Kuna mahali lazima ufike uanze kujihoji, inakuwaje unasoma Neno la Mungu kila siku, ila bado unazidi kudanganywa na manabii wa uongo, wachungaji wa uongo, mitume wa uongo, Wainjilisti wa uongo, na walimu wa uongo.

Lazima ufike mahali ujiulize inakuwaje unasoma sana Neno la Mungu, lakini bado huoni yale makatazo ya Mungu, badala yake bado unatenda yale yale yanayokatazwa. Cha kushangaza zaidi hujisikii vibaya moyoni mwako kuendelea kuyatenda hayo.

Unaweza kujiona una amani nyingi moyoni mwako ukafikiri amani hiyo imetokana na Mungu, kumbe hiyo amani haijatokana na Mungu wako. Bali imetokana na mapokeo ya mafundisho uliyolishwa, mafundisho yale yamekufanya ujione upo sahihi na salama, ndio amani yako inapotokea.

Unaweza kuwa unasali vizuri kabisa, unatoa huduma vizuri kabisa, unaweza kuwa mwombaji sana, ila ukawa umefungwa mahali. Maana wewe kama wewe unajisikia amani kuwepo mahali pale, huna mashaka na mahali pale, huenda hii imetokana na tangu utoto wako umejikuta unasali mahali hapo.

Huenda kuna mtu wako wa karibu sana unayemwamini sana, alikushawishi uingie mahali ulipo mpaka sasa. Na tangu uingie unaona ni mahali pako sahihi, watu wakijaribu kukuambia au ukiwasikia wanasema mahali fulani ulipo wewe sio mahali sahihi, unajisikia moyoni mwako kuwachukia sana.

Ipo shida mahali, shida yenyewe ni hii, umefumbwa macho yako ya ndani usiweze kuona, yaani macho yako ya ndani yametiwa upofu, kwa kawaida unajiona unaona ila huoni chochote. Masikio yako ya ndani yametiwa kiziwi, unafikiri unasikia ila husikii chochote, maana hata unachosikia huelewi unaambiwa nini. Japo kwa kawaida unaonekana unasikia, na mtu akikuita na kukusemesha unamsikia vizuri.

Yesu Kristo aliliona hili jambo mapema, hata kama watu watakataa na kujiona wapo salama, hata kama watabisha usiku na mchana. Bado hawataweza kubadilisha ukweli wa hili jambo, wapo watu wakitazama hawaoni, na wakisikia hawasikii, wala hawaelewi wanachokisikia.

Rejea: Kwa sababu hii nasema nao kwa mifano; kwa kuwa wakitazama hawaoni, na wakisikia hawasikii, wala kuelewa. Mathayo 13:13.

Hili ni muhimu sana kulijua, linaweza kukusaidia hata kwenye malenzi ya watoto wako, unaweza kuhangaika sana na mtoto wako. Kila ukimwonya kwa fimbo asifanye jambo fulani, unamkuta kesho amefanya yale yale. Unaona kutumia fimbo labda vibaya, unaona bora kuongea naye kawaida, nayo inashindikana, unafikiri labda ukitumia ukali kuongea naye huwa hakuelewi.

Unajaribu kutumia mazungumzo ya upole sana kumwelimisha, cha ajabu anakuitikia vizuri na kukuonyesha amekuelewa sana ila kesho unamtuka amezidisha zaidi kufanya kosa lile lile.

Hili ndilo linalotukumba wengi hasa tunapofika kwenye eneo la imani zetu, ukweli wapo wana macho ya kuona ila hawaoni. Wapo wana masikio ya kusikia ila hawasikii, wala hawaelewi wanachosikia, japo kibinadamu wanaonekana wanasikia vizuri.

Vizuri ukaombea ufahamu wako, vizuri ukaombea masikio yako, na vizuri kuombea macho yako, ili uweze kuelewa kile unachokiona, na kuelewa kile unachokisikia. Unaweza kusoma Biblia yako yote, ukairudia tena na tena, kama macho yako yakitazama hayaoni, kama masikio yako yanasikia ila hayasikii. Itakuwa ni kazi bure.

Tutahangaishana sana, tutawahangaisha wengine kutuonyesha maandiko mbalimbali yanayokataza tunayofanya, yanayoonyesha tunayoamini sio sahihi. Bado haitosaidia jambo lolote, maana tumefungwa uelewa wetu.

Muhimu sana kulichukulia hili kama changamoto kwako, usijione upo salama hapo ulipo, wala usidhirike na hatua uliyonayo sasa. Nikiwa na maana kwamba, hupaswi kujiona huna haja ya kumwomba Mungu afungue zaidi ufahamu/uelewa wako. Hapo ulipo unasoma sana Neno la Mungu, lakini kuna maneno unasoma ila huyaelewi, na kama unayaelewa sio kwa kiwango kile unachopaswa kuelewa.

Mungu atusaidie sana.

Chapeo Ya Wokovu

Blog: www.chapeotz.com

Email: chapeo@chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081