Kila mmoja wetu anapaona mahali anaposali ni sahihi, iwe sio sahihi, yeye atapaona ni sahihi, hata ukijaribu kumwonyesha maandiko matakatifu mbalimbali. Uwe na uhakika tayari analo jibu la kukwepa hilo andiko, kosa si lake, tangu utoto wake amejikuta anasali pale. Mafundisho mengi yamemkaa moyoni mwake, yamemfanya asione ubaya wa kanisa lake.

Inaweza isiwe dini ya zamani sana, inaweza ikawa huduma mpya kabisa, ila kupitia huduma ile alipata msaada juu ya shida yake iliyokuwa inamkabili kwa muda mrefu sana. Huenda alizunguka sana maeneo mengi hakupata msaada, ila kupitia dini hiyo mpya, alivyoingia mahali pale, akapata suluhisho la tatizo lake. Mtu huyu uwe na uhakika hutaweza kumwondoa kirahisi isipokuwa kwa neema ya Mungu tu.

Wakati mwingine tumekazana kuwaonyesha watu maandiko matakatifu, tunapowatazama kama vile wanafanya makusudi. Ufahamu wao umefungwa katika dini, dini yeyote hata kama inamwabudu baali, uwe na uhakika washirika wake watakuwa wamejengwa vizuri. Watakuwa na mafundisho ya kina sana yanayowalinda wasiyumbishwe na yeyote atakayetaka kuwashawishi waachane na dini hiyo potofu.

Usijivune sana upo mahali sahihi, wanamwabudu Mungu wa kweli, na wanafuata Neno la Mungu linavyosema. Hebu kaa chini utafakari isingekuwa wazazi wakowanasali mahali hapo unaposali sasa, ungekuwa upo hapo unaposali sasa? Bila shaka ungekuwa mahali tofauti kabisa, kama ungekuta wazazi wako wanaabudu ng’ombe, na wewe ungejiunganisha humo humo, maana umekua umekuta wanafanya hivyo.

Labda wa kujiweka kifua mbele ni yule ambaye alifanya maamzi sahihi baada ya kuhubiriwa kweli ya Mungu, akamua kujitoa kwenye dini ya wazazi wake na kuhamia mahali alipoona wanamwabudu Mungu katika kweli yote. Yaani hakuna upagani ndani yake, wanaliishi Neno la Mungu pasipo kulichakachua, hata kama linaenda kinyume na mambo wanayoyapenda.

Usije ukafikiri watu hawaoni Neno la Mungu, usije ukafikiri wanafanya utani unapowaonyesha maandiko matakatifu wanakwepa. Dini/dhehebu walipo sasa, tangu utoto wao wanasali mahali pale, wazazi wao wamewalea wakiwa kwenye dini hiyo hiyo unayokazana wewe kuwaambia haipo sawa.

Huenda bado hujanielewa vizuri ninachosema hapa, ngoja nikupe mfano huu; wewe umezaliwa kwenye nyumba ambayo jiko la kupikia ni mkaa mpaka unakua iko hivyo, leo umeenda nyumba ambayo jiko lao ni la umeme. Usipoambiwa jiko letu la kupikia ndio hili, unaweza kulitafuta jiko la mkaa humo ndani mpaka ukachanganyikiwa, wakati hata hilo jiko la mkaa halimo humo ndani.

Sio kulitafuta tu, ukiambiwa hili ndilo jiko letu la kupikia unaweza kukataa kabisa kuwa hilo sio jiko la kupikia. Unachojua wewe tangu utoto wako, jiko ni la mkaa. Hii ni tahadhari kwa wanaume wanaoa, usije kuanza kugombana na mke wako, kwa sababu ya kushindwa kufanya baadhi ya vitu. Rudi nyuma utazame mazingira aliyolelewa na mazingira uliyomleta wakati huo.

Binti wa watu hajawahi kuona nazi, wala hajui matumizi yake, leo hii unamletea unamwambia nipikie wali nazi. Uwe na uhakika hiyo nazi itapikwa jinsi ilivyo na ganda lake, usicheke ni ukweli, labda awe na mtu wa kumuuliza, sio mtu tu, awa na ujasiri huo wa kuuliza. Fikiri kama ana aibu ya kutotaka kuonekana hajui, kitakachofanyika hapo usije ukalaumu.

Umeanza kunielewa sasa, kwa hiyo unapaswa kurudi kwenye shina/mzizi, ujue huyu mtu kwanini anasoma neno la Mungu. Lakini habadiliki, fahamu kwamba mapokeo ya dini yake yamemjaa sana, misingi ya dini yake imeutawala moyo wake. Ana hoja nyingi zenye nguvu, tena ukienda vibaya kama hujajipanga anaweza kukuebisha mchana kweupe kabisa.

Najua ulikuwa unashindwa kuelewa nini shida inayowafanya watu wang’ang’ane na dini zao zinazoenda kinyume na Neno la Mungu. Tunajua Yesu Kristo hakuleta dini duniani, alileta wokovu, dini ni mpango wa mwanadamu kumwendea Mungu. Katika dini hizo zipo ambazo zinaweza kukufanya usione mbingu, utasema hata kama upo dini nzuri unaweza usione mbingu. Huo ni ukweli, ila elewa hilo ni suala la mtu binafsi, mimi ninachosemea hapa ni mahali pasio sahihi na mahali palio sahihi.

Mungu akusaidie kuelewa haya, ndio maana ni muhimu sana kuweka pembeni mapokeo ya dini yako unaposoma Neno la Mungu. Ruhusu Roho Mtakatifu akusaidie kuelewa, omba Mungu afungue ufahamu wako unaposoma Neno la Mungu. Omba Mungu akupe stamina ya kukubaliana na ukweli hata kama unaenda kinyume na mapokeo ya dini yako.

Mungu akubariki sana.

Chapeo Ya Wokovu.

Website: www.chapeotz.com

Email: chapeo@chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081