Nilichogundua ni kwamba, jambo lolote kuliamua kulifanya kutoka ndani ya moyo wako bila kujalisha kitatokea nini mbele yako. Hilo jambo litawezekana, utakutana na vikwazo vya kila namna ila utapata njia nyingine ya kulifanya.

Mtu anaweza kusingizia sijafanikiwa kufanya hili jambo, kwa sababu nilikuwa nimebanwa sana na majukumu, ukirudi katika uhalisia utaona kuna nafasi alikuwa nayo ya kufanya hilo jambo alilopaswa kulifanya. Ila hakulifanya kutokana na uvivu/uzembe wake wa kufikiri alikuwa anao muda wa kutosha kufanya hilo.

Wakati mwingine badala ya kuanza na hilo analopaswa kulifanya, anaanza na mambo mengine madogo madogo. Ambapo hayo mambo yanakula muda wake mwingi na kumaliza nguvu zake nyingi, mpaka kuja kujaribu kufanya kile alipaswa kufanya, anakuwa ameshachoka.

Wengi wanafikiri hawana muda wa kusoma Neno la Mungu, ndivyo wanavyofikiri hivyo ila tukirudi katika ukweli unakuta sio kweli. Ule muda aliopaswa kusoma Neno la Mungu, anaingia kwanza kwenye mitandao ya kijamii kufuatilia mambo mbalimbali. Akija kushtuka amemaliza lisaa limoja, na anakuwa ameshachoka.

Mwingine, muda wake mwingi anaumaliza kwenye magroup ya whatsApp kwa kuchati, kwenye mijadala ya mabishano na mikuruzano mbalimbali huwezi kumkosa. Ukimuuliza ndugu vipi mbona husomi Neno la Mungu, atakwambia nabanwa sana na majukumu sina muda wa kutosha.

Huyu ndugu anayekuambia hana muda wa kutosha, haipiti nusu saa hajaingia whatsApp kuangalia mijadala mbalimbali kwenye magroup. Humkosi instagram kila muda, humkosi facebook akilaiki kila picha za marafiki zake.

Huyu ndugu anayekuambia yupo mazingira ambayo hayana umeme, simu yake inamaliza haraka moto anashindwa kushiriki Neno la Mungu kwa kutoa tafakari yake. Kama tulivyojiwekea utaratibu wetu katika group la WhatsApp la Chapeo Ya Wokovu, simu yake hii inamaliza moto kwenye kuchati, na kuingia kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii.

Akija kurudi kutaka kufanya jambo la msingi, simu yake inakuwa imeshamaliza moto zamani, itaachaje kumaliza moto na wakati imeshinda masaa mengi ikiingia kwenye mitandao mbalimbali. Cha maana sana anachokipata unakuta ni kidogo sana kulinganisha na hasara anayoipata.

Huyu ndugu anayekuambia bando la internet kwake ni Changamoto kubwa, huyu ndugu akiweka vocha na kujiunga bando la internet. Sehemu yake ya kwanza kukimbilia ni YouTube, humu ataangalia videos za kila aina, akitoka hapo hana salio kwenye simu yake. Muda wa Neno unafika anakuwa amechoka, na anakuwa hana bando la internet.

Mbaya zaidi ndugu huyu hawezi kusoma Neno la Mungu akiwa peke yake, ndio maana tukaweka utaratibu wa kusoma Neno la Mungu kwa pamoja katika group la WhatsApp la Chapeo Ya Wokovu. Hili group linamjengea mtu yeyote nidhamu binafsi ambayo hakuwahi kuwa nayo hapo kabla. Anaposhindwa kuenendana na matakwa ya group, inakuwa ngumu kwake kujisimamia yeye mwenyewe.

Nikupe mfano hai, nilichojiwekea sasa hivi, siku za hivi karibuni, nitabanwa sana na majukumu ila sitaacha siku ipite bila kusoma sura moja ya Biblia Takatifu. Nitachoka sana siku hiyo ila sitaruhusu uchovu huo unizuie kusoma sura moja ya kitabu cha Biblia, haijalishi hiyo siku nitaamkia nipo wapi, sitakubali siku iishe bila kusoma Neno la Mungu.

Haitajalisha nitakutwa kwenye makelele mengi kiasi gani, nitaondoka kifikra katika mazingira yale ya makelele nitaingia kwenye kusoma Neno la Mungu. Makelele yataendelea kupigwa ila sitayasikia, kwa sababu tayari nimeshaondoka kifikra/kimawazo eneo lile japokuwa mwili upo pale pale.

Unaweza kujiuliza maswali inakuwaje hii, ngoja nikupe mfano rahisi, si umewahi kuona umekaa na marafiki zako. Ghafla ukawa unafikiri jambo fulani nje na mazungumzo yanayoendelea hapo, akatokea mtu akakushtua!! We vipi mbona una mawazo sana?

Hujawahi kuona upo darasani, mwalimu anafundisha weee, kumbe wewe haupo kimawazo darasani, mwalimu anaweza kukuona. Anakuja kukuuliza nilikuwa nafundisha nini, ukashindwa kumjibu, maana hukuwepo mahali pale. Hivyo ndivyo kuondoka kifikra/kimawazo.

Ndani ya Neno la Mungu kuna madini ya ukweli, yaani unaweza ukawa kwenye jaribu fulani zito sana, kupitia kusoma kwako Neno la Mungu. Ukapata tumaini jipya, ukatiwa moyo kwa namna ambayo hukuitegemea, ukakutana na mstari uliobeba majibu ya maombi yako.

Yawekana umeomba sana miaka mingi kuhusu jambo fulani, ila siku hiyo unasoma Neno la Mungu ukakutana na majibu ya maombi yako. Unaweza kujiuliza imekuwaje ila ndio utakuwa ukweli wenyewe.

Ndio maana nakwambia kuacha kusoma Neno la Mungu sijui kama itatokea tena kwangu, naelewa kuna gharama kubwa kufikia hatua ya kulipenda Neno la Mungu kwa vitendo na si kwa maneno. Ninaachoamini ni kwamba ukiamua inawezekana, bila kujalisha mazingira yakoje kwako.

Jiwekee mkakati madhubutu ambao hutouvunja, haijalishi ulijingiza kusoma Neno la Mungu kwa bahati mbaya. Hakikisha hufanyi makosa, haijalishi itatokea nini siku hiyo, ilimradi macho yako yanaona, hakikisha unasoma Neno la Mungu.

Unapokuwa safarini, hakikisha unasoma Neno la Mungu humo humo kwenye basi/gari, kama una gari lako mwenyewe yaani binafsi, hakikisha unafika mahali unapaki pembeni gari lako kisha unaingia kusoma Neno la Mungu.

Hadi hapo utakuwa umejifunza mengi ya kukusaidia kuondokana na sababu zisizo na msingi, Neno la Mungu iwe ndio ratiba yako kuu katika siku yako. Kosa kula chakula cha tumbo ila sio Neno la Mungu, Tafuta upenyo kwa namna yeyote ile kuhakikisha siku haipiti bila kusoma Neno la Mungu.

Mungu akubariki sana.

Chapeo Ya Wokovu

Blog: www.chapeotz.com

Email: chapeo@chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081.