Kuna mambo unaweza kuona uache kuyafanya kwanza wakati unapitia changamoto, bila kujua mambo mengine hupaswi kuacha hata kama unapitia wakati mgumu. Maana muda utakaopoteza hadi hiyo changamoto ije ipite, huwezi kuja kuurudisha huo muda ulioupoteza.

Yapo kweli mambo unaweza kuyapunguza kuyafanya kabisa mpaka pale utakapokuwa sawa, ila yapo mambo huwezi kuyapunguza wala kuyaondoa kwenye ratiba zako. Labda ubadilishe muda wa kuyafanya na sio kuacha kabisa, tuseme labda kila siku ikifia saa 5:00 alfajiri ulikuwa unapata muda wa kumshukuru Mungu na kuikabidhi siku yako mikononi mwake. Kutokana na huo muda umeingiliwa na ratiba nyingine ngumu badala ya kuacha kuomba, itakubidi uangalie muda mwingine nje na huo.

Sasa wengi wetu tukishaona ule muda tuliozoe kufanya mambo yetu umeingiliwa na jambo lingine, tunaona ni heri kuacha hilo jambo. Kisingizio kikubwa nimekuwa bize sana siku hizi, siwezi kuomba tena Mungu, amesahau maombi yale ndio yanamsaidia kufanikisha mipango yake.

Changamoto zinakuja na kuondoka, ila muda unaoupoteza kwa kuacha kufanya mambo ya msingi, kwa sababu ya changamoto ngumu unayopitia. Inakunyima fursa kubwa sana, maana hiyo changamoto itapita, na muda uliopoteza wakati huo hutoweza kuurudisha nyuma ili uzibe hilo pengo.

Wengi tunaacha kusoma Neno la Mungu, kwa sababu tu tumepatwa na changamoto fulani, bila kuelewa hiyo changamoto tuliyopata ilikuwa sio ya kutufanya tuache kusoma Neno la Mungu. Mtu anakwambia kwa sasa najiona sina utulivu, nimeona niache kwanza kusoma Neno la Mungu mpaka pale nitakapokuwa sawa.

Hakuna kitu kama hicho, hapo ndio itakuwa mwanzo wako wa kupoteana kabisa kwenye kusoma Neno la Mungu, tena huwezi kuja kuurudisha muda uliopoteza wakati unasubiri changamoto unayopitia iishe. Kama ulikuwa unasoma sura moja kwa siku, alafu ukapumzika mwezi/miezi, nakwambia utakuwa umepoteza sura nyingi sana.

Haijalishi unapitia changamoto gani ngumu, kama hiyo changamoto haihusiani na macho yako, yaani namaanisha kama huna tatizo la macho kuona. Unapaswa kuendelea kusoma Neno la Mungu, bila kujalisha kuna jambo linakusumbua sana moyo wako hadi unafika mahali unakosa kabisa utulivu.

Pamoja na kukosa utulivu wako uliokuwa nao kabla hujapatwa na hayo unayopitia sasa, jaribu kutuliza mawazo yako. Hata kama sio kwa kiwango chako ulichokizoea, ni bora zaidi kuliko kuacha kusoma Neno la Mungu hadi hayo unayopitia yapite kwanza.

Usijipe sababu yeyote ya kukwama kusoma Neno la Mungu, jitahidi kutulia pale unapoona unakosa utulivu. Hata kama hutosoma kwa kiwango ulichozea, ni bora zaidi kuliko kuacha, nakueleza hili ili usipate sababu ya kuacha kusoma Neno la Mungu.

Wengi walianza vizuri kusoma Neno la Mungu, pale walipokutwa na changamoto, waliona wapumzike kwanza kusoma Neno la Mungu hadi pale changamoto itakapoisha. Cha ajabu changamoto imeisha na kusoma Neno la Mungu kumeishia hapo.

Kama umeshaona changamoto inaondoka na usomaji wako wa Neno la Mungu, kwanini uruhusu kuacha kusoma Neno la Mungu? Hupaswi kuruhusu hilo kwako. Kupumzika kwako iwe kufikia kwenye kusoma Neno la Mungu baada ya mizunguko yako ya siku nzima, Neno la Mungu liwe chakula chako cha kulalia.

Ukiona kusoma Neno la Mungu usiku inakupa shida, hakikisha unapoamka tu, pale unapomaliza kumshukuru Mungu kwa sala au kabla hujamshukuru Mungu kwa sala. Hakikisha unapata dakika chache za kusoma Neno la Mungu, badala ya kuendelea kujiona unazidiwa na majaribu/changamoto, utajiona unatiwa nguvu zaidi.

Usiache kusoma Neno la Mungu kwa changamoto zinazopita, macho yako ni mazima, huna sababu ya kusitisha zoezi la kusoma Neno la Mungu. Hata kama ungepoteza viungo vingine vya mwili wako, lakini kama bado macho yako ni mazima, endelea kutafuta Mungu anasema nini juu ya maisha yako kupitia Neno lake.

Soma Neno Ukue Kiroho.

Chapeo Ya Wokovu

Website: www.chapeotz.com

Email: chapeo@chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081.