Na Shealtiely Molla.
Leo napenda kukushirikisha ushuhuda huu uliotumwa na mwanafamilia mwenzetu tunayesoma naye Neno la Mungu katika group la WhatsApp la Chapeo Ya Wokovu, unaweza ukakujenga zaidi, hasa wewe unayeona usomaji wa Neno la Mungu ni mgumu kwako.
Shalom family.
Huu ni ushuhuda wangu kuhusu usomaji wa Neno la Mungu kila siku.
Kwanza nikiri wazi huko nyuma, sikuwahi binafsi kusoma Neno la Mungu kila siku bila kukosa, kwa mfululizo kama jinsi nilivyoanza kufanya toka December 2017 nilipojiunga na familia hii ya Chapeo Ya Wokovu.
Kabla ya kujiunga humu utaratibu ulionisaidia kusoma Neno la Mungu kila siku ni ule wa ibada za kwenye familia yangu, lakini kama mtu binafsi ilikuwa ngumu.
Nilijaribu kutumia njia na miongozo mingi lakini hakuna kilichodumu zaidi ya wiki.
Nilitafuta msaada wa Mungu kwa muda mrefu sana, kwa kweli najua kuwemo humu Chapeo Ya Wokovu ni jibu la maombi yangu.
Baada ya kujiunga Chapeo Ya Wokovu WhatsApp Group, ilinichukua kama mwezi kujifunza kwa niliowakuta humu, na kufuatilia sana makala za ‘SOMA NENO UKUE KIROHO’. Mungu akubariki sana Samson Ernest(mwanzilishi wa huduma hii)
Nilishangaa kuona baadhi ya wana wa Mungu wakitoa tafakari kila siku. Kwangu hao niliwachukua kama role models wangu na kuona inawezekana hata kwangu.
Nilikusudia moyoni kuiga mfano wao, kwani biblia inaturuhusu kuiga mema ya wengine.
Nilikutana na upinzani mwingi lakini sikukubaliana na dunia wala mwili, katika kutimiza takwa hilo la kuiga mifano hiyo bora.
Kidogo kidogo kuna mambo yasiyo na msingi nilianza kuyapa kisogo, ili nipate muda wa kusoma Neno la Mungu na kutafakari kile nilichojifunza.
Kule mwanzoni nilivyojiunga, sababu kubwa ilikuwa ni kutii zile sheria za group, na hasa ile aibu ya kutolewa eti kwa sababu ya kushindwa kwenda na lengo kuu la group. Namshukuru Mungu level hiyo sasa nimeivuka, ila nimebakia na nidhamu niliyojiwekea mwenyewe. Nasoma kwa faida yangu na ya ufalme wa Mungu.
Binafsi mara nyingi Mungu hunipa Neema ya kusoma Neno la Mungu baada ya maombi ya usiku, na pia ndani ya muda huo husoma chapter(sura) ya siku na kuandaa tafakari yangu, kisha ufikapo muda uliopangwa, huandika nilichojifunza na kutuma tafakari yangu.
Ninaona mabadiliko makubwa katika utumishi na maisha yangu kijumla, kwa sababu takwa la Mungu ni kuliangalia Neno lake alitimize. Sifa na Utukufu wote ni kwa Mungu.
Ushuhuda huu ni kumtia moyo mtu fulani ya kwamba kama kweli una Roho Mtakatifu ndani yako, inawezekana kabisa kupata muda wa kutosha, wakati mwingine kwa kujilazimisha. Usisubiri sana kutiwa moyo, kwani tokea nyakati za Yohana Mbatizaji mambo ya ufalme wa Mungu hutekwa na wenye nguvu.
Tukiijua kweli ya Neno la Mungu tutakuwa huru mno, vinginevyo uchanga wa kiroho hautatutoka na tutayumba, na kuyumbishwa huku na kule.
Sijafika bado, ila nakaza mwendo kujitahidi kujaza Neno la Mungu katika moyo wangu, kwani matunda yake nayaona dhahiri katika maisha yangu, tofauti na siku za nyuma.
Mungu akubariki sana kusoma ushuhuda huu.
Je, unapenda kujiunga na group la WhatsApp, la kusoma Neno la Mungu kila siku? Na una simu yenye uwezo wa WhatsApp? Karibu sana uungane na familia hii, wasiliana nasi kwa WhatsApp namba 0759808081. Tuma ujumbe kwa njia ya WhatsApp tu.
Usiache kujifunza Neno la Mungu.
Chapeo Ya Wokovu.
www.chapeotz.com
+255759808081.