mungu, unaona ni vitu viwili tofauti kabisa.

Changamoto ni kwamba hata wakiambiwa hapo si mahali sahihi, hawawezi kukubali, maana ufahamu wao umefungwa usiweze kudaka mafundisho mengine nje na yale wamemezeshwa. Unaweza kutumia nguvu zako nyingi sana za kimwili na ukatoka matupu, bila kujua unapaswa kuombea ufahamu wao, unapaswa kuombea macho yao, unapaswa kuombea masikio yao.

Maana wapo wana macho ya kuona, ila hawaoni kabisa, wapo wana masikio ya kusikia, ila hawasikii, sio kwamba hawasikii kwa jinsi ya kawaida unayoifahamu wewe. Wala sio kwamba haowaoni kwa jinsi ya kawaida, usije ukasema mbona nikiwaita wanasikia au usije ukasema mbona nikiitwa huwa nasikia, usije ukasema mbona macho yanaona na yanafanya shughuli zake vizuri.

Masikio yanayozungumzwa ni yale ya ndani, ukipata ujumbe kwa masikio ya nje uweze kuelewa vizuri kama ilivyokusudiwa. Unakuta haiwi hivyo, inakuwa kinyume chake, unaweza kusikia vizuri kabisa ila ukawa huelewi unachosikia. Kile kilicho kinyume na mapenzi ya Mungu ndicho unakuwa unakisikia na kukielewa vizuri, ila kilicho cha kweli ya Mungu unakuwa mgumu kukielewa.

Unaweza kujiuliza kiziwi mbona anakuwa husikii hata ukimsemesha kawaida ila anamwamini Mungu haswa, unaweza kujiuliza mbona kipofu wa macho anakuwa haoni kwa jinsi ya kawaida, ila anakuwa analiamini neno la Mungu. Napenda kukumbusha kwamba, Mungu ameweka kitu cha tofauti kabisa ndani yao, unaweza kushangaa kiziwi/bubu akikutazama mdomo wako jinsi unavyoongea anakuelewa, na vipofu wana biblia zao wanasoma na kuelewa kabisa.

Shida inakuwa kwa mtu ana sifa zote kibinadamu, yaani anaona vizuri, anasikia kwa jinsi ya nje tunavyomtazama. Ila anakuwa mahali ambapo hata ukimwambia si mahala sahihi hatakaa akuelewa, hata umwambie huyo nabii sio nabii anayetumiwa na Mungu, hatakaa akuelewa, lakini macho yanaona vizuri, ana masikio yanasikia vizuri sana.

Rejea: Mwanadamu, wewe unakaa kati ya nyumba iliyoasi, watu ambao wana macho ya kuona, ila hawaoni, wana masikio ya kusikia, ila hawasikii; kwa maana ni nyumba iliyoasi. EZE. 12:2 SUV.

Kumbe unaweza kukaa nyumba iliyoasi, na usijue chochote, kumbe unaweza kuwa kanisa linaloabudu mungu mwingine na usijue chochote. Sio kana kwamba huna macho, unakuwa una macho ila hayaoni, sio kana kwamba huna masikio, unayo ila hayasikii.

Watu wanakueleza weee, watakusomea kila andiko, utasoma mwenyewe biblia nzima, lakini hutaona kile Mungu anasema ndani yake. Watu wanaweza kufikiri unafanya makusudi, sio makusudi, ufahamu wako umefungwa katika nyumba iliyoasi.

Unaweza kukazana kuwaeleza watu habari njema za Yesu Kristo, ukashangaa katika watu mia asikuelewe hata mmoja au inatokea kama bahati anakuelewa mmoja. Huyo ndio anachukua hatua, hawa wengine wanakuwa wanamwona mwenzao ni msaliti, mtu aliyepotea njia ya kweli, kumbe wao walipo ni njia ya upotevuni.

Rejea: Naye akaniambia, Enenda, ukawaambie watu hawa, Fulizeni kusikia, lakini msifahamu; fulizeni kutazama, lakini msione. ISA. 6 :9 SUV.

Umeona hilo andiko, kumbe watu wanaweza kufululiza sana kukusikiliza, lakini wakawa hawasikii unachosema, wanaweza kufuliza sana kukutazama, lakini wasione. Ndivyo maandiko matakatifu yanavyosema, usipojua namna ya kushughulika nao utapata tabu sana.

Tena maandiko matakatifu yanaendelea kusema kwamba;

Rejea: Sikilizeni neno hili, enyi watu wajinga msio na ufahamu; mlio na macho ila hamwoni; mlio na masikio ila hamsikii. YER. 5 :21 SUV.

Najaribu kukupitisha mistari ya biblia ili uweze kuona vizuri hichi ninachokueleza hapa, huenda kuna ndugu yako unahaingaika naye kwa akili zako za kawaida. Atoke mahali ambapo unaona kabisa hawamwabudu Mungu wa kweli, bali wanaabudu miungu mingine, shughulika naye kwenye maombi, ombea ufahamu wake uweze kufunguka.

Hata kama wewe unaona mahali ulipo ni sahihi, huwezi kubadili ukweli kuwa ulipo sio mahali sahihi kabisa, haijalishi unaona matendo makuu yakitendeka juu ya maisha yako, haijalishi unaona miujiza mbalimbali ikitendeka kwako. Unapaswa kujua kwamba hata shetani naye ana miujiza yake anawatendea watu wake.

Unaposoma Neno la Mungu, hakikisha umeokoka na jitahidi kumwomba Roho Mtakatifu akusaidie kuelewa ule ujumbe uliokusudiwa kwako. Mwambie Mungu afungue ufahamu wako uweze kuelewa vizuri Neno lake, vinginevyo utakazana kusoma Neno la Mungu utakuwa huoni, wala husikii chochote.

Mungu akubariki sana.

Chapeo Ya Wokovu

Website: www.chapeotz.com

Email: chapeo@chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081