Wazo lenye nguvu sana na linalopata kibali haraka unapokuwa kwenye mapito fulani magumu katika maisha yako, ni wazo la kuacha kufanya kile kizuri ulichokuwa unakifanya. Utapata msukumo mkubwa wa kuacha kwanza mambo yaliyokuwa yanakujenga kiroho, hasa kama ulikuwa mtu unayejitoa kwa mambo ya Mungu.

Kweli kuna mambo unapaswa kuyapunguza katika ratiba zako za siku, pale unapoona huna uwezo tena wa kutelekeza mambo yote uliyojipangia kufanya. Ila fahamu kwamba yapo mambo ukiacha unajirudisha nyuma hatua kubwa sana, hasa kwa mambo ya kiroho na baadhi ya mambo ya kimwili.

Mfano, unaweza kupuuza kwenye eneo la malezi ya watoto wako, kwa kufikiri upo bize sana huwezi kupata nafasi ya kukaa na watoto wako ujue maendeleo yao yakoje. Utajikuta umeruhusu kuwa na watoto wasio na adabu, watoto wasio na maadili mazuri, maana mzazi ulikuwa bize na mambo yako. Hata kama mambo hayo yalikua muhimu sana, ulisahau hata suala la malezi ya watoto wako lilikuwa jambo la muhimu sana.

Pamoja na kubanwa sana, unaona hapa kuna mambo huwezi kuacha kuyapa muda wa kutosha, hata kama itatokea jambo linalokufanya ukose utulivu wako uliokuwa nao siku za nyuma. Itakubidi uwe na muda wa kufanya kile unapaswa kufanya, hata kama unaona hutafanya kwa ubora sana, usikubali wazo hilo la kuacha likakutawala, vizuri kufanya hata kwa muda mfupi ila kwa ubora.

Kwanini nakueleza haya yote, wengi tunapenda kuacha kusoma na kutafakari Neno la Mungu pale tunapojikuta tunapitia changamoto ngumu za maisha. Wazo la kwanza na la mwisho tunalopataga, ni kuacha kwanza kusoma Neno la Mungu mpaka pale tutakapokuwa vizuri.

Nimekueleza sana hili kwenye makala nyingi zilizopita, na nazidi kukusisitiza hili usiache kusoma Neno la Mungu kwa sababu yeyote ile. Najua hutakuwa na nafasi ile ile kila siku, yaani kama leo umebanwa sana, hutoendelea kubanwa hivyo siku zote, lazima upo wakati utakuwa huru. Na kama leo upo huru sana kufanya mambo yako, elewa hutokuwa hivyo kila siku, kuna wakati utabanwa sana na majukumu mengine nje na hayo.

Unapaswa kuelewa vizuri hili, kuacha kusoma Neno la Mungu kwa sababu yeyote ile ni kosa kubwa mno, kwanini ni kosa. Hebu fikiri tangu utoto wako hadi leo mtu mzima, hujawahi kuwa na ratiba ya kusoma Neno la Mungu. Na kama uliwahi kuwa na ratiba ya kusoma Neno la Mungu, hukuwa unasoma kama sasa unavyosoma, alafu leo hii unataka kujipumzisha! Nakwambia unajirudisha kule kule pa zamani.

Wengi wanaokuja kwangu kuomba ruhusa ya kupumzika kwanza kusoma Neno la Mungu, huwa siwaruhusu kabisa kufanya hivyo. Najua hawatarudi tena hata kama changamoto yao waliyokuwa wanapitia itaisha, na kama watarudi tena itachukua muda mrefu sana kurudi.

Kusoma Neno la Mungu ni zoezi ambalo linalonekana ni gumu sana, kwa sababu wengi wanakuwa wanaanza vizuri, ila baada ya muda wanashindwa kuendelea. Hili linakuja kwa hizi sababu zinazokueleza hapa, kuruhusu kupumzika kwa namna yeyote ile, ni kujirudisha nyuma kabisa.

Nakueleza haya kwa sababu najua, ukitaka kwenda kwa mtiririko mzuri, usikubali kukatisha usomaji wako kwa namna yeyote ile. Ukichunguza vizuri utakuta hujawahi kuacha kula chakula siku nzima kwa sababu ya kubanwa sana au kwa sababu ya kuumizwa sana. Lazima kuna kitu utakula, hata kama sio kwa kiwango kizuri, ila kuna kitu utapeleka mdomoni.

Usiseme mbona kuna kufunga kula, kufunga ni habari tofauti kabisa na kuacha kula chakula, kufunga unakuwa kwenye maombi maalum mbele za Mungu. Kama umewahi kufuatilia vizuri, njaa ya mtu alifunga na ambaye hajafunga alafu akawa hajala tu kwa sababu zozote zile, njaa hizi mbili, za aliyefunga na asiyefunga, zipo tofauti kabisa. Hata mimi sielewi kwanini huwa inakuwa hivyo.

Ukiamua kusoma Neno la Mungu kila siku, usije ukajidanganya kupumzika kwa namna yeyote ile, itokee dharura tu ambayo hukuipaga ikakufanya ukashindwa kusoma Neno la Mungu. Ila hakikisha kesho yake unaendelea na ratiba yako ile ile, zaidi ya hapo utajikuta unapoteana.

Mungu akubariki sana.

Chapeo Ya Wokovu

Website: www.chapeotz.com

Email: chapeo@chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081