Unapoanza kujenga tabia yeyote ile mpya katika maisha yako, inahitaji uamue kweli kutoka ndani ya moyo wako, bila kuangalia nani anakutazama. Kuacha kwako tabia fulani mbaya na kuanza kuishi tabia nyingine mpya na inayompendeza Mungu wako, hupaswi kujenga fikira za kutaka kuonekana na kundi fulani hivi.

Labda unataka kuolewa/kuoa, na huyo anayetaka kukuoa/kumuoa hapendi tabia fulani mbaya kwako, kwa kuwa umependa na unahitaji awe mwenzi wako wa maisha. Unaamua kutubu na kuachana na hiyo tabia mbovu, unaanza kuishi maisha fulani tofauti kabisa na mwanzo.

Inatokea siku mmeachana kabla ya kuwa wanandoa ile tabia yako ya zamani unairudia tena na kuacha ile tabia yako nzuri uliyoanza kuishi. Kwa sababu tu aliyekuwa anaipenda hiyo tabia yako nzuri amekuacha badala ya kuendelea kuishi tabia yako ile ile njema, unarudi kwenye tabia yako mbaya.

Tabia ya kujenga tabia fulani nzuri kwa ajili ya kutaka kuonekana na wengine, haitokufikisha mbali sana utarudi kwenye tabia yako ile ile. Kujenga tabia mpya na nzuri inahitajika nidhamu ya hali juu, na kuendelea kuishi hiyo tabia kila siku unapaswa kujitoa kweli kweli bila kuangalia nani ananitazama.

Kuacha tabia fulani kwa ajili ya kumfurahisha mtu fulani, siku ukigundua hafurahii hiyo tabia kwa kukuona unaingiza na sio kwamba kweli umeamua kubadilika. Utarudi kwenye kile ulichokuwa unakiishi kila siku, maana ulikuwa unaigiza na sio kwamba uliamua kabisa kutoka ndani ya moyo wako kwa ajili ya manufaa yako mbele za Mungu.

Wapo watu wanarudi nyuma kihuduma, moja wapo ni hili la kuanza huduma kwa ajili ya kutaka kuonekana na watu, akiona anafanya kila juhudi na watu hawaonyeshi sana kumjali kwa kile anafanya. Anavunjika moyo na kuacha kabisa kumtumikia Mungu wake, anarudi kwenye maisha yake ya zamani.

Hapo ndipo unapojiuliza, huyu alipata wito wa kumtumikia Mungu wake kweli au kuna kitu kilimsukuma kufanya hivyo. Maana utumishi ulio ndani ya mtu, huwezi kuondolewa na kutokuonwa na wengine, kwanza Mungu akiweka wito ndani ya mtu. Mtu yule hawezi kutulia, utamvunja moyo sasa hivi ila baadaye utamwona ameinuka tena.

Kinachomwinua huyu mtu ni ule moto unaowaka ndani yake, hana uwezo wa kutulia kabisa, ukimwekea vikwazo vya kila namna. Utamwona ameinuka kwa namna nyingine tena, tena zaidi ya mwanzo, maana anayemfanya awe hivyo ni Roho wa Mungu aliye ndani yake.

Tofauti na mtu anayeanza huduma ya Mungu kwa kutaka kuonekana na watu wengine, yaani mtu anaanza kuimba nyimbo za kumsifu Mungu ili kupata umaarufu mkubwa kama mwimbaji fulani anayempenda yeye. Huyu ndugu hatofika mbali sana, kwanza atamalizwa na wale watu wanaomwambia sauti gani hiyo ya unayoimba wewe. Na akikutana na kundi lingine la watu ambao hawashtuki na nyimbo zake, hapo ndio anaona kama kuimba ndio hivi ngoja nirudi kwenye maisha yangu ya kutokuimba.

Changamoto hii imeenda hadi kwa wanaoanza kusoma Neno la Mungu, kuna mtu anaanza kusoma Neno la Mungu kwa malengo ya kuonekana na watu/mtu fulani. Siku akitimiza haja ya moyo wake, anapotea na kupotea kabisa, kwa sababu kile alichokuwa anakitafuta ameshakipata kwa wale/yule aliyemlenga amwone.

Watu wa namna hii huwa hawaondoki na fundisho lolote la kuwasaidia katika maisha yao ya Wokovu, maana wao hutafuta kuonekana kwa watu na sio kwa ajili ya kutaka kujenga uhusiano wao mzuri na Mungu wao. Na sio kutaka kujua Mungu anasema nini juu ya maisha yao kupitia Neno lake.

Kuepukana na hili, usisome Neno la Mungu kwa malengo fulani ya kutaka kutimiza haja ya mwili wako, usisome Neno la Mungu kwa kutaka kuonekana na watu. Kufanya hivyo haitokufikisha popote pale badala yake utaishia kuacha.

Neno la Mungu ni tamu sana ikiwa utalisoma bila kuangalia nani atakutazama, nani atakusifia, na nani atakuona mcha Mungu.

Mungu akubariki sana.

Chapeo Ya Wokovu

Blog: www.chapeotz.com

Email: chapeo@chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081