Huna muda mwingine zaidi ya ulionao sasa wa kufanya mambo yako kwa uhuru unaoutaka, huo muda mchache unaouona sasa. Usiuchezee kwa kufikiri utapata mwingine mwingi zaidi, utakuwa unajidanganya mwenyewe.
Kama umekaa unasubiri uwe na muda wa kutosha kufanya mambo yako kwa uhuru mkubwa, utakuwa unajidanganya, tena utakuwa unapoteza nguvu nyingi sana. Ambazo ulipaswa kuzitumia wakati huo ila hukuzitumia kwa kufikiri utapata muda mwingine zaidi ya huo.
Changamoto iliyopo ni kwamba, muda husubiri mtu, siku zenyewe zinaenda tu, iwe una furaha sana zenyewe zinaenda tu, uwe una huzuni sana zenyewe zinaenda tu. Hakuna siku muda utakusubiri, uwe umemaliza mambo yako, uwe hujamaliza mambo yako, wenyewe hukusubirii.
Iwe siku hiyo ulipaswa kwenda kazini mapema, lakini ukaamka mvua zinanyesha sana, muda hujali mvua inanyesha sana ukusubiri. Utakuta wenyewe unaenda tu, usipojiongeza kutumia chombo kinachokukinga na mvua. Ili kukufikisha kwenye kituo chako cha kazi, utakuwa umeipoteza siku ki hivyo. Na kama kazi yako mvua ikinyesha huwezi kufanya chochote, jua siku hiyo ndio imepotea hivyo haiwezi kurudia tena.
Kama muda huwezi kukusubiri wewe hata siku moja, haijalishi ulipatwa na nini, inakuwaje wewe unausubiri? Unasubiri upate muda gani mzuri ndio uanze kusoma Neno la Mungu? Miaka nenda rudi wewe unasubiriaga tu upate muda mzuri, kama nia yako ni kupata muda mzuri, mbona huo muda mzuri hujawahi kuupata?
Unajidanganya ndugu yangu, muda mzuri ni huo ulionao sasa, usikubali kupoteza siku yako kizembe bila kusoma Neno la Mungu. Acha habari za kusubiri upate muda mzuri ndio uje uanze kusoma Neno la Mungu, unajiona sasa umebanwa sana na masomo ya shule/chuo. Nakwambia hata siku ukimaliza hayo masomo yako, hutoweza kupata huo muda unaoufikiria utaupata.
Wengi sana walisema ngoja nikimaliza chuo nitakuwa na muda wa kutosha wa kusoma Neno la Mungu, baada ya kumaliza chuo hawakuupata huo muda. Ndio maana nakwambia Usijidanganye utapata muda mwingine zaidi ya huo ulionao sasa.
Hakikisha unapenyeza ratiba yako ya kusoma Neno la Mungu kwa namna yeyote ile, usikubali kauli ya “umebanwa sana huwezi kusoma Neno la Mungu”. Huko ni kuendelea kujididimiza chini mwenyewe, hakuna siku utakuwa na uhuru unaoutaka wewe wa kukupa hamu/kiu ya kusoma Neno la Mungu.
Kama umeshindwa sasa hivi kujipa nusu saa ya kushika Biblia yako na kuanza kuisoma na kutafakari yale uliyojifunza. Nakwambia hakuna siku utaamka, utakuwa na huo muda unaoutaka wewe, badala yake utakuwa na muda wa kutosha kuimba Wimbo wa ahadi isiyotimia.
Kama unasubiri upite kwanza changamoto unayopitia sasa, na kama unasubiri kwanza ujisikie vizuri, utakuwa unajidanganya vibaya sana. Hakuna siku changamoto zitakuisha, ikiisha hiyo inayokukabili leo, kesho inakuja nyingine mpya kabisa tena kwa namna ya tofauti.
Lazima uwe na uelewa wa haya mambo, vinginevyo utazidi kupoteza muda wako zaidi na zaidi, maana Neno la Mungu lenyewe unapaswa kujitoa haswa. Si unaona ukishika Biblia na kuanza kuisoma usingizi unakujia ghafla, na wakati ulikuwa unachati na simu karibia masaa mawili hukusinzia ila umeshika Biblia imekuwa tabu.
Usipojitoa ki kweli kweli, utakuwa unateswa na hiyo hali kila siku, maana shetani anajua ukilijua Neno la Mungu, utakuwa umepata kitu kikubwa sana ndani yako tena cha thamani kubwa. Ndio maana anajaribu kukuwekea vikwazo vya kila namna, ili uweze kuona huna muda wa kutosha wa kusoma Neno la Mungu.
Mungu akusaidie ufunguke zaidi katika eneo hili.
Chapeo Ya Wokovu.
Blog: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.