Ukitaka kujenga tabia yeyote ile nzuri, kuna gharama utapaswa kuilipa, utapaswa kuwa mvumilivu kila hatua, utapaswa kujisemehe pale unapokosea kanuni ulizojiwekea. Hutapaswa kuwa na kisingizio chochote kinachokufanya usiendelee na zoezi lako la kujenga tabia mpya unayopenda iwe kwako.

Tunachokuja kushindwa kuelewa, ni pale tunapojihisi tumechoka, badala ya kuendelea kufanya kile tumejipangia kila siku kukifanya. Tunaacha kufanya kwa sababu ya uchovu wa miili yetu, tunapojipa nafasi ya kupumzika, hapo ndipo tunapotoa nafasi ya kujirudisha nyuma.

Wengi wetu zoezi la kusoma Neno la Mungu linaonekana ni jambo gumu sana kwetu, tunapoanza hili zoezi la kusoma Neno la Mungu, mara nyingi tumejikuta tunaishia njiani. Hii kuishia njiani muda mwingine imetokana na sisi wenyewe kuvunja ratiba yetu tuliyojiwekea ya kusoma Neno la Mungu.

Unapokubali kupumzika siku moja, wakati huo huna hata mwaka katika usomaji wako wa Neno la Mungu. Nakwambia utakuwa umejikwamisha mwenyewe, utakuwa umekubali kurudi kule kule pa zamani wakati husomi kabisa Neno la Mungu.

Ndio maana nilitakungulia kusema, unapotaka kujenga tabia mpya, unapaswa kuwa mvumlivu sana, tena mtu asiyejipa sababu nyingi za kutokufanya. Bali unapaswa kuwa na sababu nyingi za kufanya kuliko za kushindwa kufanya.

Siku unayojikuta umechoka sana au hujisikii kabisa kusoma Neno la Mungu, usikubali hiyo siku ipite bila kusoma Neno la Mungu. Hakikisha unasoma hivyo hivyo, bila kujali hali ya udhaifu uliyonayo wakati huo.

Kupumzika kusoma Neno la Mungu, ona kwako ni kosa kubwa sana, usikubali kabisa kuvunja ratiba yako, wala usijipe mapumziko ambayo hukuyapanga. Kwanini nasema hivyo; Biblia unayo kwenye simu yako, huna sababu ya kusema leo sipo nyumbani, huwezi kusema leo nimesahau kubeba Biblia, huwezi kusema leo nimeona uvivu kubeba Biblia.

Simu yako ni Biblia yako, nina maana kwamba, smartphone yako ina uwezo wa kuhifadhi Biblia, unapofika mahali upo mbali na Biblia yako ya kawaida. Unaweza kusoma iliopo kwenye simu yako, unaweza kuona ni jinsi gani hupaswi kujipa sababu ya kutokusoma Neno la Mungu.

Nazungumzia kuchoka, hili wengi wameliruhusu bila kujua lina madhara kwao, kuchoka kupo, ila usikubali kukutawale hadi ukashindwa kutekeleza ratiba yako ya siku. Mpaka pale utakapo hakikisha tabia ya kusoma Neno la Mungu imejengeka moyoni mwako, kiasi kwamba huwezi kuacha siku ipite hivi hivi bila kusoma Neno la Mungu.

Unaweza kuoga maji ya baridi kuondoa uchovu kwa muda fulani ili uweze kusoma Neno la Mungu, sura moja ya kitabu haiwezi kukushinda. Haijalishi umechoka sana, kama umeweza kula chakula, kama unaweza kupokea simu, kama unaweza kujibu sms, kama umeweza kuingia kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii. Hutoshindwa kusoma sura moja ya Biblia, tena ukiamua unaweza kusoma zaidi ya hapo.

Tangu mwaka 2015, nimejiwekea utaratibu wa kusoma Neno la Mungu kila siku isipokuwa siku ya jpili, maana ni siku ya ibada na kutafakari yale niliyojifunza kanisani. Sijawahi kuacha hadi leo, ninachokueleza hapa ni kitu ninachokifanya kila siku, kama mimi nimeweza na wewe utaweza. Maana nilikuwa mvivu haswa huenda kushinda hata wewe unayefikiri huwezi, ila nilipoamua kutojipa sababu yeyote nimefanikiwa.

Shughuli zako za kutwa nzima zinaweza kukufanya ukachoka sana, ila hakikisha unapata dakika chache za kusoma Neno la Mungu. Ukiona mchana au jioni au usiku inakuwa ngumu kwako kusoma Neno la Mungu, soma ile alfajiri/asubuhi unapoamka. Tenga dakika chache za alfajiri/asubuhi, tena ni muda mzuri uliotulia na akili yako inakuwa na nguvu, na utulivu wa kutosha.

Chukua hatua uone mabadiliko.

Chapeo Ya Wokovu.

Website: www.chapeotz.com

Email: chapeo@chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081