Usifikiri unachokifanya hakitakuwa na upinzani, hata usipomtangazia mtu yeyote kuwa huwa una utaratibu wa kusoma Neno la Mungu kila siku. Utafika mahali mtu atazungumza tu neno litakugusa vibaya, na kukuvunja moyo wa kuendelea kusoma Neno la Mungu. Anaweza akawa kiongozi mkubwa unayemweshimu, anaweza kuwa mzazi wako, anaweza akawa mlezi wako, anaweza akawa rafiki yako, na anaweza akawa ndugu yako.

Kama ndio ulikuwa unaanza zoezi la kusoma Neno la Mungu, alafu ukakutana na maneno magumu yasiyo na bembelezo/faraja kwako. Unaweza kuona ya nini kuendelea kujihangaisha kusoma Neno la Mungu, na wakati napata shida kulielewa, sio hilo tu, unakuwa na uvivu mkubwa wa kusoma Neno la Mungu. Inapotokea mtu yeyote akakuvunja moyo hata kama yeye hajui kama amekuvunja moyo, utaona bora uache tu.

Bila kuelewa yeye anaweza asipate hasara yeyote, maana huenda hajui kabisa ulichokuwa unafanya, na kama anajua ulichokuwa unafanya. Anaweza asijue kilichokufanya uache kujifunza Neno la Mungu, shetani anaweza akawa amemtumia kwa namna ambayo hata yeye huenda asijue kama alitumiwa kukutoa kwenye mpango wako wa kila siku.

Unapaswa kuwa makini sana kwa hili, zipo njia nyingi sana za kukuvunja moyo, unaweza kumwona mwenzako jinsi anavyotiririka katika uchambuzi wa Biblia. Kwa kuwa wewe bado hujapata huo uwezo, badala ya kupata wivu wa kusoma zaidi Neno la Mungu, unavunjika moyo na kushindwa kuendelea mbele.

Anaweza akatokea mtu tu, akakuta unasoma zako Biblia, akakutupia ka neno kakakuondoa kabisa kwenye utaratibu wako wa kusoma Neno la Mungu kila siku. Kwa mfano anaweza kukuambia hivi, na wewe utaiweza Biblia? Imetushinda sisi tuliokoka siku nyingi, wewe mtoto wa juzi utaiweza? Au akatokea mwingine akakuambia, wachungaji wenyewe Biblia inawashinda, itakuwa wewe ambaye hata chuo chenyewe cha Biblia hujaenda.

Nakuambia yanaweza yakawa maneno machache, ila ni maneno yenye sumu kali sana kwa mtu ambaye hakujipanga kukutana nayo. Kuanzia siku hiyo utaona ile bidii yako inazidi kupotea taratibu, hutojua moja kwa moja kilichokuvunja moyo ni yale maneno uliyoambiwa.

Chunguza vizuri kilichoondoa bidii yako ya kusoma Neno la Mungu ni nini, utakuta ni jambo dogo tu, unaweza kusingizia majukumu yamekuwa mengi. Kumbe sio majukumu ni maneno ya marafiki zako, ndugu zako, wazazi/walezi wako, ndio yaliyokuondoa kwenye usomaji wako wa Neno la Mungu. Siku ulivyoongea na rafiki yako, ndugu yako, mzazi wako, hayo maneno aliyokuambia yamechangia kiasi kikubwa kuacha kwako kusoma Neno la Mungu.

Hii changamoto ipo kwenye jambo lolote unalolifanya, unavyomwona mtu amefika pale alipo, kuna mambo mengi sana ya kuvunja moyo amekutana nayo. Hakuwa mwepesi kukubali kurudi nyuma, pamoja na kuna wakati aliona bora aache, ila alijitia moyo wa kusonga mbele. Ndio maana unamwona hapo alipo, ukimwona mnyama yeyote porini ni mzee sana ujue ameishinda mishale mingi sana.

Jipange kisawasawa kwenye usomaji wako wa Neno la Mungu, usikurupuke kwa hili utaishia njiani, nakueleza lililo kweli. Hii shughuli sio ya mchezo mchezo, unapaswa kujitoa haswa, unapaswa kuwa tayari kukabiliana na lolote lile mbele yako. Maana lazima utafika mahali utavunjwa moyo, huenda hapo ulipo umeshavunjwa moyo na una siku kadhaa hujasoma Neno la Mungu.

Usikubali kuacha kusoma Neno la Mungu kwa sababu yeyote ile, unayo Roho Mtakatifu ndani yako, huyo ndiye kiongozi wako wa kukusaidia kuelewa unachosoma. Achana na maneno ya watu hayatakufikisha mahali popote, zaidi yatakurudisha nyuma.

Mungu akupe kuona haya, usije ukaacha kusoma Neno lake.

Chapeo Ya Wokovu

Website: www.chapeotz.com

Email: chapeo@chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081.