Unaweza ukawa unasali mahali, ukapapenda kutokana na jinsi wanavyoendesha ibada zao, jinsi wanavyokuwa huru kwa mambo fulani, jinsi wasivyojali mambo mabaya yanavyotendwa na waumini, na wasio waumini wao.

Jinsi wanavyopenda mambo ya dunia kuliko ya Mungu, wao hakuna tofauti ya mtu anayeimba nyimbo za kidunia na anayeimba nyimbo zenye kumtukuza Mungu katika roho na kweli.

Siku moja nikimsikia mtumishi mmoja akihubiri washirika wake, akawaambia kusikiliza nyimbo za bongofleva haina shida kabisa. Tena akawapa na maelekezo, akawaambia wawe wanasikiliza nyimbo za mapenzi. Kwa sababu watu wanapenda uhuru wa kuendelea kufanya maovu yao bila kubanwa na sheria za Mungu mioyoni mwao, watamwona mchungaji wao, nabii wao, mtume wao, na mwalimu wao yupo sawa.

Ukiona kanisa au kikundi fulani kinaruhusu mambo ya ovyo, hawapendi kusikia kweli ya Mungu, wanapenda sana kusikiliza injili ya uongo, wanapenda kusikia utabiri wa uongo. Wapenda zile tabiri za mwaka huu hutopita lazima ufanikiwe sana, hata kama ni uongo, wao wanapenda tu kusikia hivyo. Ujue hapo upo sehemu isiyo salama.

Ukiona upo mahali wanazuia waonaji wa Mungu, wasione mambo ya kiMungu, wao wanapenda uwapake pake uongo usio na ukweli wa Mungu ndani yako. Fahamu hao watu, ni watu waliomwasi Mungu wao, mioyo yao imejaa uasi.

Nakueleza haya uweze kuelewa vizuri, unapokutana na jambo kama hili, uwe unajua pa kuanzia, kuliko kutokujua ukaanza kuhangaika na wakati mwingine ukaona labda wapo sahihi kwa wanayofanya.

Unaweza kufika mahali, kusema uongo kwao ni jambo la kawaida kabisa, tena wanaona ni jambo zuri, na kiongozi wao anawaunga mkono kwa hilo. Maana hawezi kukemea hilo, na wakienda kumuuliza kama ni sahihi, atawajibu ni sahihi.

Mhubiri anayekuja kuwahubiri ataelekezwa cha kuhubiri, ataambiwa aseme maneno yadanganyayo, yaani yasiyo na kweli ya Mungu ndani yake. Na nabii anaweza akaambiwa kabisa usitabiri unabii wa ukweli, tabiri uongo.

Kusoma kwao Neno la Mungu wanaweza wakasoma, ila wakawa wanasoma kwa namna ambayo wamefundishwa, namna ambayo hawawezi kukubali kweli ya Mungu. Na wakati mwingine wanaweza kupandiwa kitu ambacho kitawafanya wasiwe na muda wa kujifunza Neno la Mungu wakiwa peke yao.

Wao wanachopenda kusikia kwao ni utabiri wa maneno laini usio na ukweli ndani yake, wanapenda mahubiri laini yasiyogusa tabia zao mbaya. Maana ni watu waliomwasi Mungu wao, na shetani amewabana kila kona wasiweza kusikia kweli ya Mungu, wakamrudia Mungu wao.

Rejea: Kwa maana watu hawa ni watu waasi, watoto wasemao uongo, watoto wasiotaka kuisikia sheria ya BWANA; wawaambiao waonaji, Msione; na manabii, Msitoe unabii wa mambo ya haki, tuambieni maneno laini, hubirini maneno yadanganyayo. ISA. 30:9-10 SUV.

Umeona hilo andiko, huenda ulianza kufikiri ninayokueleza hapa ni mambo ambayo hayapo ndani ya Biblia yako, yapo kabisa. Usifikiri haya unayoyaona ni mambo mapya, sio mapya, tayari Mungu alishasema kupitia Neno lake.

Mungu hawezi kusema mambo ya uongo, wala Mungu hawezi kukuahidi mambo ya uongo, wala hao manabii hakuwatuma yeye watabiri. Wanajua wao amewatuma nani watabiri uongo, kwa sababu ya kutokujua kwako Neno la Mungu, unasema Bwana amewatuma.

Rejea: Wameona ubatili, na uganga wa uongo, hao wasemao, BWANA asema; lakini BWANA hakuwatuma; nao wamewatumainisha watu ya kuwa neno lile litatimizwa. Je! Hamkuona maono ya bure, hamkunena mabashiri ya uongo? Nanyi mwasema, BWANA asema; ila mimi sikusema neno. EZE. 13:6‭-‬7 SUV.

Acha kuhangaika na nabii za uongo, huku ukiendelea kumtenda Mungu dhambi, tubu dhambi zako, uanze kuishi maisha matakatifu yanayompendeza Mungu wako. Utaona akitenda mambo makuu katika maisha yako. Tena utaanza kuona ukiambiwa kweli ya Mungu, huwezi kuikataa.

Ijue kweli ya Mungu kupitia Neno lake takatifu, utatambua mengi sana kupitia Neno lake takatifu, hutoyumbishwa na jambo lolote. Hata manabii feki utawatambua kwa matendo yao, hata makusanyiko yaliyomwasi Mungu utayatambua kwa matendo yao.

Mungu akubariki sana.

Chapeo Ya Wokovu

Website: www.chapeotz.com

Email: chapeo@chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081