Kuona haraka kile unafanya kina msaada mkubwa kwako, inaweza ikawa ngumu kwako kutokana na unavyojitazama kwa nje. Kutokana na vile unavyojilinganisha na wengine waliokutangulia au wale mliokuwa nao pamoja ila wao wameonyesha kufanikiwa zaidi.
Unaweza kujitazama kabla hujaanza hicho unachofanya sasa, na baada ya kuanza hicho unachofanya sasa, unaweza usione yale mabadiliko makubwa uliyoyategemea uyapate. Badala yake ile bidii yako uliyoanza nayo ikaanza kupoa kutokana na matokeo uliyojipa.
Unachopaswa kukijua ni kwamba, chochote unachoamua kukifanya, ile tu kuanza kufanya kuna maana kubwa sana. Unachopaswa kujua utapaswa kuendelea kufanya kile umeamua kukifanya kila siku, bila kuangalia mazingira, bila kujipa sababu za kuacha.
Kama umeamua kuamka kila siku asubuhi na mapema, usifikiri utakuwa ni uamzi utakaokupa furaha, usifikiri ni zoezi ambalo litakuwa rahisi sana kwako. Linaweza likawa ni zoezi gumu sana kwako, likakupa shida sana siku za mwanzo, tena unaweza kufika mahali ukaona ni mateso.
Usipokuwa makini unaweza usione faida unayopata ukiamka asubuhi, badala yake unaweza kuona hasara unazopata ukiamka asubuhi na mapema. Hii itakufanya ufikiri kuacha kabisa kuamka mapema au inaweza kukuletea uvivu wa kujiona bora kulala kuliko kuamka mapema, alafu hakuna cha zaidi unachopata.
Hali kama hizi zinatukumbuka kwenye maeneo mengi tunayoanza kuyafanyia kazi, wengi tunapenda kufurahia mafanikio makubwa ya mtu bila kutazama gharama alizotoa kufika hapo alipo. Tunafikiri ni bahati tu kufikia viwango alivyofikia, kumbe yapo mengi amekutana nayo hadi kufikia pale.
Hili ndio linawasumbua wasomaji wengi wa Neno la Mungu, mtu anaanza kusoma leo Neno la Mungu anataka wiki/mwezi huo huo aone mabadiliko makubwa ndani yake. Bila kufahamu kujenga tabia mpya na nzuri ni mchakato wa muda mrefu, mchakato unaohitaji nidhamu na uvumilivu wa hali ya juu.
Unapoanza kusoma Neno la Mungu tu, ni hatua kubwa sana umeichukua, utahitaji kujenga nidhamu ya hali ya juu kuendelea kusoma Neno la Mungu kila siku. Unaweza usione mabadiliko unayoyataka kuyaona ila fahamu kwamba, kuna mabadiliko ndani yako yanazidi kujenga/kuumbika taratibu ndani yako hadi kuja kuyaona dhahiri.
Utachukua muda mrefu kidogo mpaka kuja kuwa vile unatamani kuwa, ukweli huu lazima ufahamu mapema, na nalazimika kukueleza ukweli huu ili uweze kukusaidia katika usomaji wako wa Neno la Mungu. Hutakiwi kupata shida sana ndani yako, haijalishi unajionaje sasa, haijalishi unaonaje kiwango chako cha uelewa. Hupaswi kufikiri hakuna unachofanya, kipo kikubwa sana unazidi kuwekeza ndani yako.
Usitishike na matokeo madogo unayoyaona kwa nje, matokeo hayo madogo yanazaa kitu kikubwa sana ndani yako. Huwezi kukiona leo ila yaja siku utajipongeza kwa maamzi sahihi ulyofanya ya kusoma Neno la Mungu. Kwa sasa nakushauri uendelee kuwa mvumilivu, haijalishi unajionaje ila fahamu jambo moja tu “usiache kusoma Neno la Mungu”.
Najua kuna mtu huwa unajilinganisha naye, umejikuta badala ya kukutia moyo wa kusonga mbele, amekuwa sehemu ya kukuvunja moyo wa kusonga mbele. Kitu usichokijua ni kwamba, hadi amefikia hapo, kuna gharama kubwa sana ametoa, ipo gharama ya muda ametoa. Hii ndio gharama kubwa kuliko zote, muda ndio kitu kinasumbua wengi sana.
Hapo ulipo, vile unajiona haupo imara sana tangu uanze kusoma Neno la Mungu, jipe muda wa kutosha, endelea kukazana zaidi kwa kuweka bidii zaidi katika usomaji wako wa Neno la Mungu. Nakuhakikishia baada ya muda fulani utaona mabadiliko hayo makubwa unayoyatamani.
Mfano mzuri ni kwangu, zamani nilikuwa nikishika tu Biblia kusoma naanza kusinzia palepale, ila siku hizi najishangaa sana hiyo hali ya kusinzia ovyo haipo tena. Badala yake siku hizi nikishika Biblia kusoma napata nguvu inayosukumwa na hamu ya kutaka kujua Mungu anataka kusema nini juu ya maisha yangu kupitia Neno lake.
Kama kwangu hali ya kusinzia ovyo imetoweka, hata kwako inawezekana kabisa kutoweka. Endelea kuweka bidii zaidi hata pale unapokutana na changamoto, hata pale unapoona hakuna mabadiliko yeyote ndani yako, wewe soma tu.
Mungu akubariki sana.
Chapeo Ya Wokovu
Blog: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081