Tumeshuhudia ndugu zetu, marafiki zetu, na majirani zetu, wakipoteza maisha yao na wengine kupatwa na mishtuko ya ajabu, kwa sababu ya kupoteza mali zao. Wengine mahusiano yao ya ndoa/uchumba kuharibika, wengine kufukuzwa kazi waliyokuwa wanafanya, na wengine kuondokewa na wapendwa wao.

Haya mambo yamewafanya wengi sana kuchukua maamzi ya kujiua, mtu alikuwa na mali nyingi, alivyofilisika akaona ajiue, mwingine walipoachana na mume/mke wake. Akaona achukue kamba ajinyonge, mwingine akaona anywe sumu afe.

Kukosa kwake maarifa sahihi ya Neno la Mungu, yaliyo na pumzi ya Mungu ndani yake, bahati mbaya anakutana na mtu asiye na Roho wa Mungu ndani yake. Akamshauri jambo baya, ushauri huo mbaya unaweza kumpelekea kufanya maamzi mabovu.

Mtu asiyemcha Mungu, lazima awe na ushauri mbovu, tena humpoteza jirani yake kwa ushauri usiofaa. Na wengi tusio na muda kutafuta maarifa ya Mungu, huwa tunakutana na ndugu/majirani zetu wasiomcha Mungu. Tunaomba ushauri kwao, badala kutupa ushauri mzuri, wanatupa ushauri mbaya.

Rejea: Asiyemcha Mungu humpoteza jirani yake kwa kinywa chake; Bali wenye haki watapona kwa maarifa. Mithali 11:9.

Mtu asiyemcha Mungu, mtu asiyependa mafundisho ya Neno la Mungu, mtu huyu hayupo salama, atapotea mwenyewe na atampotosha mwingine atakayepata nafasi ya kuzungumza naye. Hebu fikiri mtu wa namna hii yupo kwenye changamoto ngumu na hamchi Mungu, akakutane na rafiki yake asiyemcha Mungu pia. Lazima mtu huyu apate ushauri mbaya kwa rafiki yake, ushauri usiomjenga bali kumharibu.

Lakini ukisoma ule mstari b yake inasema hivi;Bali wenye haki watapona kwa maarifa. Mithali 11:9b. Je! wenye haki ni akina nani hao? ni wale waliompokea Bwana Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wa maisha yao. Wanaoishi maisha ya kumpendeza Mungu wao, yaani wanaojiepusha na matendo maovu/machafu, wanaopenda haki, hao ni wenye haki. Rejea: Asiye haki hukopa wala halipi, Bali mwenye haki hufadhili, hukirimu. Zaburi 37:21.

Unaweza kuona ni jinsi gani ilivyo hatari kwa mtu asiye na Yesu Kristo moyoni, unaweza kuona ilivyo hatari kwa mtu aliyeokoka, alafu hana maarifa ya Neno la Mungu. Mtu huyu akipatwa na changamoto ngumu, atatolewa haraka sana kwenye njia ya uzima na kuingia njia ya mauti.

Kukosa neno la Mungu ndani ya nafsi yako si vizuri, maana kukosa maarifa ndani ya nafsi yako, unajipeleka kumkosea Mungu wako. Unakosa ulinzi wa kiMungu ndani yako, maana tayari umeruhusu roho ya uasi imekuwa ndani yako.

Rejea: Tena si vizuri nafsi ya mtu ikose maarifa; Naye afanyaye haraka kwa miguu hutenda dhambi. Mithali 19:2.

Kuwa na maarifa ya Neno la Mungu ni salama sana kwa mkristo yeyote yule, unaporuhusu kukosa maarifa sahihi ya Neno la Mungu, unaruhusu uangamivu wa nafsi yako. Dhambi itakuingia kirahisi, kwa sababu huna kinga ndani yako, kupotoshwa itakuwa rahisi kwako, kwa sababu huna chujio ambalo ni Neno la Mungu.

Kuepukana na hayo yote, lazima tuwe na kiu ya kutafuta maarifa ya Neno la Mungu, Neno la Mungu ndio linatufanya tuishi. Unapokosa Neno la Mungu ndani ya nafsi yako, umekosa jambo la msingi sana, utakuwa mchanga wa kiroho siku zako zote.

Utapatwa na changamoto ngumu, utashindwa kuhimili maumivu yake, na misukosuko yake, maana ni makali mno. Lakini yule aliye na Neno la Mungu moyoni mwake, au aliye na mafundisho ya Neno la Mungu, mtu yule ni salama sana. Atapitishwa kwenye jaribu ngumu, lakini utamwona anatoka salama, lakini wewe usiye na maarifa ya Mungu, changamoto ngumu inaweza kukuondoa/kukuangusha.

Usiruhusu nafsi yako ikose maarifa ya Mungu, ni jambo la hatari sana kwako, jaza moyo wako Neno la Mungu, huwezi kushindwa kupata nusu saa kila siku ya kusoma Neno la Mungu.

Kujifunza iwe kanuni yako ya maisha.

Chapeo Ya Wokovu.

Blog: www.chapeotz.com

Email: chapeo@chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081.